Home LOCAL WATU 2,926 WAKUTWA NA KIFUA KIKUU MKOANI RUVUMA

WATU 2,926 WAKUTWA NA KIFUA KIKUU MKOANI RUVUMA

Mratibu wa kifua kikuu na ukoma wa mkoa wa Ruvuma Dkt Xavier Mbawala akitoa taarufa ya hali ya ugonjwa wa kifua kikuu katika mkoa huo wakati wa maadhimisho ya siku ya kifua kikuu Duniani ambayo kimkoa yalifanyika kijiji cha Tingi wilayani Nysasa.

Baadhi ya wananchi wa kijiji cha Tingi wilayani Nyasa wakimsikiliza mratibu wa kifua kikuu na ukoma wa mkoa wa Ruvuma Dkt Xavier Mbawala(haypo pichani)wakati wa Siku ya Maadhimisho ya ugonjwa wa kifua kikuu Dunia ambayo kimkoa yalifanyika katika kijiji hicho,


Kaimu Mganga Mkuu wa mkoa wa Ruvuma ambaye ni Mganga Mkuu wa wilaya ya Mbinga Dkt Klint Nyamryakung’e akizungumza na wananchi waliojitokeza katika maadhimisho ya siku ya kifua kikuu Duniani ambayo katika mkoa wa Ruvuma yalifanyika kijiji cha Tingi wilyani Nyasa.

Wanafunzi wa shule ya Sekondari Tingi kata ya Tingi wilayani Nyasa wakiimba wimbo maalum wenye ujumbe wa kuhamasisha jamii kujitokeza kupima ugonjwa wa TB ili kufahamu afya zao.

Picha zote na Muhidin Amri,


Na Muhidin Amri,
Nyasa

JUMLA ya watu 2,926 walikutwa na maambukizi ya ugonjwa wa kifua kikuu kwa mwaka 2021 kati yao watoto kuanzia umri wa miaka 0-14 walikuwa 721 na wenye virusi vya ukimwi ni 329 mkoani Ruvuma.

Hayo yamesemwa na Mratibu wa kifua kikuu na ukoma wa mkoa huo Dkt Xavier Mbawala, wakati akitoa taarifa ya utekelezaji wa shughuli za kudhibiti ugonjwa TB katika maadhimisho ya siku ya kifua kikuu Duniani ambayo kimkoa ilifanyika kijiji cha Tingi wilayani Nyasa.

Dkt Mbawala alisema kuibuliwa kwa watu hao kunatokana na kampeni za zinazofanyika za kuhamasisha,kutoa elimu na kufanya uchunguzi  katika maeneo mbalimbali ya mkoa huo  zinazofanywa na wataalam wa kitengo cha kifua kikuu na ukoma.

Alisema,mwaka 2019 mkoa wa Ruvuma ulipewa malengo  ya  kuibua wagonjwa 1896 lakini walivuka lengo na kuibua wagonjwa 1807 kati  ya hao watoto walikuwa 282,wenye virusi vya ukimwi 389  na mchango kutoka ngazi ya jamii walikuwa 1332.

Aidha alisema,mwaka 2020 walifanikiwa kuvuka  kwa kuibua wagonjwa 4,264 kati ya lengo la  kuibua wagonjwa 1984 ambapo watoto walikuwa 497 na wenye virusi vya ukimwi walikuwa 415na mchango ngazi ya jamii ni wagonjwa 1603.


Pia alisema,mkoa wa Ruvuma una jumla ya vituo vya kutolea huduma za afya 354 kati ya hivyo 13ni Hospitali,27 vituo vituo vya afya na 314 ni zahanati ambapo vituo vyenye uwezo wa kutoa  matibabu ya kifua kikuu ni 304 sawa na asilimia 86.


Kwa mujibu wa Dkt Mbawala,vituo vyenye uwezo wa kupima na kugundua kifua kikuu ni 73,vituo vyenye gene Xpert ni 9 na vituo vyenye Hadubini ni 73 na vyenye X-ray  13.


Dkt Mbawala alisema, mafanikio kutokemeza ugonjwa huo katika mkoa wa Ruvuma yamepatikana kutokana ushiriki wa  wadau ikiwamo Shirika lisilo la Kiserikali la MDH katika kutekeleza shughuli  za kudhibiti ugonjwa huo.


Alisema, shirika hilo limekuwa na mchango mkubwa katika suala zima la kampeni ya mapambano ya kifua kikuu kwa kutoa posho kwa wahudumu ngazi ya jamii,waganga wa tiba asili,na waendesha boda boda  wanaosafirisha sampuli za makohozi.

Alitaja mchango mwingine unaotolewa na MDH, ni  kutoa mafunzo kwa watumishi wa afya juu ya maboresho katika kugundua wagonjwa kwenye vituo vya afya,mafunzo kwa watoa huduma,wamiliki wa maduka ya dawa na Pharmacy na kugharamia usimamizi shirikishi na mafunzo kazini kwa watumishi wa afya.

Kwa upande wake  Mganga Mkuu wa mkoa wa Ruvuma Dkt Jairy Khanga ambaye aliwakilishwa na Mganga Mkuu wa wilaya ya Mbinga Dkt Klint Nyamryakung’e ameziagiza Hospitali za wilaya  katika mkoa huo kuongeza mikakati ya pamoja katika mapambano  dhidi ya ugonjwa wa kifua kikuu.

Alisema,mikakati hiyo ijikite katika kuwagundua wagonjwa mapema kwa kuhakikisha wataalam wanachukua vipimo vya makohozi kutoka kwa wahisiwa na kufikisha mapema maabara ili kubaini uwepo wa vimelea vya ugonjwa huo  na watakaobainia waanzishiwe matibabu mapema.

Alisema,ugonjwa wa kifua kikuu ni kati ya magonjwa hatari ya kuambukiza ambayo huathiri wananchi wa  vijijini na mjini na husababisha vifo vingi kwa jamii ambayo ni nguvu kazi inayotegemewa katika uzalishaji mali na shughuli nyingi za kiuchumi katika Taifa letu.
MWISHO.

 

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here