Meneja wa RUWASA Wilaya ya Tandahimba Mhandisi Ndorima Kijigo akiwa katika ngazi akipanda juu ya moja ya tanki ambalo ujenzi wake uko hatua za mwisho kukamilika ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa miradi ya maji ambayo inatekelezwa kwa fedha za Ustawi maarufu kwa jina la fedha za UVIKO-19 ambazo zimetolewa na Serikali inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan.
Mhandisi Ndorima Kijigo ambaye ni Meneja wa RUWASA Wilaya ya Tandahimba akijiridhisha na ujenzi wa mradi wa maji kwa kupima vipimo mbalimbali kwa lengo la kujiridhisha wakati mafunzi wakiendelea na ujenzi wa banio la maji.
Meneja wa RUWASA Wilaya ya Tandahimba Mhandisi Ndorima Kijigo (kushoto) akiwa na moja ya mafundi wanaojenga banio la maji wakati akikagua maendeleo ya ujenzi wa mradi wa maji wa Kijiji cha Lipalwe A.
Mafundi wa ujenzi wa mradi wa maji Lipalwe A wakiwa wamebeba vifaa mbalimbali kwa ajili ya ujenzi wa mradi huo wakiongozwa na Meneja wa RUWASA Wilaya ya Tandahimba Mhandisi Ndorima Kijigo.
Mhandisi Ndorima Kijigo ambaye ni Meneja wa RUWASA Wilaya Tandahimba mkoani Mtwara akiwa ameshika daftari lenye maelezo mbalimbali ya utekelezaji wa mradi wa maji Kijiji cha Lipalwe.
Mmoja ya wasimamizi wa mradi wa Maji Lipalwe (kulia) akisaini kitabu cha wageni baada ya kufika kwenye mradi huo akiwa ameambatana na Meneja wa RUWASA Wilaya ya Tandahimba mkoani Mtwara(hayuko pichani).
RAIS wetu anaupiga mwingi!Hiyo ni kauli ya Meneja wa RUWASA Wilaya ya Tandahimba mkoani Mtwara Mhandisi Ndorima Kijigo akimuelezea Rais Samia Suluhu Hassan kutokana na fedha alizotoa kwa wananchi wa Wilaya hiyo kutekeleza Miradi ya Maji.
Akizungumza katika ziara ya kukagua miradi ya maji wilayani Tandahimba, Mhandisi Kijigo amesema kwa mara ya kwanza wananchi wa Kijiji cha Lipalwe wamepata maji safi na salama kutokana na mradi wa maji uliojengwa na Rais Samia kwa ufadhili wa fedha zilizotolewa za UVIKO-19.
Mhandisi Kijigo amesema kufikia April 30 mwaka huu wananchi zaidi ya 2,900 wa Lipalwe wataanza kunywa maji hayo baada ya mradi huo kukamilika na tayari pia wameshapokea Sh. Milioni 30 kwa ajili ya ujenzi wa kibanio.
Amesema mradi huo umegharimu kiasi cha Sh. Milioni 470 bila mabomba na utaratibu wa kununua mabomba hayo utasimamiwa na Wizara ya Maji.
“Kwa sasa tunajenga kibanio ambacho gharama yake ni zaidi ya Sh milioni 30 kwanini nasema hivyo ni kwa sababu haya maji tukiweza kuyaingiza hapa tutapeleka kwenye matenki mawili , Kuna tenki moja la lita 25000 ,hilo tenki ni kwa ajili ya kupunguza mteremko huu ili mabomba yasipasuke na tenki la pili ni la lita 50,000 ambalo sasa litakuwa kwenye Kijiji cha Lipalwe A.
“Matenki yote Wakandarasi wako kazini kama alivyo huyu hapa na wenyewe mnaweza kujionea kasi ni kubwa na tutamaliza kwa wakati,mkataba wake anatakiwa kumaliza Mei 30 mwaka huu lakini kwa spidi yake Aprili 30 tutakuwa tumekamilisha,” amesema Mhandisi Kijigo.
Ameongeza ni jambo la kushukuru kuona Serikali inayoongozwa na Rais Samia kupitia Wizara ya Maji chini ya Waziri Jumaa Aweso inatoa fedha nyingi kwa ajili ya ujenzi wa niradi ya maji kwa wananchi wake haswa maeneo ambayo hajawahi kupata maji kabisa.
“Sisi RUWASA Tandahimba kiukweli kuna miradi mingi tumefanya ,kuna mradi wa Mkwiti wa Sh.bilioni 6.4 ,Nanyula Maundo wa Sh. bilioni 4.2, mradi wa Nanyanga wa Sh milioni 230 ,Tukuyu Mdimba Sh milioni 337 na miradi yote hii tumetekeleza sisi.”
Kuhusu hali ya upatikanaji maji wilayani Tandahimba ilikuwa imeshuka hadi asilimia 46 lakini kwa sasa kupitia huu mradi wa UVIKO-19 imepanda kutokana na miradi inayoendelea kutekelezwa.
Kwa upande wake Mkandarasi wa mradi wa huo wa Maji Kijiji Cha Lipalwe Mhandisi Anold Leopard kutoka Kampuni ya Alem Construction amesema maendeleo ya ujenzi wa mradi huo yanaenda kama yalivyopangwa na wataukamilisha ndani ya muda uliowekwa.
“Pamoja na changamoto tunayoipata kutokana na miundombinu ya barabara pale mvua inaponyeesha bado tunajitahidi kwenda na muda na mpaka sasa tumefikia asilimia 80 ya ujenzi na kufikia April 30 tutakua tumekabidhi mradi.
“Nitoe shukrani zangu kwa Serikali ya Rais Samia kwa kuthamini wakandarasi wazawa na kwetu sisi hili ni deni katika kuhakikisha tunalinda Imani hiyo kwetu, tunasema asante Kwani kupitia mradi huu zaidi ya Watanzania 40 wamepata ajira.”
Mwisho.
Imeandaliwa Na: Said Mwishehe – Michuzi TV, TANDAHIMBA.