Home LOCAL RAIS SAMIA AFUTA MACHOZI YA WANANCHI WALIOKUA WAKIFUATA MAJI KWA SAA TATU

RAIS SAMIA AFUTA MACHOZI YA WANANCHI WALIOKUA WAKIFUATA MAJI KWA SAA TATU

Meneja wa RUWASA Wilaya ya Newala Mhandisi Nsajigwa Sadick akimtishwa ndoo ya maji mmoja wa Wakazi wa Kijiji cha Mandara mkoani Mtwara baada ya kukamilisha ujenzi wa kituo Cha kuchotea maji katika eneo hilo.

Baadhi ya akina mama wa Kijiji cha Mandara wilayani Newala mkoani Mtwara wakiwa makini kumsikiliza maelezo yaliyokuwa yakitolewa na Meneja wa RUWASA katika Wilaya hiyo Mhandisi Nsajigwa Sadick ( hayuko pichani) kuhusu hatua mbalimbali zinazochukuliwa na Serikali ya Awamu ya Sita katika kutatua changamoto ya maji Vijijini.
 

Mwenyekiti wa Kijiji cha Mandara wilayani Newala mkoani Mtwara Ismail Lukanda akitoa shukrani za Wananchi wa Kijiji hicho kwa Rais Samia Suluhu Hassan baada ya kuwaondolea changamoto ya kufuata maji umbali mrefu.

Na: Mwandishi Wetu,Michuzi TV- Newala

WANANCHI wa Kijiji Cha Mandara wilayani Newala mkoani Mtwara wamemshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuwapelekea mradi wa maji katika Kijiji chao na hivyo kuondokana na adha ya kufuata maji umbali mrefu iliyokua ikiwakabili.

Wananchi hao wamesema wanatoa shukrani hizo kwani hapo kabla walikua wakifuata maji umbali wa saa tatu na hivyo kusababisha watoto wao ambao ni wanafunzi kukosa masomo lakini pia akina Mama kushindwa kutimiza majukumu yao ya nyumbani kwa Wakati.

Wakizungumza na wandishi wa habari walioko kwenye ziara ya kukagua ujenzi wa miradi ya maji inayotekelezwa kwa fedha za ustawi za UVIKO-19 ambazo zimetolewa na Serikali kukamilisha miradi hiyo kupitia RUWASA Wananchi wa Kijiji Cha Mandari wamesema Rais Samia aliahidi kumtua ndoo mama kichwani na kwao hilo limetekelezwa kwa kupata mradi huo wa maji.

Bishea Mohamed ambaye ni mkazi wa Kijiji hiko amesema wanashukuru kwa kupata maji katika Kijiji chao kupitia mradi wa maji ambao umejengwa kwa fedha za UVIKO-19 na ni matarajio yao kuwa watakuwa wanakunywa maji safi na salama.

” Maji ndio uhai wetu na sisi wanawake ndio kabisa, maji tunatumia kwenye kupika, kufua, kuoga, kuosha vyombo na mambo mengine kwa hiyo tunashukuru kwa kweli, tunachoomba haya maji yawepo kila siku yasiwe ya kukatika.

“Kabla ya kuja haya maji hali ilikuwa ngumu tulikuwa tunaenda bondeni kufuata maji yaani tena kama mimi ambaye ninasumbuliwa na kifua nilikuwa nikibeba ndoo moja tu kifua chote kinauma lakini sasa nitakuwa nachota maji hapa hapa nyumbani, ninamshukuru Rais Samia Suluh kwa kutuletea mradi huu na tunamuahidi katika Uchaguzi Mkuu ujao wa mwaka 2025 tutamchagua kwa kura nyingi ili aendelee kutuletea maendeleo,”amesema Bishea.

Kwa upande wake Fatma Nawanji ambaye ni  mwanafunzi wa shule ya msingi anasema kuwa anaishukuru Serikali na RUWASA kwa kupeleka maji kwenye Kijiji chao kwani baada ya maji hayo kuwa karibu na nyumba zao amekuwa akiwahi Shule tofauti na awali ambapo kabla ya kwenda shule alikuwa akifuata maji umbali mrefu.

“Sasa nachota maji hapa hapa, naoga ,nawahi shuleni, tunamshukuru Rais Samia kwani maji haya aliyoyaleta kwetu hata sisi wanafunzi hatutateseka tena,” Amesema Fatma.

Mkazi mwingine wa Kijiji Cha Mandala Shamira Mwaya amesema wanamshukuru Rais Samia kwa kupatiwa mradi huo wa maji katika Kijiji chao kwani kabla ya mradi huo wameteseka kwa muda mrefu kutokana na kufuata maji maeneo ya mbali.

“Mwanzo tulikuwa tunapata shida tulikuwa tunafuata maji Mitema ,akina mama tulikuwa tunaumia maana unakuwa na mtoto mgongoni na maji kichwani.”

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Kijiji cha Mandala Ismail Lukanda amesema kwa niaba ya Wananchi wanashukuru sana kwa kupelekewa mradi wa maji kijijini kwao, kwani kipindi cha walikuwa wanapata shida sana.

“Tulikuwa tunaenda umbali mrefu kufuata maji kwenye milima lakini sasa kwa mradi huu kwa kweli tunampongeza Mama Samia Suluhu Hassan kwa kutuletea mradi huu na niwapongeze ndugu zetu wa RUWASA ambao tumeshirikiana kwa pamoja hadi mradi huu umekamilika na sasa maji yanatoka.

Kuhusu kuutunza mradi huo amesema kwa namna ambavyo wameteseka kwa muda mrefu kufuata maji umbali mrefu  Wananchi watautunza mradi huo na kulinda miundombinu iliyopo.”Tuko tayari kuulinda mradi huu na sisi utulinde.”

Mkazi mwingine wa Kijiji cha Mandala Abdallah Mohamed amesema anaishukuru Serikali ya Rais Samia kwa kuwapatia mradi wa maji chini ya RUWASA huku akifafanua mwanzoni hali ilikuwa ngumu ,walikuwa wanafuata maji kwenye chanzo cha maji Mitema ambako walikuwa wanatumia saa tatu wakikokota madumu kwa baiskeli.

“Ukweli tumepata shida kwa miaka mingi,hakika leo tunashukuru kwa kuletewa maji karibu na nyumba zetu, tunashukuru sana Mama Samia na ikimpendeza tunaomba aje mwenyewe tumpe shukrani yetu.Baada ya maji haya kuja hatutatumia muda mwingi kutafuta maji, Watoto wetu watakuwa wanawahi shuleni maaana hata akiwa na kindoo kidogo anachukua maji.”

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here