Home BUSINESS DKT. NCHEMBA AITAKA CITIBANK KUHARAKISHA TATHIMINI YA UWEZO WA NCHI KIUCHUMI

DKT. NCHEMBA AITAKA CITIBANK KUHARAKISHA TATHIMINI YA UWEZO WA NCHI KIUCHUMI

Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb), akizungumza jambo wakati ujumbe wa Tanzania ulipokutana na kufanya mazungumzo uongozi wa Benki ya Mitsubish ya Japan, kwenye Ofisi za Ubalozi wa Tanzania, jijini Washinton DC, Marekani. Kulia ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Fedha na Mipango-Zanzibar Mhe. Saada Mkuya Salum.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Fedha na Mipango-Zanzibar Mhe. Saada Mkuya Salum (Mb), akizungumza jambo wakati ujumbe wa Tanzania ulipokutana na kufanya mazungumzo uongozi wa Benki ya Mitsubish ya Japan, kwenye Ofisi za Ubalozi wa Tanzania, jijini Washinton DC, Marekani. Kushoto ni Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb).

Ujumbe wa Tanzania ukiongozwa na Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb) (wa nne kushoto), ukiwa katika picha ya pamoja na Ujumbe kutoka Benki ya Mitsubish ya Japan, katika Ofisi za Ubalozi wa Tanzania, Jijini Washington DC, Marekani. Wa pili kushoto ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Fedha na Mipango-Zanzibar Mhe. Saada Mkuya Salum (Mb), wa nne kulia ni Kiongozi wa Ujumbe wa Benki ya Mitsubish ya Japan, Bw. Christopher Marks

Ujumbe wa Tanzania ukiongozwa na Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb) (wa nne kushoto), ukiwa katika picha ya pamoja na Ujumbe kutoka Benki ya Mitsubish ya Japan, katika Ofisi za Ubalozi wa Tanzania, Jijini Washington DC, Marekani. Wa nne kulia ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Fedha na Mipango-Zanzibar Mhe. Saada Mkuya Salum (Mb). Wa pili kulia ni Kiongozi wa Ujumbe wa Citibank, Bw. Peter Sullivan.

(Picha na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini-Wizara ya Fedha na Mipango-Washington DC)

Na: Benny Mwaipaja, Washington DC.

WAZIRI wa Fedha na Mipango, Mheshimiwa Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba, ameitaka CitiBank kuharakisha mchakato wa kuifanyia Tanzania tathimini ya uwezo wake wa kukopa na kurejesha mikopo (credit rating) ili iweze kuyafikia masoko ya kimataifa yanayotoa mikopo kwa gharama nafuu.

Dkt. Nchemba alitoa rai hiyo Jijini Washington DC, Marekani, baada ya kukutana na uongozi wa Benki hiyo pamoja na Benki ya Mitsubish ya Japan, ambayo pia imeonesha nia ya kuiwezesha Tanzania kupata mikopo itakayosaidia kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo nchini.

Alisema kuwa Serikali iliahidi bungeni wakati wa Bajeti Kuu ya Serikali ya Mwaka 2021/2022 kwamba ingefanyiwa tathimini kuhusu uwezo wake wa kukopa na kulipa madeni na kuitaka Citibank na washirika wake kukamilisha kazi hiyo kabla ya mwezi Julai mwaka huu.

Dkt. Nchemba alisema kuwa Ukamilishwaji wa zoezi hilo utasaidia nchi kuweza kuyafikia masoko mbalimbali ya fedha duniani kwa gharama nafuu na kuongeza imani ya wawekezaji kwenda kuwekeza teknolojia na mitaji nchini.

Kwa upande wake Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Fedha na Mipango – Zanzibar, Mhe. Saada Mkuya Salum, alisema kuwa mazungumzo yao na Benki ya Mitsubish ya Japan yalikuwa na mafanikio makubwa ambapo Benki hiyo imeahidi kushirikiana na Tanzania kwa kuipatia mikopo ya kibiashara lakini yenye masharti nafuu.

Alisema kuwa mikopo hiyo imelenga kuharakisha utekelezaji wa miradi mikubwa ya kimkakati inayoendelea kutekelezwa nchini pamoja na miradi mipya itakayoombewa fedha ili kuharakisha utekelezaji wake kwa manufaa ya nchi.

Alitolea mfano wa mahitaji ya Zanzibar ya kutekeleza mpango wa uchumi wa buluu pamoja na ujenzi wa miundombinu itakayosaidia kuchochea maendeleo ya wananchi ikiwemo ujenzi wa bandari, viwanja vya ndege, barabara, nishati ya umeme, kuimarisha sekta ya utalii na masuala ya uvuvi.

Wakizungumza katika mikutano hiyo, Mkurugenzi Mtendaji wa Citibank Bw. Peter Sullivan, pamoja na Kiongozi wa Ujumbe wa Benki ya Mitsubish ya Japan Bw. Christopher Marks, waliahidi kuwa watahakikisha Tanzania inafikia malengo yake ya kujitathimini lakini pia kupata mikopo nafuu ya kutekeleza program mbalimbali za miradi ya maendeleo.

Waziri wa Fedha na Mipango Mheshimiwa Dkt. Mwigulu Nchemba, anaongoza ujumbe wa Tanzania kwenye mikutano ya Majira ya Kipupwe inayoendelea mjini Washington DC, Marekani ambapo pamoja na mikutano hiyo ya kawaida, ujumbe huo unakutana na taasisi na mashirika mbalimbali yanayoonesha nia ya kuwekeza fedha zao nchini Tanzania.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here