Kamati ya Sera ya Fedha ya Benki Kuu ya Tanzania imefanya kikao chake cha kawaida cha 219 tarehe 24 Machi 2022, kutathmini utekelezaji wa sera ya fedha na mwenendo wa uchumi wa ndani na wa dunia. Kamati imeridhishwa na utekelezaji wa sera ya fedha katika kipindi cha Januari na Februari 2022, uliowezesha uwepo wa ukwasi wa kutosha katika uchumi na utulivu wa viwango vya riba katika soko la fedha kulingana na matakwa ya sera ya fedha. Kamati imeidhinisha Benki Kuu kuendelea kutekeleza sera wezeshi ya fedha inayolenga kuongeza ukwasi, ili kusaidia ukuaji zaidi wa mikopo kwa sekta binafsi na kuimarisha biashara na uwekezaji, kwa kuzingatia matarajio ya mfumuko wa bei katika kipindi kilichosalia cha 2021/22.
Mwenendo wa uchumi kwa mwaka 2021 ulikuwa wa kuridhisha na inatarajiwa ukuaji chanya kuendelea kwa mwaka 2022, kutokana na kuendelea kuimarika kwa shughuli za biasharana uwekezaji baada ya janga ya UVIKO–19. Bei za bidhaa na huduma zimepanda katika kipindi cha hivi karibuni, lakini mfumuko wa bei uliendelea kuwa ndani ya malengo ya asilimia 3–5 kwa upande wa Tanzania Bara na chini ya asilimia 5 kwa Zanzibar.
Mfumuko wabei unatarajiwa kuendelea kuwa sawia na malengo kutokana na upatikanaji wa chakula cha kutosha na sera madhubuti za uchumi. Aidha, athari zitokanazo na kupanda kwa bei ya nishati na bidhaa katika soko la dunia, hali inayochangiwa zaidi na mikwamo kwenye minyororo ya ugavi na mgogoro unaoendelea Ulaya Mashariki inaweza kusababisha kupanda kwa bei za bidhaa nchini.
Kamati ya Sera ya Fedha imeridhishwa na kasi ya ukuaji wa mikopo kwa sekta binafsi ambayo imeendelea kuimarika hadi kufikia asilimia 11.9 mwezi Februari 2022. Ongezeko la kasi ya ukuaji wa mikopo kwa sekta binafsi linatokana na kuimarika kwa hali ya biashara kutoka kwenye athari hasi za janga la UVIKO–19, hatua za kisera zilizochukuliwa na Benki Kuu ili kuchochea mikopo na kupunguza viwango vya riba, pamoja na sera wezeshi za fedha na bajeti.
Sekta ya nje imeendelea kuimarika na akiba ya fedha za kigeni imeendelea kuwa ya kuridhisha, ikiwa na kiasi cha kutosheleza kuagiza bidhaa na huduma kutoka nje kwa takriban miezi 5.9, sawia na malengo ya nchi na jumuiya za kikanda. Katika miezi saba ya kwanza ya 2021/22, ukusanyaji wa mapato ulikuwa wa kuridhisha kutokana na kuendelea kuimarika kwa shughuli za kiuchumi, juhudi za kukusanya mapato na jitihada za kuboresha makusanyo ya kodi.
Kutokana na mgogoro unaoendelea Ulaya Mashariki na hali ya mikwamo kwenye
minyororo ya ugavi katika soko la dunia, Kamati ya Sera ya Fedha itaendelea kufuatilia kwa karibu mwenendo wa uchumi na kuchukua hatua stahiki pale itakapohitajika, ili kuulinda uchumi na athari za misukosuko ya nje na kusaidia kuimarika kwa sekta mbalimbali za kiuchumi.