Jumatano, Machi 16, 2022, Dodoma.
Ndugu Wananchi, Leo tarehe 16 Machi 2022, nchi yetu inatimiza miaka miwili kamili tangu kuthibitika kwa uwepo wa Ugonjwa wa Virusi vya Korona (UVIKO-19) kwa mara ya kwanza hapa nchini. Katika kipindi chote hiki, Serikali kwa kushirikiana na wadau wa maendeleo, mashirika yasiyo ya kiserikali, Taasisi za Dini na wanataaluma wa afya na wananchi kwa ujumla imeendelea kutekeleza mikakati mbalimbali ya kukabiliana na ugonjwa huu. Hatua ambazo zimechukuliwa na Serikali katika kupambana na UVIKO19 kwa kiasi kikubwa zimezingatia mazingira na hali ya jamii yetu ikiwemo kuruhusu wananchi kuendelea kujitafutia kipato chao (yaani kutokuwa na lockdown) na hivyo kupunguza hofu na kunusuru uchumi wa jamii na Taifa kwa ujumla.
Ndugu Wananchi, hadi kufikia tarehe 15 Machi 2022, jumla ya watu 33,789 wamethibitika kuwa na maambukizi ya UVIKO – 19 na watu 803 wamepoteza Maisha nchini. Kwa niaba ya Serikali, natoa pole za dhati kwa familia, ndugu, jamaa na marafiki waliopoteza wapendwa wao na wote waliopatwa na madhara mbalimbali kutokana na ugonjwa huu.
Ndugu Wananchi, mikakati iliyotekelezwa na Serikali ni pamoja na kuwaondoa hofu wananchi kuhusu mwanzoni mwa mlipuko wa ugonjwa huu, kufunga Shule, Vyuo na Taasisi za Elimu ya juu, kutoa elimu kwa jamii ju ya kujikinga na ugonjwa huu, kuhimiza jamii kusitisha mikusanyiko isiyokuwa ya lazima, kuimarisha huduma za ukaguzi na uchunguzi wa afya kwa wasafiri katika maeneo ya viwanja vya ndege, bandari na mipaka ya nchi kavu ili kuzuia kuingia kwa maambukizi nchini na kuboresha mchango wa tiba asili. Aidha katika kipindi hiki pia tumeweza kuongeza wigo wa uchunguzi wa kimaabara wa UVIKO-19 ambapo kwa sasa kuna maabara saba ndani ya nchi zenye uwezo wa kupima UVIKO19 kulinganisha na Maabara moja ya Afya ya Jamii iliyokuwepo wakati wa kulipuka kwa ugonjwa huu mwezi Machi 2020. Maabara hizi ni pamoja na Maabara ya Taifa ya Afya ya Jamii, Maabara katika Hospitali za Kanda za Bugando, Mbeya na Maabara katika Hospitali za Rufaa za Mikoa ya Dodoma, Arusha, Kigoma, na Maabara iliyopo katika Hifadhi ya Taifa ya Ngorongoro. Aidha, Serikali imesimika mitambo 15 ya hewa tiba ya Oksijeni katika Hospitali mbalimbali nchini ili kuweza kutoa huduma za wagonjwa mahututi wanaohitaji uangalizi maalum.
Ndugu Wananchi, Serikali pia imeendelea kuikinga jamii kwa kuwezesha upatikanaji wa chanjo ya UVIKO-19 nchini, ambapo hadi kufikia tarehe 12 Machi 2022, jumla ya watu 2,820,545 wenye umri wa miaka 18 na kuendelea, wamepata chanjo kamili dhidi ya ugonjwa huu. Idadi hii ni sawa na asilimia 9.17 ya watanzania 30,740,928 wenye umri wa miaka 18 na kuendelea ambao wanakidhi vigezo vya kuchanja. Idadi hii bado hairidhishi kwa kuwa ili tuweze kufikia kinga ya jamii (Heard immunity) tunapaswa kuchanja angalau asilimia 70 ya watu wenye umrii wa miaka 18 na kuendelea. Hali ya kiwanjo cha uchanjaji Kimikoa ni kama ifuatavyo: Ruvuma (23%), Katavi (14%), Dodoma (13%), Mtwara (12%), Mara (11%), Mwanza (11%), Lindi (10%), Dar-es-Salaam (10%), Simiyu (10%), Pwani (9), Kilimanjaro (9%), Kagera (9%) na Mbeya (9%) , Arusha (8%), Geita (7%), Shinyanga (7%), Iringa (7%), Njombe (7%), Rukwa (6%), Morogoro (6%), Tanga (5%), Kigoma (5%), Tabora (5%), Singida (5%), Songwe (4%) na Manyara (3%). Kuzingatia hali hii, Mikoa inahitaji kuongeza juhudi katika kuhimiza wananchi kujitokeza kuchanja.
