Home Uncategorized DKT. ABBASI: TUWE WATU WA KUANGALIA FURSA NA KUZITUMIA

DKT. ABBASI: TUWE WATU WA KUANGALIA FURSA NA KUZITUMIA

Katibu Mkuu wa Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo Dkt. Hassan Abbasi amewataka Maafisa Utamaduni na Michezo kuwa watu wa kuangalia fursa mbalimbali zilizopo katika sekta zao na kuhakikisha kuwa wanazitumia kwa kuzitekeleza fursa hizo.

“Tunataka Maafisa Utamaduni na Michezo wa kimkakati, kuweni wabunifu,”amesisitiza Dkt. Abbasi.

Ameyasema hayo leo tarehe 04 Aprili, 2022 wakati akifungua kikao kazi cha  Maafisa Utamaduni na Michezo wa Tanzania Bara kinachofanyika kwa siku tatu (3)  kuanzia tarehe 04 hadi 06 Aprili Jijini Dodoma.

Katibu Mkuu ameendelea kwa kuwataka Maafisa michezo kuzitumia fursa ikiwemo ya asilimia 5 ya michezo ya kubashiri ambayo ipo Baraza la Michezo la Taifa (BMT) kwa ngazi ya taifa  kwa kuja na mipango ya kazi za kutekeleza katika maeneo yao ili waweze kufaidika nazo.

Aidha, Dkt. Abbasi amewataka Maafisa Utamaduni na Michezo kuandaa mipango mikakati yao  kwa kuzingatia Ilani ya uchaguzi ya 2020, Mpango wa taifa wa miaka mitano, Sera ya Michezo na Sera Utamaduni. 

“Hizi ni sekta muhimu sana katika nchi zinazoisaidia Serikali kwa kutoa ajira kwa vijana, natamani muwe watu wa kubadilika ili tufike mbali,”alisisitiza.

Dkt. Abbasi amesema kuwa, sekta ya Michezo imekuwa na mafanikio  makubwa sana Kimataifa ambapo kwa mwaka huu mwezi Julai hadi Agosti kuna michezo inayoiwakilisha nchi katika michezo ya Jumuiya ya Madola ikiwemo Riadha, Judo, Kuogelea, Ngumi na Wanyanyua vitu vizito kwa watu wenye ulemavu.

Pia, timu ya mpira wa miguu kwa watu wenye ulemavu (Tembo Worriors) itaiwakilisha nchi katika michezo ya dunia nchini Uturuki, huku tarehe 03 Aprili, 2022 Alphonce Simbu ameshika nafasi ya tatu (3) katika mbio za Milano nchini Italia.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here