Waziri wa Nchi Ofisi ya waziri Mkuu Sera Bunge na Uratibu Mhe. George Simbachawene (Katikati) akizungumza na Waandishi wa habari katika mkutano uliojumuisha Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais, ( Sera, Uratibu na Baraza la Wawakilishi) Zanzibar Mhe. Hamza Hasssan Juma (Kulia) na Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Dkt. Selemani Jafo kuhusu maandalizi ya sherehe hizo katika Ukumbi wa Ofisi ya Waziri Mkuu Aprili 20. 2022 Dodoma.
Baadhi ya Watendaji wa Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu) wakifuatilia mkutano wa Mawaziri na Waandishi wa habari ( hawapo pichani) kuhusu maaandalizi ya maadhimisho ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar, mkutano uliofanyika katika ukumbi wa Ofisi ya waziri Mkuu, Aprili 20, 2022 Jijini, Dodoma.
Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera Bunge na Uratibu Ndug. Kaspar Mmuya (kushoto) katika Mkutano wa Mawaziri na waandishi wa habari kuhusu maandalizi ya sherehe ya siku ya Muungano wa Tanganyika na Zanzanibar katika Ukumbi wa Ofisi ya Waziri Mkuu Aprili 20. 2022 Dodoma.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Sera Bunge na Uratibu Mhe. George Simabachawene akizungumza jambo na Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Dkt. Selemani Jafo wakati wa mkutano wao na waandishi wa habari kuhusu maandalizi ya sherehe za muungano wa Tanganyika na Zanzibar Ukumbi wa Ofisi ya Waziri Mkuu Aprili 20. 2022 Dodoma.
(PICHA NA OFISI YA WAZIRI MKUU)
(SERA, BUNGE NA URATIBU)
Na: Mwandishi wetu- Dodoma
Kulelekea kilele cha maadhimisho ya siku ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar Serikali imeandaa mashindano ya Insha kwa wanafunzi wa Shule za Msingi na Sekondari Nchi nzima (Tanzania Bara na Zanzibar) yatakayofanyika kuanzia ngazi ya Shule hadi Mkoa ambapo hadi sasa yamefikia ngazi ya Mikoa.
Hayo yamesemwa Aprili 20, 2022 na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Sera Bunge na Uratibu Mhe. George Simbachawene katika Mkutano wake na waandishi wa habari Mjini Dodoma akielezea maandalizi ya sherehe za Muungano wa Tanganyika na Zanzibar zinazotarajiwa kufanyika Aprili 26, mwaka huu.
Mhe. Simbachawene alisema mashindano yatafanyika kuanzia ngazi ya Shule hadi Mkoa ambapo Aprili 23, 2022 watapatikana washindi sita katika ngazi za Taifa kwa idadi ya washindi watatu kutoka Tanzania Bara na watatu kutoka Zanzibar.
“Washindi hawa watapatikana kutoka Shule za Msingi Tanzania Bara 1 na Zanzibar 1, Sekondari O-level Tanzania Bara 1 na Zanzibar 1 na Sekondari A-Level Tanzania Bara 1 na Zanzibar 1). Aidha, Washindi hao Sita (6) wanatarajia kukabidhiwa zawadi,”alisema Mhe. Simbachawene.
Pia Simbachawene alisema maadhimisho hayo yataambatana na utekelezaji wa shughuli za kijamii zikihusisha Mikoa, Taasisi za Serikali na vyombo vyote vya ulinzi na usalama katika maeneo yao au vikosi vyao.
“Sherehe za Mungano wa Tanganyika na Zanzibar zitafanyika Mjini Dodoma 26/04/2022 katika Ukumbi wa mikutano wa Jakaya Kikwete Convetion Centre na Mgeni rasmi anatarajiwa kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan,”alieleza.
Kwa upande wake Waziri wa wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira Dkt. Selemani Jafo alibainisha kwamba Katika kuadhimisha miaka 58 ya Muungano, Serikali itazindua andiko la historia ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar likilenga kuweka historia kwa vizazi vijavyo.
“Andiko hili linakwenda kuzinduliwa na Ofisi ya Makamu wa Rais itaendelea kutoa mafunzo baada ya Kongamano hilo, kila mtanzania aweze kupitia andiko hilo ambalo litaenda kuibua mambo mengi ambayo hayafahamiki kuhusu mchakato wa muungano,” Alisema Dkt. Jafo.
Aidha akihitimisha Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais (Sera, Uratibu na Baraza la Wawakilishi) Zanzibar Mhe. Hamza Hassan Juma alieleza kwa upande wa Zanzibar maadhimisho ya miaka 58 ya muungano yanaenda sambamba na kumbukumbu ya miaka 50 ya kifo cha Makamu wa Kwanza wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Hayati Abeid Amani Karume aliyekuwa muasisi wa muungano huo.
“Waasisi wa Muungano wetuHayati Abeid Amani Karume na Hayati Mwalimu Julius Nyerere tunajivunia mawazo yao na kujinasibu tunaendelea kuimarisha Muungano wetu na kutakuwa na Maonesho ya Muungano ambayo yatafanyika Zanzibar kuanzia tarehe 22 Aprili, 2022 hadi tarehe 6 Mei, 2022 ambayo yatahusisha Taasisi za Muungano,”alihitimisha.
MWISHO