Home LOCAL BAJETI YA EAC MWAKA 2022/2023 KUWA USD MILIONI 91.6

BAJETI YA EAC MWAKA 2022/2023 KUWA USD MILIONI 91.6

Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb), na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Liberata Mulamula, wakisikiliza taarifa kwa ajili ya Mkutano Maalumu wa 47 wa Baraza la Mawaziri wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, iliyosomwa na Katibu Mkuu wa  Wazara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Joseph Sokoine (hayupo pichani), Jijini Arusha.

Katibu Mkuu wa Wazara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Joseph Sokoine, akiwapitisha Mawaziri kwenye taarifa ya Mkutano Maalumu wa 47 wa Barazala Mawaziri wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, Jijini Arusha. Wanaomsikiliza ni Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb) (kushoto), Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Liberata Mulamula (katikati) na Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango, Bw. Emmanuel Tutuba (kulia).
 
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Liberata Mulamula akizungumza jambo baada ya Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Joseph Sokoine kuwapitisha kwenye taarifa ya Mkutano Maalumu wa 47 wa Baraza la Mawaziri wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, Jijiji Arusha. Kulia kwake ni Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb).
 
Naibu Waziri, Ofisi ya Rais Utumishi na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi (katikati), akifuatilia kwa umakini Mkutano Maalumu wa 47 wa Baraza la Mawaziri wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, uliojadili kuhusu bajeti ya Jumuiya hiyo pamoja na kujaza nafasi za ajira katika Jumyuiya hiyo, Jijini Arusha.
Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango na Mlipaji Mkuu wa Serikali Bw. Emmanul Tutuba, (kushoto)), akifuatilia kwa umakini Mkutano Maalumu wa 47 wa Baraza la Mawaziri wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, uliojadili kuhusu bajeti ya Jumuiya hiyo pamoja na kujaza nafasi za ajira katika Jumyuiya hiyo, Jijini Arusha.

(Picha na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini – Wizara ya Fedha na Mipango- Arusha)

Na: Benny Mwaipaja, WFM, Arusha

Baraza la Mawaziri wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) limetoa mapendekezo ya bajeti ya jumla ya dola za Marekani milioni 91.6 kwa mwaka wa fedha 2022/2023 ambapo kati ya fedha hizo, dola za Marekani milioni 37.5 zinatarajiwa kutolewa na wadau wa maendeleo.

Mapendekezo hayo yametolewa kwenye Mkutano Maalum wa 47 wa Baraza la Mawaziri wa Jumuiya hiyo uliofanyika katika Ofisi za Makao Makuu ya Jumuiya hiyo, jijini Arusha.

Akizungumza kuhusu Mkutano huo, Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango ambaye pia ni Mlipaji Mkuu wa Serikali Bw. Emmanuel Tutuba alisema kuwa Bajeti inayopendekezwa imezingatia kubana matumizi na kuelekeza fedha nyingi kwenye miradi ya maendeleo ya Jumuiya hiyo.

Mapendekezo ya Bajeti ya Jumuiya hiyo inayoundwa na nchi sita wanachama, ikiwemo Tanzania, Kenya, Uganda, Burundi, Rwanda na Sudani Kusini kwa mwaka wa fedha 2022/2023, ni sawa na Bajeti ya mwaka wa fedha uliopita 2021/2022 na yamebaki hivyo kutokana na changamoto inayopitiwa na Nchi Wanachama katika kukabiliana na madhara ya UVIKO-19.

Baraza hilo limependekeza kuwa kiasi cha dola za Marekani milioni 54.1 kitumike kwa ajili ya mihimili ya Sekretarieti ikiwemo Mahakama ya Afrika Mashariki, Bunge la Afrika Mashariki na Taasisi zake ikiwemo Tume ya Sayansi na Teknolojia ya Jumuiya ya Afrika Mashariki (EASTECO) na Tume ya Bonde la Ziwa Victoria (LVBC).

Taasisi nyingine ni Tume ya Kiswahili (EAKC), Tume ya Utafiti wa Afya (EAHRC) na Mamlaka ya Ushindani ya Jumuiya hiyo (EACA); dola za Marekani 644,219 ni kwa ajili ya Baraza la Vyuo Vikuu Afrika Mashariki (IUCEA) na dola za Marekani 465,500 zitaelekezwa kwa ajili ya kutekeleza majukumu ya Taasisi ya Uvuvi ya Ziwa Victoria (LVFO).

Aidha, Baraza hilo Maalum la Mawaziri limependekeza Bajeti ya mwaka 2022/2023 igharamie utekelezaji wa miradi ndani ya Jumuiya, ikiwemo, awamu ya pili ya Ujenzi wa Makao Makuu ya Baraza la Vyuo Vikuu Afrika Mashariki (IUCEA), Matengenezo ya Meli ya Utafiti katika Ziwa Victoria ijulikanayo kama RV Jumuiya, Ujenzi wa Awamu ya Pili ya Makao Makuu ya Tume ya Bonde la Ziwa Victoria (LVBC) na Kuwezesha zoezi la uangalizi wa Uchaguzi Mkuu nchini Kenya.

Aidha, Mkutano huo Maalum wa 47 wa Baraza Maalum la Mawaziri wa EAC umepitia na kujadili taarifa ya Kamati ya Fedha na Utawala na Taarifa ya matokeo ya zoezi la usaili wa watumishi wapya wanaotarajiwa kuajiriwa katika Jumuiya hiyo.

Mkutano huo Maalum ulitanguliwa na mikutano ya awali ambayo ni; Mkutano Ngazi ya Wataalamu uliofanyika tarehe 4 Aprili 2022 na Mkutano Ngazi ya Makatibu Wakuu uliofanyika tarehe 5 Aprili 2022.

Ujumbe wa Tanzania katika mkutano huu umeongozwa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Liberata Mulamula ambaye ameambatana na; Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Mwigulu Nchemba, Naibu Waziri, Ofisi ya Rais Utumishi na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi na Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Dkt. Evaristo Longopa.

Mwisho

Previous articleVIONGOZI WA KAMATI YA AMANI MKOA WA MWANZA WAPEWA ELIMU JUU YA UMUHIMU WA ANWANI ZA MAKAZI
Next articleSINGIDA WAANZA KUTATUA CHANGAMOTO ZA ELIMU KWA WATOTO WADOGO
Hughes Dugilo is a Writer, News Producer, Video-Photographer Journalist, and Video Editor experienced for 20 years now performing in News, Documentary, Advertisements and Television Programs. Aside from all above he own and operate his Blog known as Green Waves Media TZ since 2018.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here