Home BUSINESS ‘‘TADB WEKENI UTARATIBU WA RIBA NA MASHARTI NAFUU’’ – MAJALIWA

‘‘TADB WEKENI UTARATIBU WA RIBA NA MASHARTI NAFUU’’ – MAJALIWA


Benki ya Maendeleo ya kilimo Tanzania (TADB) imeaswa kuweka utaratibu wa riba na masharti nafuu utakaowawezesha Watanzania wengi kunufaika kupitia mikopo ya muda mrefu na muda mfupi.

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa mradi wa ushirikiano wa wasindikaji na wazalishaji katika tasnia ya maziwa Tanzania (TI3P) uliofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT) leo jijini Dar es Salaam, Waziri Mkuu, Mhe. Kassim Majaliwa, amesema nia ya serikali ni kuhakikisha kwamba TADB inawafikia wakulima, wafugaji na wavuvi wengi zaidi na kuongeza ufanisi katika utoaji wa huduma.

“TADB zingatieni agizo la Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan la kuhakikisha kwamba fedha kwa ajili ya mikopo zinatumika ipasavyo nakuwafikia wakulima wengi Zaidi ikiwemo wakulima wadogo na kuongeza ufanisi katika utendaji kazi”, alisema Waziri Mkuu.

Aidha, Waziri Mkuu ameagiza Wizara ya Mifugo na Uvuvi iimarisheni eneo la utafiti, hasa kwenye vyuo vya utafiti, kwa kufanya tafiti ambazo zitatoa suluhisho kwa changamoto katika sekta ya mifugo ili kuongeza ubora na wingi wa maziwa.

Mapema, Naibu Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania, Uthabiti na Usimamizi wa Sekta ya Fedha, Dkt. Bernard Kibesse, alisema licha ya misukosuko iliyochangiwa na janga la UVIKO-19, sekta ya kibenki nchini imeendelea kukua.

“Sekta ya kibenki imeendelea kukua kwenye maeneo ya amana, mikopo na uwekezaji wa hatifungani; huku ikichagizwa na mazingira mazuri ya uchumi mpana pamoja na udhibiti na usimamizi wa benki na taasisi za fedha,”alisema Dkt. Kibesse.

Alieleza kuwa Benki Kuu imekua mstari wa mbele katika kukuza huduma za benki za maendeleo Tanzania ikiwa ni pamoja na kuhakikisha sheria na kanuni zinakuwa wezeshi ili benki hizo ziweze kuwa chachu ya maendeleo nchini.

Katika kutimiza adhma hiyo, Naibu Gavana aliongeza kuwa, mwaka 2021, Benki Kuu ilipitia kanuni za kusimamia benki za maendeleo, kuziboresha, na kuwa na kanuni mpya za mwaka 2021, yaani The Banking and Financial Institution (Development Finance Regulations, 2021).

“Kanuni hizi zimeweka mazingira wezeshi kwa benki hizi kuweza kujiendesha kwa kufuata misingi ya sheria na kanuni ili kuleta maendeleo Tanzania,”
alisema.

Dkt. Kibesse alisema kuwa Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB) imeendelea kushirikiana na wadau mbalimbali katika kufanikisha maendeleo katika sekta ya kilimo hapa nchini, na kwamba, kwa sasa, TADB imeingia makubaliano na taasisi ya Bill and Melinda Gates Foundation (BMGF) ya kupatiwa msaada (grant) wenye thamani ya dola za kimarekani milioni saba.

“Fedha hizi ni kwa ajili ya kuendeleza sekta ndogo ya maziwa nchini kupitia mradi wa Ushirikiano wa Wasindikaji na Wazalishaji Katika Sekta ya Maziwa (Tanzania Inclusive Processor-Producer Partnership in Dairy (TI3P), aliongeza Dkt. Kibesse.

Alisisitiza kuwa lengo la mradi huo ni kuleta mabadiliko chanya katika sekta ndogo ya maziwa kupitia uhamasishaji wa uwekezaji kutoka sekta ya umma na sekta binafsi kwa kusudi la kuongeza tija katika uzalishaji wa maziwa, kuongeza ukusanyaji wa maziwa katika mfumo ulio rasmi, kukuza uwezo wa viwanda katika uchakataji wa maziwa na kupanua wigo wa soko la bidhaa za maziwa.

Dkt. Kibesse aliongeza kuwa BoT itaendelea kusimamia kwa karibu uchumi pamoja na sekta ya fedha kwa lengo la kuongeza kasi ya maendeleo ya wananchi, na kuisimamia TADB ili faida zinazotarajiwa kutokana na mradi huu na shughuli nyingine za benki hii ziweze kupatikana.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here