Home BUSINESS TCB KUUNGA MKONO JUHUDI ZA WAJASIRIAMALI WANAWAKE ZANZIBAR

TCB KUUNGA MKONO JUHUDI ZA WAJASIRIAMALI WANAWAKE ZANZIBAR

 
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk.Hussein Ali Mwinyi akizungumza na Ujumbe wa Benki ya Biashara Tanzania (TCB) ukiongozwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Benki hiyo Bw.Sabasaba Moshingi (kulia kwa Rais) na (kushoto kwa Rais) Katibu wa Baraza la Mapinduzi na Katibu Mkuu Kiongozi Mhandisi Zena Ahmed Said, walipofika Ikulu Zanzibar kwa mazungumzo na kujitambulisha. (Picha na Ikulu)

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi ameipongeza azma ya Benki ya Biashara Tanzania (TCB) ya kuunga mkono juhudi za wajasiriamali wanawake hapa Zanzibar katika kukuza uchumi hasa uchumi wa Buluu.

Rais Dk. Mwinyi aliyasema hayo leo wakati alipokutana na kufanya mazungumzo na uongozi wa Benki ya Biashara Tanzania (TCB), Ikulu Jijini Zanzibar ukiongozwa na Mkurugenzi Mkuu wa Beki hiyo Sabasaba Moshingi.
Katika maelezo yake Rais Dk. Mwinyi alisema kwamba maono ya Serrikali anayoiongoza ni kuubadilisha uchumi wa Zanzibar hivyo wadau kama Benki hiyo wanahitajika katika kufanya kazi pamoja na Serikali hasa katika kuwainua akina mama kiuchumi.
Alisema kwamba kusaidia akina mama ni jambo muhimu sana kwani hapa Zanzibar kuna kundi kubwa la wajasiriamali ambao wengi wao ni akina mama hivyo, kuna haja ya kuwaunga mkono hasa kwa wale wanaojishughulisha na ukulima wa mwani.
Rais Dk. Mwinyi alisema kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar iko tayari kufanya kazi pamoja na benki hiyo kwani kumekuwa na mambo mawili ambayo yamekuwa yakiwakwaza wajasiriamali likiwemo dhamana pamoja na riba na ndio maana Serikali imeamua kwa makusudi kuingia makubaliano na benki ili iweze kuwasaidia.
Alisema kubwa wakopaji walio wengi walikuwa hawana elimu ya kukopa na ndio maana hapo siku za nyuma walikuwa wakiuziwa mali zao za thamani hivyo, wamekuwa na woga mkubwa na ndio maana Serikali imeamua kulibeba na kuwachukulia dhamana wakopaji.
Rais Dk. Mwinyi alitumia fusa hiyo kuipongeza benki ya Biashara Tanzania (TCB) kwa kutoa mikopo yenye thamani ya TZS Bilioni 3 kwa akina mama wadogo wadogo hapa Zanzibar na kusisitiza haja ya Benki hiyo kuongeza kiasi hicho cha fedha ili mikopo hiyo iwafaidishe walio wengi.

Alisema kwamba kuwepo kwa Kongamano la wanawake Zanzibar, linalotarajiwa kufanyika Machi 5,mwaka huu 2022 lenye kauli mbiu ya “Nafasi ya Mwanamke katika kukuza uchumi wa Buluu kwa maendeleo endelevu”, kutasaidia kwa kiasi kikubwa katika kuimarisha sekta za uchumi wa buluu ikiwemo uvuvi, kilimo cha mwani pamoja na ufugaji wa samaki hasa kwa akina mama.
Alipongeza hatua ya Benki hiyo ya kutoa mikopo inayokwenda sambamba na mafunzo ambayo yatasaidia kwa kiasi kikubwa kufanya shuhuli zao za ujasiriamali.
Aidha, Rais Dk. Mwinyi alitoa pongezi kwa misaada mbali mbali iliyotolewa na Benki hiyo kwa ajili ya Taasisi, vikundi vya akina mama wajasiriamali wanaojishughulisha na ukulima wa mwani na uchimbaji visima hatua ambayo itasaiidia kwa kiasi kikubwa kuwaendeleza wanawake.
Nae Katibu wa Baraza la Mapinduzi na Katibu Mkuu Kiongozi Mhandisi Zena Ahmed Said alieleza haja kwa Benki hiyo kufanya kazi na Taasisi ya ‘Zanzibar Maisha Bora Foundation’ kwa ajili ya kuwasaidia akina mama wanaojishughulisha na ukulima wa zao la mwani kwani Taasisi hiyo imelenga kuwasaidia wajasiriamali hao.
Mapema Mkurugenzi Mkuu wa Benki ya Biashara Tanzania (TCB), Sabasaba Moshingi kwa upande wake alitoa pongezi kwa Rais Dk. Mwinyi kwa maono yake ya Uchumi wa Buluu hatua ambayo itasaidia kwa kiasi kikubwa kuinua uchumi wa Zanzibar.
Alieleza matumaini yake ya maendeleo makubwa yatakayofikiwa Zanzibar kutokana na mikakati madhubuti iliyowekwa na Serikali anayoiongoza Rais Dk. Mwinyi.
Alisema kuwa Benki hiyo ya Biashara (TCB) ni Benki kongwe ambayo ina miaka 97 tokea kuanzishwa kwake na ambayo imepita katika mabadiliko mbali mbali makubwa ambapo hapo mwanzo ilijulikanwa kama ni Benki ya TPB.
Mkurugenzi huyo alieleza jinsi ya umiliki wa Benki hiyo hivi sasa na kueleza kwamba Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ina hisa katika Benki hiyo na imekuwa na Meneja wake anayefanya kazi Unguja na Pemba.
Alisema kuwa Benki hiyo imepitia Mapinduzi makubwa na hivi sasa imeimarika kwa kiasi kikubwa ambapo ina matawi 82 kutoka matawi 30 na ina wafanyakazi 1001 ambayo inawalenga wananchi wa kawaida pamoja na hata wale wananchi wenye wakubwa.
Alisema kwamba mwaka 2018 TCB ilikabidhiwa Benki ya Wanawake ambayo hapo nyuma ilipata changamoto ya uendeshaji ambayo tayari imeshaanza kutoa huduma sanjari na kufungua matawi kadhaa nchini na kuweza kutoa mikopo kwa akina mama yenye thamani ya TZS Bilioni 127 na kwa upande wa Zanzibar tayari imeshatoa TZS Bilioni 3.
Alisema kuwa kuwepo kwa Makongamano yaliyoanza katika Mikoa ya Dar es Salaam, Dodoma na kwengineko kutasaidia kutunza kumbukumbu, faida na mafunzo mengine ambayo akina mama wameweza kupata mafanikio. Pia, alieleza misaada mbali mbali wanayotarajia kuitoa kwa akina mama wajasiriamali siku ya Kongamano hilo.
Imetayarishwa na Kitengo cha Habari,
Ikulu Zanzibar.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here