Home LOCAL WAKAZI 10,234 KATA YA MARATANI WILAYANI NANYUMBU KUNUFAIKA NA MRADI WA MAJI...

WAKAZI 10,234 KATA YA MARATANI WILAYANI NANYUMBU KUNUFAIKA NA MRADI WA MAJI YA BWA

 

Kaimu Meneja wa wakala wa maji safi na usafi wa mazingira(RUWASA)wilaya ya Nanyumbu mkoani Mtwara Mhandisi Simon Mchucha wa tatu kulia, akiwaongoza wakazi na viongozi wa kijiji cha Maratani waliotembelea mradi wa Bwawa la maji lililochimbwa na Wizara ya maji ajili ya kupeleka huduma ya maji safi na salama kwa wakazi wa kata ya Maratani na vijiji vinavyozunguka kata hiyo,wa tatu kulia Diwani wa kata hiyo Salum Mmole na katikati mwenyekiti wa Serikali ya kijiji Abdala Tango.

Na: Muhidin Amri,, Nanyumbu.

WAKAZI 10,234 wa vijiji vinne katika kata ya Maratani wilaya ya Nanyumbu mkoani Mtwara, wanatarajia kuondokana na kero ya maji safi na salama kufuatia wizara ya maji kukamilisha kuchimba Bwala kubwa  lenye uwezo wa kuhifadhi  mita za ujazo 375,460 sawa na lita 375,460,000.

Kaimu Meneja wa wakala wa usambazaji maji safi na usafi wa mazingira vijijini(Ruwasa)wilaya ya Nanyumbu Mkoani Mtwara Simon Mchucha,alivitaja vijiji vitakavyonufaika na mradi huo ni Maratani,Namasogo,Chilunda na Mikangaula.

Alisema, ujenzi wa bwawa hilo uliibuliwa mwaka 2018 katika jitihada za kutatua changamoto za upatikanaji wa huduma ya maji kwa wakazi wa kata hiyo.

Alisema,utekelezaji wa bwawa hilo ulianza mwezi Julai 2020 na kukamilika Desemba 2021 kwa kutumia wataalam wa ujenzi wa mabwawa, ambapo mbali na kuwanufaisha wakazi wa Maratani pia  litahudumia vijiji  jirani vinavyozunguka kata  hiyo na mifugo 356.

Alisema, awali serikali ilipanga kutumia jumla ya Sh.bilioni 1,430,179,978.87 kama gharama za mradi kwa kumtumia mkandarasi,lakini kutokana na kutumia mfumo wa force account,wamefanikiwa kuokoa  jumla ya Sh.290,605,732.75 na hivyo kufanya gharama halisi ya mradi ni Sh.1,139,574,066.12.

Alisema,kukamilika kwa bwawa hilo kutatua changamoto ya huduma ya maji safi na salama kwa wakazi wa kata ya Maratani,na kupunguza  kero ya kufuata maji umbali mrefu hasa kwa wanawake na watoto .

Alitaja faida nyingine, ni wananchi wataongeza muda wa kufanya kazi za uzalishaji mali na kukuza uchumi,tofauti na sasa ambapo wanatumia muda mwingi na kutembea umbali kusaka maji kwa matumizi ya familia.

Aidha, alitaja changamoto kubwa wakati wa ujenzi wa mradi huo ni kuchelewa kwa fedha, jambo lililosababisha bwawa kutokamilika kwa wakati na kupelekea kushinwa kuvuna maji ya kutosha,hata hivyo kutokana na mvua za masika  zinazoendelea kunyesha sasa wameanza kuvuna maji.

Baadhi ya wakazi wa kata ya Maratani,wameishukuru Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan kwa jitihada zake katika kumaliza kero  ya maji na huduma nyingine za kijamii.

Walisema,tangu Uhuru  wa Tanganyika na sasa Tanzania mwaka 1961 kijiji hicho na vingine vinavyounda kata ya Maratani havijawaji kupata maji ya bomba, badala yake walikuwa wanachota maji kwenye visima vya asili vilivyochimbwa  kwa ajili ya kukabiliana na  kero hiyo.

Diwani wa kata ya Maratani Salum Mmole alisema, ni muda mrefu katika kijiji hicho na kata nzima ya Maratani hakuna maji ya  kutosha jambo  lililopelekea baadhi ya wananchi  kubaki nyuma kimaendeleo kutokana na kukosa muda wa kufanya kazi za uzalishaji mali na kukuza uchumi wao.

Ameiomba Serikali, kukamilisha kazi ya kupeleka miundombinu ili  maji hayo yafike hadi katika makazi  yao,ili wasiendelea kutumia maji ya visima vya asili au kutumia maji ya bwawa hilo ambayo  sio salama.

Akizungumza kwa niaba ya wazee kabila la Wamakuha Mwenye Akwirimpwe Ali,ameishukuru serikali kuchimba bwawa hilo kwani limewaondolea adha  ya muda mrefu ya kutumia maji ambayo  sio safi na salama na kuwapunguzia umbali  wa kwenda kutafuta maji.
MWISHO.


Previous articleMAHAKAMA YAKATAA PINGAMIZI LA ALIYEKUWA MKUU WA WILAYA YA TABORA.
Next articleRAIS WA ZANZIBAR MHE.DK.HUSSEIN ALI MWINYI AMEWEKA JIWE LA MSINGI MRADI WA IHUISHAJI NA UIMARISHAJI WA MFUMO WA USAMBAZAJI WA MAJI ZANZIBAR
Hughes Dugilo is a Writer, News Producer, Video-Photographer Journalist, and Video Editor experienced for 20 years now performing in News, Documentary, Advertisements and Television Programs. Aside from all above he own and operate his Blog known as Green Waves Media TZ since 2018.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here