Home LOCAL ANWANI ZA MAKAZI, NJIA SAHIHI YA TANZANIA KUFIKIA UCHUMI WA KIDIGITALI

ANWANI ZA MAKAZI, NJIA SAHIHI YA TANZANIA KUFIKIA UCHUMI WA KIDIGITALI

 

Na: Mwandishi Wetu.

Anwani za Makazi ni mfumo unaotambulisha mahali halisi ambapo mtu anaishi, mahali ilipo biashara yake au ofisi anayofanyia kazi kwa kufuata jina la barabara na mtaa, namba ya nyumba au jengo pamoja na Postikodi. Postikodi au simbo za posta kama inavyotambulika ni mfumo maalum wa tarakimu unaotambulisha eneo la kufikisha huduma za posta ambapo kwa nchi ya Tanzania inaanzia katika ngazi ya kata, wilaya, mkoa na kanda.

Serikali kupitia Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari kwa kushirikiana na Ofisi ya Rais TAMISEMI na Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi inatekeleza mradi wa Anwani za Makazi na Postikodi nchini lengo likiwa ni kurahisisha mawasiliano, ufikishaji wa huduma za Serikali kwa wananchi na kufanyika kwa shughuli za kijamii, kiuchumi na kiutawala.

Kuna aina tatu kuu za anwani zinazotumika ulimwenguni ambazo ni anwani za kijiografia, anwani za posta na anwani za Makazi. Anwani za Kijiografia ambazo huitwa pia anwani za maeneo hutumia mifumo ya urejeleaji (kwa mfano longitudo na latitudo) kutoa maelezo sahihi na ya kudumu ya mahali kitu kilipo duniani (mfano ni 10º 44’ 50” Latitudo Kaskazini na 20º 15’ 45” Longitudo Mashariki).

Aina ya pili ni Anwani ya Posta hutumia taarifa za mahali halisi ili kufikisha bidhaa za kiposta au kifurushi (mfano: Sanduku la Posta); na hatimae ni Anwani ya makazi ambayo hutumia majina ya barabara/ mitaa na namba za nyumba kuonesha mahali sahihi, kamili, pa kudumu na mahususi kitu kilipo (kwa mfano: anwani za maeneo na milki). Anwani za makazi hutumia mfumo wa utambulisho wa barabara/ mitaa, majina ya majengo, nambari za nyumba, kielelezo kama vile Postikodi.

Manufaa ya Mfumo wa Anwani za Makazi

Anwani za makazi zitaiwezesha nchi yetu kufikika kirahisi. Aidha utawawezesha wananchi kushiriki katika uchumi wa Kidijitali, kwamba wananchi wataweza kufanya biashara kati yao na nje ya nchi kwa kuzingatia kuwa mizigo inaweza kutumwa pale mtu alipo au kutumiwa mzigo ukamfikia pale alipo. Aidha mfumo wa anwani za makazi na Postikodi utawezesha kila raia kuwa na anwani halisi ya makazi tofauti na ilivyokuwa awali ambapo suala la anwani lilikuwa uchaguzi wa mtu binafsi; kwa utaratibu huu wa Anwani za makazi kila biashara inayosajiliwa Tanzania itakuwa na anwani halisi, utambulisho wa watu wanaoishi katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania utarahisishwa, pia usajili wa mali, biashara, vizazi na vifo utaboreshwa, Huduma za dharura, kama vile polisi, zimamoto na magari ya wagonjwa, zitaweza kutambua maeneo yenye dharura na kuyafikia kwa haraka na urahisi zaidi. Aidha wageni wataweza kubaini mahali wanakokwenda kwa urahisi zaidi badala ya kuuliza mara kwa mara uelekeo wa kule waendako.

