Home LOCAL WIZARA YA AFYA ZANZIBAR KUTOA MAFUNZO

WIZARA YA AFYA ZANZIBAR KUTOA MAFUNZO

Waziri wa Afya Zanzibar Mhe.Nassor Ahmed Mazrui akizungumza na Ujumbe kutoka Shirika la misaada la Marekani kuhusu maswala ya Ukimwi mara walipofika Ofisini kwake Mnazimmoja kujitambulisha na kujadiliana mambo mbalimbali ikiwemo kuwapatia misaada walioathirika na Virusi hivyo.

Waziri wa Afya Mhe.Nassor Ahmed Mazrui akimpatia maelekezo mjumbe kutoka shirika la misaada la Marekani ambao wanajishughulisha na maswala ya Ukimwi Michele Chevalier kuhusu matumizi ya karafuu kabla ya kumkabidhi kama zawadi maalum kutoka kwa Waziri huyo ,alipofika na ujumbe wake katika Ofisi za Wizara ya Afya Mnazimmoja kujitambulisha .

PICHA NA FAUZIA MUSSA –MAELEZO ZANZIBAR.

NA: SABIHA KHAMIS ,MAELEZO  

Waziri wa Afya Nassor Ahmed Mazrui amesema Wizara yake inakusudia kuimarisha maabara na kuwapatia mafunzo wafanyakazi wa sekta ya afya ili waweze kutoa huduma bora kwa wananchi.

Akizungumza na Ugeni kutoka Shirika la Misaada Marekani ambao wanawakilisha OGAC na CDC huko ofisini kwake Mnazi Mmoja amesema kupitia Shirika hilo watakuwa mstari wa mbele katika kupambana na maambukizi ya UKIMWI.

Amesema wafanyakazi watapatiwa mafunzo ya kuwajengea uwezo wa kufanya utafiti ili kuongeza kiwango cha utoaji huduma na kuimarisha sekta ya afya nchini.

“Katika kuwajenga katika kuimarisha huduma za afya kwa wananchi ni kuwajengea uwezo wafanyakazi wa kufanya utafiti ambao utasaidia katika kutoa huduma bora kwa jamii”, alisema Waziri Mazrui.

Ameeleza kuwa kupitia Shirika hilo wamekuwa mstari wa mbele katika kupambana na UKIMWI nchini, hivyo ameomba kuwepo na ushirikiano wa kutosha  ili kutokomeza janga hilo.

“Ni kweli hivi sasa tuna waathirika wa UKIMWI 7600, waathirika 400 kwa mwaka 2020 hadi 2021 hichi si kiwango kidogo katika Nchi yetu”, amesema Waziri Mazrui.

Waziri Mazrui amesisitiza jamii kuongeza juhudi ya kutoa ushauri kwa walioathirika wasiwaambukize wengine, kuwapatia matibabu kwa wale walioathirika ili waendelee kuishi vizuri.

Hata hivyo Waziri Mazrui amesema wapo katika ujenzi wa hospital 10 za Wilaya na moja ya Mkoa ambazo zina malengo ya kutoa huduma bora za afya kwa jamii  na jukumu kuu la sekta ya Afya ni kuimarisha  afya za wananchi.

Amefahamisha kuwa katika kupambana na maradhi ya kuambikiza Mke wa Rais Mama Maryam Mwinyi yupo mstari wa mbele katika kupambana na kupinga maambukizi ya UKIMWI nchini.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Ujumbe huo Michelle Chevalier amesema lengo la Shirika hilo ni kuweka mashirikiano ya karibu na sekta ya Afya katika mapambano ya kujikinga na maradhi ya UKIMWI, viashiria vya maradhi hayo pamoja na kuwapatia huduma waathirika.

Vile vile ameahidi kuweka mashirikiano katika suala zima la kuzuia maradhi ya UKIMWI na mengine makubwa yakiwemo Saratani kwa wanawake na watoto.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here