Ndugu Wananchi, hali ya UVIKO-19 katika wimbi la nne nchini kwa sasa imepungua kwa kiasi kikubwa tokea lilipoanza mwanzoni mwa mwezi Desemba 2021 ambapo kwa mwezi Desemba 2021 jumla ya watu 4,285 walithibitika kuwa na maambuzi ya ugonjwa huu. Kwa upande wa mwezi Januari 2022 wagonjwa waliothibitika walikuwa 2,737 na kwa kipindi cha mwezi Februari 2022, jumla ya wagonjwa 401 walithibitika kupata maambukizi ya ugonjwa huu. Kupungua kwa maambukizi mapya ya ugonjwa wa COVID19 kumeripotiwa pia katika baadhi ya nchi Duniani huku kukiambatana na kulegezwa kwa masharti ya kuzuia kusambaa kwa maambukizi.
Ndugu Wananchi, pamoja na kuonekana kupungua kwa ugonjwa huu kwa sasa hapa nchini, ugonjwa huu hutokea kwa mtindo wa mawimbi ambayo yanaambatana na mabadiliko mbalimbali ikiwemo kuibuka kwa anuai mpya za kirusi, kubadilika kwa dalili, kuongezeka makali ya ugonjwa na kubadilika kwa njia mahususi za kukabiliana nao. Aidha ndani ya wiki hii kumeripotiwa taarifa ambazo bado hazijathibitishwa na Shirika la Afya Duniani (WHO) kuhusu kuibuka kwa aina mpya ya kirusi cha COVID19 katika nchi za China, South Korea na Japan. Wizara ya Afya inaendelea kuwasiliana na Shirika la Afya Duniani kuhusu suala hili sambamba na kuendelea kuimarisha ukaguzi na ufuatilia wa wasafiri wanaongia nchini kwetu.
Ndugu Wananchi, kwa kuwa bado ugonjwa wa UVIKO19 upo katika nchi yetu, Serikali itaendelea kutekeleza mikakati mbalimbali ya kupambana na ugonjwa huu ikiwemo kufanya yafuatayo;-
1. Kuimarisha ufuatiliaji wa hali ya ugonjwa ndani na nje ya nchi na kuishirikisha jamii katika mapambano dhidi ya ugonjwa huu
2. Kuimarisha huduma za ukaguzi na uchunguzi wa afya kwa wasafiri wanaoingia nchini katika maeneo ya viwanja vya ndege, Bandari na mipaka ya nchi kavu. Kwa kuzingatia hali ya sasa ya maambukizi ya UVIKO-19 nchini na mwenendo wa ugonjwa huu duniani, Serikali inalegeza masharti kwa Wasafiri wanaoingia nchini ambao wamekamilisha dozi ya chanjo ya UVIKO-19 hivyo kuanzia kesho tarehe 17/03/2022 wanaondolewa hitaji la kuwa na cheti cha kipimo cha kuthibitisha kutokuwa na maambukizi (negative RT – PCR certifícate) kilichokuwa kikihitajika hapo awali. Masharti haya na masharti mengine yataainishwa kwenye mwongozo wa wasafiri ambao utakua ukibadilika kulingana na mwenendo wa maambukizi ya ugonjwa huu nchini na duniani kwa ujumla.
3. Kuongeza wigo wa uchunguzi wa kimaabara katika Mikoa yote nchini na hivyo kuhakikisha upatikanaji wa majibu ya wagonjwa kwa wakati. Aidha huduma za kipimo cha haraka (COVID-19 Rapid Antigen Test) zitaanza kutolewa ndani ya wiki moja katika vituo mbalimbali vya huduma za afya nchini.