 

Kwanini viwango vya uwekaji Anwani za makazi, Postikodi na namba ufanane

Uwekaji wa Anwani za makazi unalindwa na taratibu za Kimataifa ambazo zimeridhiwa na nchi wanachama wa Umoja wa Posta Duniani. Viwango stahiki vya uwekaji Anwani za makazi na Postikodi vinapaswa kuzingatiwa na nchi zote wanachama. Tanzania ina Mwongozo wa Mfumo wa Anwani za Makazi uliotolewa na Ofisi ya Rais-TAMISEMI unaoelekeza hatua na taratibu za kufuatwa wakati wa uwekaji Anwani za makazi nchini. Hivyo viwango vya uwekaji wa Anwani huzingatia taratibu za Kimataifa na kinchi kwa kadri zinavyoelekeza. 

Aidha viwango vya mfumo wa anwani wa Taifa kwa ajili ya Tanzania vimewekwa kwa kuzingatia Mwongozo wa kiwango cha Kimataifa (S42) cha Umoja wa Posta Duniani (PAPU). Umoja wa Posta Duniani ni Shirika la Umoja wa Mataifa lenye dhamana ya maendeleo ya sekta ya Posta duniani, pia ni msingi wa ushirikiano baina ya watoaji wa huduma za posta duniani. Umoja huu unasaidia kujenga mtandao wa uhakika duniani unaohakikisha utoaji wa huduma za kisasa za Posta. Kwa njia hii, shirika linafanya kazi za kushauri, kupatanisha, na kutoa msaada wa kitaalamu kila upohitajika. 

Umuhimu wa Viwango vya Mfumo wa Anwani.

Lengo la viwango vya mfumo wa anwani ni kuwasaidia watoa huduma za posta na huduma nyinginezo zikiwemo za dharura na biashara, kutoa huduma kwa ufanisi, usahihi, na kwa wakati, hivyo kupunguza uwezekano wa hasara na upotevu wa namna yoyote uwe wa mali, muda au maisha na hatimae kumwezesha mpokeaji huduma kuipata bila vikwazo.

Viwango katika zoezi la Anwani ni muhimu kwa kuwa vinarahisisha mawasiliano – Moja ya vipengele muhimu vya mafanikio ya uwekaji viwango katika zoezi la utoaji wa Anwani ni Kuwezesha mawasiliano yenye mpangilio bora uliohifadhiwa. 

Uhakika wa huduma; kwa wafanyabiashara hasa katika zama hizi za TEHAMA biashara-mtandao ndiyo mtindo muhimu wa ufanyaji biashara kwa sasa; katika mtindo huu muhimu wa maingiliano ya kiuchumi baina ya muuzaji na mnunuaji unahitajika uhakika kwa mnunuzi kuwa ataipokea bidhaa yake kutoka kwa mnunuzi bila kuchelewa, hili linawezekana ikiwa mpokeaji au mnunuaji ana Anwani inayomwezesha muuzaji kumfikia kwa urahisi. 

Utaratibu wa Utoaji wa Jina la Barabara au Mtaa

Ili kuipa majina mitaa au Barabara mtaa utashirikisha wadau wote wa eneo husika hususan wakazi wa eneo hilo. Meneja wa Kitengo cha Huduma za Posta katika Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) Haruni Lemanya, alisisitiza kuwa utaratibu huu ni muhimu kuzingatiwa kwa kuwa unaondosha uwezekano wa migogoro miongoni mwa wadau wa mtaa husika. 

“Suala la utoaji majina ya mitaa na Barabara ni muhimu sana kuwa shirikishi kwa kuwa barabara ni miundombinu ya umma; na Anwani za makazi ni suala linaloigusa jamii nzima” alisisitiza na kuongeza Lemanya.

Utaratibu wa utoaji majina ya mitaa na Barabara utaanzia katika ngazi ya mtaa/kitongoji na kuendelea katika Ngazi ya Kijiji, Kamati ya Maendeleo ya Kata, Kamati ya Kudumu inayohusika na masuala ya mipango miji na mazingira na hatimaye Baraza la Madiwani. Mwongozo wa Anwani za Makazi umebainisha kuwa Halmashauri itawajibika kutoa taarifa kwa wadau wote juu ya majina ya mitaa yaliyoidhinishwa na kuingizwa katika Daftari la Kudumu la Majina ya Barabara/mitaa katika Halmashauri husika.

