Na: Mwandishi Wetu
SERIKALI imefanikiwa kuongeza umiliki wa hisa katika Kampuni ya Madini ya Almasi ya Williamson kutoka asilimia 25 hadi asilimia 37.
Aidha, kufikia Machi mwaka huu, Serikali imesaini mikataba ya ubia na kumiliki asilimia 16 ya hisa zisizohamishika kwa kampuni tano za madini. Kampuni hizo ni Black Rock Mining Limited; Strandline Resources Limited; Petra Diamonds Limited; Nyanzaga Mining Limited na LZ Nickel Limited.
Kauli hiyo imetolewa na Msajili wa Hazina, Mgonya Benedicto akielezea mafanikio ya Serikali Awamu ya Sita katika kipindi cha mwaka mmoja ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan.
Akifafanua zaidi kazi zilizofanyika, alisema pia kwamba vyeti vya umiliki wa hisa vya Kampuni za Faru Graphite Corporation, Sota Mining Corporation, Williamson Diamond Limited (Class A & Class B Shares), Nyati Minerals Limited pamoja na Tembo Nickel Refining Limited vilisainiwa na kukabidhiwa kwa Serikali.
Akielezea mafanikio ya awamu ya sita katika kipidni cha mwaka mmoja Msajili wa Hazina, alisema wamekuwa na mafanikio makubwa katika kutekeleza Kifungu cha 10 cha Sheria ya Madini, Sura 123 kuhusu hisa zisisohamishika za serikali zinazowezesha umiliki.
Ofisi ya Msajili wa Hazina, kutokana na wajibu wake imewezesha Serikali kumiliki hisa katika Kampuni za Madini zisizopungua asilimia 16 (undilutable 16% Free Carried Interest).
Utekelezaji wa Kifungu cha 10 cha Sheria ya Madini, Sura 123 kuhusu hisa zisizohamishika umeendelea kuiwezesha Serikali kuwa na hisa katika baadhi ya kampuni za madini pamoja na kuongeza umiliki kwenye baadhi ya kampuni katika kipindi kinachoishia Machi 2022.
Akizungumzia ulipaji wa pensheni kwa Wastaafu waliokuwa chini ya Jumuiya ya Afrika Mashariki, alisema kuanzia Machi 2021 hadi Machi 2022, Serikali imelipa jumla ya Sh bilioni 8.7 kwa wastaafu hao ambao walikuwa hawajaanza kulipwa kiwango cha chini cha pensheni (Minimum Pension) kwa mujibu wa Tangazo la Serikali la Mwaka 2009 na 2015.
Alisema kati ya fedha hizo, kiasi cha Sh bilioni 1.77 zimetumika kulipa wastaafu 992 wa Shirika la Reli (TRC), Sh milioni 798.62 wastaafu 267 wa Shirika la Posta (TPC), Sh bilioni 6.2 wastaafu 848 wa TTCL. Aidha, kati ya fedha zote zilizolipwa kwa TTCL kiasi cha Sh bilioni 4.77 ni malimbikizo ya nyongeza ya pensheni kwa wastaafu 636 kwa kipindi cha 2009 hadi Februari 2022.
Msajili huyo alisema kwamba Ofisi ya Msajili wa Hazina kama msimamizi mkuu wa uwekezaji wa Serikali kwa niaba ya Rais itaendelea kusimamia kwa karibu utendaji wa Mashirika na Taasisi za Umma ili kuhakikisha kuwa Serikali inapata faida ya uwekezaji wake sambamba na kuongezeka kwa mapato yasiyo ya kodi ili kusaidia miradi ya maendeleo kwa faida ya Taifa na wananchi wote kwa ujumla.
Mwisho