4. Kuimarisha upatikanaji wa dawa na vifaatiba muhimu katika kukabiliana na ugonjwa huu ikiwemo kuimarisha huduma za wagonjwa mahututi na wanaohitaji uangalizi maalumu. Na katika hili tunamshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan kwa kuwezesha upatikanaji wa fedha za mkopo wa masharti nafuu wa Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) ambao umeleta manufaa makubwa nchini katika kuboresha huduma za afya kwa wananchi. Fedha hizi zimeimarisha huduma za afya ambapo zimefanya ujenzi, upanuzi na ukarabati wa miundombinu katika ngazi mbalimbali za vituo vya kutolea huduma za afya nchini ikiwa ni pamoja na ujenzi wa vyumba 64 vya wagonjwa mahututi (ICU), ujenzi wa vyumba vya huduma za dharura (Emergency Department) katika Hospitali 100, ununuzi na usimikaji wa mashine za uchunguzi (MRI na CT Scan) katika hospital za Rufaa za Mikoa na Kanda, ununuzi wa magari maalum ya kubebea wagonjwa, kutoa mafunzo kwa watumishi na kuongeza wataalam wa kada mbalimbali za afya.
5. Kuhamasisha wananchi kupata chanjo dhidi ya ugonjwa wa UVIKO-19. Ninawahimiza wananchi wenye umri wa miaka 18 na kuendelea kupata chanjo dhidi ya UVIKO-19 kwa kuwa chanjo ndio nguzo kuu kwa sasa katika kujikinga na kukabiliana na ugonjwa huu. Hivyo nahimiza wananchi kuhakikisha kuwa wanapata chanjo kamili kwa wakati hususani kwa sababu zifuatazo:
I. Chanjo ziko salama na mpaka sasa chanjo ndiyo njia pekee iliyothibitika kupunguza madhara yatokanayo na janga hili la kidunia. Takwimu zetu zinaonyesha kuwa zaidi ya asilimia 90 ya wagonjwa wanaolazwa na wanaohitaji huduma za wagonjwa mahututi ni ambao hawajachanja.
II. Wananchi wengi kwa sasa hapa nchini bado hawajapata kinga ya kuzuia au kupunguza makali ya UVIKO-19 pindi wakikutana na watu wenye maambukizi.
III. Ugonjwa wa UVIKO-19 bado upo duniani na siyo rahisi kujua nani anaweza kukuambukiza.
IV. Mpaka sasa chanjo ndiyo njia pekee iliyothibitika kupunguza madhara yatokanayo na janga hili la kidunia.
V. Kuondokana na changamoto ambazo zinaweza kujitokeza pindi mtu anapotaka kusafiri. Kwa sasa hivi duniani bila chanjo unaweza kukosa baadhi ya huduma za kijamii.
Ndugu Wananchi, Sambamba na chanjo ninawahimiza wananchi kuendelea kuchukua hatua za kujikinga na ugonjwa huu ikiwemo kuvaa barakoa kwa usahihi mnapokuwa kwenye maeneo yenye mikukanyiko na kwenye mikutano ya ndani, kuzingatia usafi binafsi ikiwemo kunawa mikono mara kwa mara kwa sabuni na maji tiririka au kutumia vipukusi (sanitezers), kufunika mdomo na pua wakati wa kukohoa kwa kitambaa safi au kutumia kiwiko cha mkono, kuendelea kuchukua hatua za kujenga mwili imara ikiwemo kuzingatia ulaji wa vyakula unaofaa na kufanya mazoezi ya mwili angalau mara tatu kwa wiki.
Ndugu Wananchi, narudia kusisitiza kuwa UVIKO-19 bado upo na hutokea kwa mtindo wa mawimbi yanayoambatana na mabadiliko mbalimbali. Hivyo kila mmoja wetu anao wajibu wa kushiriki katika mapambano dhidi ya ugonjwa huu. Nitumie fursa hii kuwashukuru sekta mbalimbali ndani ya Serikali, wadau wa maendeleo, viongozi wa dini, viongozi wa kijamii na makundi mbalimbali ya kijamii kwa kutuunga mkono katika mapambano dhidi ya ugonjwa huu. Kipekee ninawashukuru WATUMISHI WA AFYA nchni hususani walio mstari wa mbele katika kuwahudumia wagonjwa. Tunawashukuru sana! Serikali kupitia Wizara ya Afya itaendelea kushirikiana na wote katika kuhakikisha tunaudhiti ugonjwa huu. Hata hivyo badala ya kupambana na ugonjwa huu peke yake, mwelekeo wetu sasa ni kuendelea kutoa huduma za kudhibiti UVIKO-19 kupitia huduma nyingine jumuishi za afya kama vile Kifua Kikuu, huduma za mama na mtoto, huduma za VVU/UKIMWI, huduma za malaria, huduma za magonjwa yasiyoambukiza na kadhalika.
Asanteni na imetolewa na:
Ummy Ally Mwalimu (Mb)
WAZIRI WA AFYA