Mkazi wa kijiji cha Nanganga Fatuma Lukanga akifungua maji kwenye bomba huku baadhi ya maofisa wa RUWASA (kushoto) na Mtangazaji wa TBC Bertha Mwambela kulia wakiangalia namna maji yanavyotoka bombani
Mhandisi Laurance Mapunda ambaye ni Meneja wa RUWASA Wilaya ya Ruanga akifafanua jambo kuhusu wanavyotekeleza miradi ya maji kupitia fedha za UVIKO-19 ambazo zimetolewa na Serikali ya Awamu ya Sita ikiwa ni mkakati wa kuendelea kutatua changamoto ya uhaba wa maji kwa wananchi.
Mmoja wakazi wa Kijiji cha Nanganga akifunga koki ya maji kwa kisanduku maalum ili kuhakikisha hakuna anayeweza kuchezea bomba hilo.
Na: Mwandishi Wetu – Ruangwa
MENEJA wa Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) Ruangwa, Mhandisi Lawrence Mapunda amesema wamedhamiria kumtua ndoo mama kichwani kwa kumfikisha maji safi na salama bombani kwa umbali usiozidi mita 400.
Akizungumza kuhusu hatua ambazo zinachukuliwa na RUWASA Wilaya ya Ruangwa Mhandisi Mapunda amesema wanachokifanya RUWASA ni kuhakikisha wanatekeleza Sera ya Taifa ya Maji inayoeleza mwananchi anatakiwa kupata maji safi na salama umbali usiozidi mita 400.
Hivyo kupitia miradi inayoendelea kutekelezwa ikiwemo ya fedha za UVIKO-19 ni matumani yao wanakwenda kuondoa changamoto.
Kwa upande wake Meneja wa Mamlaka ya Maji Ruangwa Mjini Yohana Matimbwi amefafanua kwa kina ambavyo fedha za UVIKO-19 ambavyo zimekuwa zikiendelea kutekeleza miradi ndani ya wilaya hiyo.
Amesema kupitia fedha hizo wamepata Sh.milioni 313 zinatumika kuongeza mtandao wa upatikanaji maji na matarajio ya Ruangwa ni kwamba watu 3,120 watanufaika.
“Kupitia fedha hizi za UVIKO-19 Sh.milioni 313 tunaendelea na ukarabati wa tenki la maji lenye ujazo wa lita 135,000, tunaongeza mtandao wa maji wa kilomita 11.8 na kujenga vituo vya maji na hadi sasa kazi imekalimika kwa asilimia 93,”amesema.
Aidha amesema kupitia mradi huo na mingine wanatarajia Wilaya ya Ruangwa itafikia lengo la upatikanaji maji kwa asilimia 95 ifikapo 2025.”Tunaishukuru Serikali ya Awamu ya Sita kwa kutupatia fedha hizi kwa ajili ya kuongeza huduma ya upatikanaji maji.”
Wakati huo huo baadhi ya wananchi katika vijiji ambavyo miradi ya maji inatekelezwa wameeleza kufurahishwa kwao na hatua ya Serikali kuona haja ya kutatua changamoto ya maji, kwani wamepitia mateso ya muda mrefu ya kutafuta maji na wengine wamepoteza maisha kwa kulima na mamba baada ya kufuata maji mto Lukuledi.
Mkazi wa Kijiji cha Nanganga Fatuma Lukanga amesema yeye anaishi na majeraha baada ya mamba kumn’gata kwenye paja la mguu wake wa kushoto huku akieleza zaidi kuwa mjomba wake alifashafariki kwa kuliwa na mamba alipokwenda kuchota maji mtoni.
Imeandaliwa na Saidi Mwishehe Msagala, Michuzi TV
Mwisho.