Home LOCAL BUNGE LAPITISHA BAJETI YA OR – TAMISEMI YA TILIONI 8.8/-

BUNGE LAPITISHA BAJETI YA OR – TAMISEMI YA TILIONI 8.8/-

 

NA: ANGELA MSIMBIRA, OR-TAMISEMI

BUNGE la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania limepitisha bajeti ya Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OR-TAMISEMI), Tume ya Utumishi wa Walimu, Mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa kwa mwaka wa Fedha 2022/2023 shilingi trilioni 8.779.
Akitoa maelezo kuhusu hoja za wabunge zilizojitokeza wakati wa kujadili hotuba ya bajeti ya Ofisi ya Rais –TAMISEMI kwa mwaka wa Fedha 2022/2023 Waziri Bashungwa amesema, Serikali imetoa kiasi cha Shilingi bilioni 5.0 kwa ajili ya kuboresha maeneo ya kufanyia biashara wafanyabiashara ndogo ndogo (machinga) katika halmashauri 11 nchini.

Waziri Bashugwa ameendelea kufafanua kuwa, majadiliano na Wizara ya Fedha na Mipango yanaendelea ili kufanya marekebisho ya Sheria ya Fedha za Serikali za Mitaa Sura 290 kuruhusu sehemu ya fedha za mikopo ya asilimia 10 kutumika katika kuboresha miundombinu ya Machinga, ambapo Shilingi bilioni 38.01 zitapatikana kupitia eneo hilo na kuwezesha ujenzi na uboreshaji wa miundombinu ya wafanyabiashara wadogo hao.

Waziri Bashungwa amesema, katika mwaka wa fedha 2022/2023 Serikali imetoa kibali cha ajira za watumishi wa Sekta ya Elimu na Afya 17,412 ambapo nafasi 9,800 ni za walimu na 7,612 ni za kada za afya na kuwataka Watanzania wenye sifa kuanza kuomba na kusisitiza kuwa asilimia tatu (3%) ya ajira hizo ni kuajili ya watu wenye Ulemavu kulingana na Sheria.

Amewaagiza Mameneja wa TARURA wa Mikoa na Wilaya kuhakikisha wanawashirikisha Wadau ikiwa ni pamoja na Waheshimiwa Wabunge wakati wa kuainisha vipaumbele na kuhakikisha katika mwaka wa fedha 2022/23, ununuzi wa kazi utaanza mwanzoni mwa mwezi Mei, 2022.

Kuhusu uboreshaji ugawaji wa rasilimali fedha Waziri Bashungwa amesema, TARURA inafanya mapitio ya fomula itakayotumika katika kugawa rasilimali fedha za ujenzi na matengenezo ya miundombinu ya barabara kulingana na hali ya maeneo husika.

Aidha, Waziri Bashungwa amesema katika mwaka wa fedha 2022/23 Serikali imeongeza bajeti ya matumizi mengineyo katika Ofisi za Wakuu wa Mikoa kutoka Shilingi bilioni 57.44 hadi Shilingi bilioni 79.09 ili kuwezesha utekelezaji wa majukumu ya Ofisi hizo, ikiwemo ufuatiliaji na usimamizi wa shughuli za Mamlaka za Serikali za Mitaa.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here