Katika Mkutano kazi na Wakuu wa Mikoa uliofanyika mwezi Februari jijini Dodoma mwaka huu Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan alisisitiza kuwa ni muhimu wananchi wakashirikishwa katika kila hatua ya mradi wa Anwani za makazi. 

“Kwa hiyo tukiwashirikisha vizuri wananchi, hili zoezi litakwenda kuwa rahisi na halina ughali ule ambao tuliutarajia wa kitaalam” alisisitiza Rais Samia Suluhu.

Wakuu wa Wilaya wanena kuhusu utaratibu wa kupata majina ya mitaa na Barabara 

Katika maeneo mengi hasa mijini majina ya mitaa na Barabara hutegemea zaidi umaarufu wa mtu, kitu au jiografia ya mahali husika kwa mfano wakati wa eneo lenye mwinuko wanaweza kuita eneo lao ‘Kilimani’ eneo ambalo anaishi mwanamaji maarufu pakapewa jina ‘kwa baharia’ nakadhalika; aidha ikiwa mkazi mmoja akaanza kujenga akiwa wa kwanza kwenye mtaa husika huweza kuamua kuupa mtaa jina lake mfano ‘mtaa wa kwa Komba’. Pamoja na utaratibu huo uliozoeleka Mwongozo wa Anwani za makazi umeweka utaratibu unaoambatana na maelekezo ya serikali jinsi ya kutoa majina ya mitaa na barabara. 

Utaratibu wa upatikanaji wa majina ya mitaa upo katika Mamlaka ya wananchi kupitia Mamlaka za serikali za mitaa kama inavyoelekezwa kwenye Mwongozo wa Anwani.

Akizungumza na Mwandishi wa Makala hii Mkuu wa Wilaya ya Ubungo Kheri James alisisitiza kuwa Wilaya anayoiongoza inazingatia utaratibu unaotumika katika kupata majina ya mitaa kama ulivyobainishwa kwenye mwongozo ambapo jina la mtaa litatoka kwa wananchi kupitia mkutano mkuu wa mtaa au kitongoji husika.

“Watu wengine wanaweza kuchagua jina la mtu kutokana na kusaidia jamii hiyo kama kujenga barabara na wakati huo huo na yeye kuwa mkazi wa mtaa au kitongoji” alisisitiza James.

Shauku ya serikali awamu ya sita ni kuona Mfumo wa Anwani za Makazi unakamilika ifikapo mwezi Mei 2022. Tayari jitihada za makusudi zinafanywa kote nchini chini ya Usimamizi wa Wizara Zenye dhamana ikiwa ni pamoja na kuweka mazingira wezeshi; kwa mfano mfumo huu unapatikana kupitia programu tumizi ya simu za mkononi inayoitwa NAPA Mobile App ambayo inaingizwa taarifa zote za makazi ya watu, majengo ya ofisi za Serikali na Binafsi, barabara, njia, majina ya vituo vinavyotoa huduma za kijamii kama hospitali, shule, zahanati n.k inafanya kazi kama google map, ambapo mwananchi anaweza kuingia kwenye programu hiyo kupitia simu ya mkononi na kuandika mahali anapotaka kwenda kutoka mahali alipo kwa muda huo na programu hiyo itamuonesha njia ya kupita mpaka kufika sehemu husika. Ushiriki wa kila raia ni muhimu katika Kuwezesha zoezi hili kukamilika katika kuijenga Tanzania ya Kidijitali ambapo serikali kupitia Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania inasimamia mfumo wa Anwani za makazi na Postikodi katika kuhakikisha Tanzania inakuwa ya kisasa pasipo kuachwa kwenye kujenga uchumi wa Kidijitali unaoendana na mabadiliko ya TEHAMA.  

 

 

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here