Home LOCAL KAMPENI YA KUPAMBANA NA KIFUA KIKUU,WANANCHI MBINGA WAIOMBA SERIKALI KUFIKISHA HUDUMA HIYO...

KAMPENI YA KUPAMBANA NA KIFUA KIKUU,WANANCHI MBINGA WAIOMBA SERIKALI KUFIKISHA HUDUMA HIYO VIJIJINI

Baadhi ya wakazi wa kijiji cha Tanga Halmashauri ya Mji Mbinga mkoani Ruvuma wakiwa katika foleni kwa ajili ya kupata huduma ya uchunguzi wa vimelea vya ugonjwa wa kifua kikuu wakati wa kampeni ya kupambana na ugonjwa huo iliyofanywa na Serikali kwa kushirikiana na wadau wa maendeleo Shirika la MDH-Amref Health Africa wilayani Mbinga.


Mratibu wa kifua kikuu na ukoma wa Halmashauri ya Mji Mbinga Dkt Wenceslaus Socky kushoto akimsikiliza mkazi wa Mtaa wa Bethelehem Sipilian Samlongo aliyefika kufanya uchunguzi wa afya yake wakati wa kampeni ya mapambano dhidi ya ugonjwa wa kifua kikuu iliyofanyika kwa siku mbili katika Halmashauri ya Mji Mbinga.


Muhudumu wa Afya ngazi ya jamii(CHW) Gerold Komba akitoa elimu ya ugonjwa wa kifua kikuu kwa baadhi ya watoto wa kijiji cha Tanga Halmashauri ya Mji Mbinga waliofika katika kampeni ya uchunguzi wa ugonjwa huo iliyofanyika katika kijiji hicho.

Baadhi ya wakazi wa mtaa wa Bethelehem Halmashauri ya Mji Mbinga,wakisubiri kufanyiwa uchunguzi wa ugonjwa wa kifua kikuu iliyotolewa na wizara ya Afya kwa kushirikiana na Shirika la MDH-Amrefu Health Africa katika Mji wa Mbinga ambapo zaidi ya watu 130 walifanyiwa uchunguzi na 14 walikutwa na ugonjwa huo.

Picha na Muhidin Amri

Na: Muhidin Amri,, Mbinga

BAADHI ya wakazi  wa Halmashauri ya Mji Mbinga mkoani Ruvuma,wameiomba Serikali kupitia wizara ya afya  kuendelea kutoa huduma ya upimaji wa vimelea vya ugonjwa wa kifua kikuu kwa watu waishio vijijini kutokana na maeneo hayo kutofikiwa kiurahisi na wataalam.

Wametoa ombi hilo kwa nyakati tofauti, wakati wa kampeni ya uchunguzi wa kifua kikuu inayofanywa na wizara ya afya kwa kushirikiana na wadau wa maendeleo shirika lisilo la kiserikali la MDH-Amref Health Africa.

Kosmas Kumburu mkazi wa kijiji cha Litembo alisema,licha ya kazi nzuri inayofanywa na  wataalam wa kitengo cha kifua kikuu kuibua watu wanaougua ugonjwa huo,hata hivyo kampeni hizo hazitakuwa na tija kama zitafanyika maeneo ya mjini pekee.

Alisema, ugonjwa wa kifua kikuu upo kila mahali,lakini  maeneo ya vijijini kuna watu wengi wenye ugonjwa wa kifua kikuu kutokana na kuishi kwenye makazi holela na yasio bora, yenye mzunguko mdogo wa hewa na msongamano wa watu wengi.

Alisema,kuna wagonjwa wanaoteseka na ugonjwa huo,lakini wanashindwa kujitokeza kupima afya zao na kuanza matibabu kwa  kutopata elimu sahihi  na wengine kutokana na umaskini.

Aidha alisema,kampeni hiyo ikifanyika mara kwa mara itawezesha kuibua wagonjwa wengi wa kifua kikuu ambao wako majumbani  wakiteseka na hawajui wafanye nini na waende wapi kwa ajili ya kupata majibu ya shida zao.

Kwa mujibu wake, msaada pekeekwa watu hao ni serikali kupitia wataalam wake kufika katika maeneo hayo  kwa ajili ya kufanya uchunguzi na kuwaanzishia matibabu.

Adela Mbawala mkazi wa mtaa wa Bethelehem Mbinga mjini, ameishukuru serikali kupeleka huduma hiyo katika makazi yao kwani imetoa fursa kwa watu wengi kufanya uchunguzi wa afya zao na wale wenye matatizo kuanza matibabu.

Mratibu wa kifua Kikuu Halmashauri ya Mji Mbinga Dkt Wenceslaus Socky alisema, jumla ya watu 129 walifikiwa na huduma ya uchunguzi wa kifua kikuu kwa kutumia kliniki tembezi chini ya ufadhili wa Shirika lisilo la Kiserikali la MDH-Amref Health Africa.

Socky alisema, kati yao 14 wamekutwa na maambuizi ya ugonjwa huo na wameanzishiwa Dawa ambapo ameishukuru serikali kupitia wizara ya afya na wadau waliofanikisha kampeni ya uchunguzi wa kifua kikuu kwa wakazi wa mji wa Mbinga.

Kwa mujibu wa Dkt Socky,mwaka 2022  lengo ni kuibua wagonjwa 327,hata hivyo changamoto kubwa katika mapambano dhidi ya ugonjwa wa kifua kikuu ni uhaba wa vitendea kazi,miundombinu mibovu ya barabara hasa kipindi cha masika.

Dkt Socky alitaja changamoto nyingine ni pamoja na Halmashauri kutoweka kwenye bajeti ya mgao wa Global Fund kwa shughuli za kifua kikuu na ukoma.

Aidha alisema,katika kampeni hiyo iliyofanyika kwa siku mbili katika mtaa wa Bethelehem na kijiji cha Tanga ilikwenda sambamba na upimaji wa virusi vya ukimwi ambapo jumla ya watu 23 waliojitokeza,na 2 walikutwa na virusi vya ugonjwa huo.

Alisema,mwaka jana lengo  lilikuwa kuibua wagonjwa wa kikuu 255,lakini walivuka lengo kwa kuibuwa wagonjwa  288 kati yao watu wazima walikuwa 274 na watoto walio chini ya miaka mitano  14  ambapo  watu 6 walipoteza maisha.
MWISHO.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here