Home LOCAL WALEMAVU SUMBAWANGA WASHUKURU SERIKALI KWA MIKOPO

WALEMAVU SUMBAWANGA WASHUKURU SERIKALI KWA MIKOPO

Mwenyekiti wa CCM mkoa wa Rukwa Ndugu Rainer Lukala (kulia) akiongea na walemavu waliopata mkopo wa halmashauri juzi wakati Kamati ya Siasa Mkoa ilipotembelea kijiji cha Ilemba Sumbawanga.

Wananchi wa kijiji cha Msila kata ya Mfinga wilaya ya Sumbawanga wakiwa kwenye kikao na viongozi wa Kamati ya Siasa ya CCM mkoa wa Rukwa juzi wakati kamati hiyo ilipokagua utekelezaji wa Ilani ya CCM.

Mwenyekiti wa CCM Rukwa Ndugu Rainer Lukala akizungumza na wananchi wa kijiji cha Msila kata ya Mfinga wilaya ya Sumbawanga juzi walipokagua utekelezaji wa Ilani. Kulia kwake ni Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Joseph Mkirikiti.

Wanachama wa kikundi cha Kilimo Kwanza walionufaika na mkopo shilingi Milioni sita toka halmashauri ya wilaya ya Sumbawanga juzi  wakifuatilia kikao na viongozi wa CCM mkoa huo walipotembelea kijiji cha Msila kata ya Mfinga.

Mwenyekiti wa CCM mkoa wa Rukwa Rainer Lukala akiongea na wanufaika wa mkopo wa shilingi Milioni tano toka halmashauri ya wilaya ya Sumbawanga kwa kundi la walemavu juzi katika kijiji cha Ilemba.

(Habari na Picha na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Rukwa)

Na. OMM Rukwa

Halmashauri ya Wilaya ya Sumbawanga imepongezwa kwa kuwezesha walemavu na wanawake kupata mikopo inayotokana na mapato ya ndani hatua inayosaidia kukuza uchumi wa kaya.

Pongezi hizo zimetolewa jana na Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi Rainer Lukala wakati akiongea na wanufaike wa mikopo katika vijiji vya Msila na Ilemba ikiwa ni ziara ya ukaguzi wa utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM.

“Maelekezo ya Ilani ya CCM ni kutumia fedha asilimia kumi ya mapato ya ndani ya halmashauri kwa ajili ya kuwezesha mikopo kwa makundi ya wanawake, vijana na walemavu kwa riba nafuu. Tunawapongeza halmashauri kwa kufanikisha hilo” alisema Lukala.

Halmashauri hiyo katika mwaka 2021/22 imetoa mikopo ya shilingi Milioni Sita (6) kwa kikundi cha wanawake wa kijiji cha Msila na shilingi Milioni Tano (5) kwa walemavu wawili wa kijiji cha Ilemba.

Lukala alitoa wito kwa wanufaike wa mikopo hiyo kuwa na utaratibu wa kuutunza fedha kwenye akaunti za benki ili wawe na uhakika wa kufanya marejesho na kuwa halmashauri itoe kipaumbele kwa vikundi vinavyorejesha vizuri ili wapate mikopo awamu ya pili.

Naye Katibu wa Kikundi cha Kilimo Kwanza kijiji cha Msila kata ya Mfinga Anastazia Joseph alisema anaomba halmashauri iongeze kipindi cha kurejesha mkopo toka mwaka mmoja hadi miwili kwa kuwa rejesho la shilingi 500,000 kila mwezi kati ya mkopo wa shilingi Milioni 6 ni kubwa.

Kikundi hicho chenye wanachama kumi na mbili (12) kinajishughulisha na kazi za kilimo ambapo wamelima hekari nne za mahindi na moja ya alizeti huku wanachama wakiweka akiba na kukopeshana.

Kwa upande wake Joseph Mwendapole mnufaika wa mikopo ya walemavu toka kijiji cha Ilemba alisema ameweza kununua pikipiki kutokana na mkopo wa Milioni 2.5 hatua inayomwezesha kupata kipato cha kuutunza familia na shughuli za kilimo.

Mnufaika huyo aliwaambia wajumbe wa Kamati ya Siasa Mkoa wa Rukwa kuwa kwa sasa anamiliki pia bajaji kutokana na mkopo aliopata awali ambapo ametoa wito kwa halmashauri kuwapa pia wahitaji wengine mikopo ikiwemo vijana kwa masharti nafuu.

“Ninaahidi nitajitahidi kufanya marejesho ili walemavu wengine wapate mikopo hii. Sasa napambania uzee wangu ili niwe na amani uzeeni kwa kuwa na uhakika wa kipato” alisema Mwendapole.

Previous articleTMA YATAKIWA KUJIKITA KATIKA KUKUZA MAPATO YA NDANI
Next articleWAFANYAKAZI WANAWAKE WA KAMPUNI YA SGA WATOA MSAADA WA VIFAA HOSPITALI YA OCEAN ROAD
Hughes Dugilo is a Writer, News Producer, Video-Photographer Journalist, and Video Editor experienced for 20 years now performing in News, Documentary, Advertisements and Television Programs. Aside from all above he own and operate his Blog known as Green Waves Media TZ since 2018.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here