Home BUSINESS MAAFISA BIASHARA WATAKIWA KUVUTIA WAWEKEZAJI

MAAFISA BIASHARA WATAKIWA KUVUTIA WAWEKEZAJI

Mkuu wa Mkoa wa Mbeya Mhe. Juma Homera akifungua mafunzo ya Sheria ya Leseni za Biashara  kwa Maafisa Biashara kutoka mikoa ya Mbeya,  Rukwa, na Songwe, Jijini Mbeya. Aliyeketi kulia ni Afisa Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni  (BRELA) Bw. Godfrey Nyaisa na kushoto ni Afisa Biashara kutoka Wizara ya Uwekezaji,  Viwanda na Biashara Bw. Denis Mzamilu. Mafunzo haya ya siku tano yaliyoandaliwa na BRELA yana lengo la kuwajengea uwezo maafisa hao ili watekeleze sheria hiyo kwa ukamilifu


15 Machi,2022, Mbeya

Mkuu wa Mkoa  wa Mbeya, Mhe. Juma Homera, amewataka Maafisa Biashara nchini kubadilika na kuwa wabunifu katika maeneo wanayofanyia kazi ili kuleta tija katika uwekezaji.

Mhe. Homera ametoa rai hiyo leo tarehe 15 Machi, 2022 wakati akifungua mafunzo kwa Maafisa Biashara kutoka mikoa ya Mbeya, Songwe na Rukwa iliyopo Kanda ya Nyanda za Juu Kusini, kuhusu Sheria ya Leseni za Biashara Sura Na. 208, yaliyoandaliwa na Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA) Jijini Mbeya.

Mhe.Homera amesema ili kuwa na uchumi wa kati umefika wakati sasa kwa Maafisa Biashara kuacha kufanya kazi kwa mazoea badala yake wawe wabunifu kwa kuangalia fursa zilizopo katika maeneo yao na kutengeneza mazingira ya kuvutia wawekezaji.

“Hampaswi kuendekeza urasimu bali muwe msaada kwa wafanyabiashara na kuangalia ni uwekezaji upi wenye tija katika maeneo yenu ya kazi , hilo litafanikiwa kila mmoja wenu akitimiza wajibu wake,” amefafanua Mhe. Homera.

Ameongeza kuwa Maafisa Biashara ni watu muhimu sana kwenye Halmashari kwani mbali na kusimamia biashara, viwanda na wawekezaji, wanawajibika pia kutoa huduma bora na kupunguza kero kwa wananchi.

Amewataka Maafisa hao kujitathmini tangu walipoingia katika vituo vya kazi  wamefanya nini katika kuhamasisha biashara, viwanda pamoja na uwekezaji kwa kutambua kuwa wao ndiyo engine ya uchumi.

Hata hivyo Mhe. Homera amewataka Wakurugenzi wa Halmashauri kutoa ushirikiano wa kutosha kwa Maafisa Biashara kwa kuwawezesha usafiri wanapotekeleza majukumu yao ili kuleta tija kwani Maafisa hao ni watu muhimu kwenye Halmashauri.

Akizungumzia mafunzo hayo Mhe. Homera amesema anatarajia kuwa utendaji utabadilika na akawataka baada ya mwaka mmoja watoe taarifa kuhusu wawekezaji waliowapata na hii itakuwa ni sehemu ya kutathmini utendaji wao wa kazi.

Mhe. Homera pia ametoa pongezi kwa BRELA kurahisisha utendaji kazi kupitia usajili na utoaji wa leseni kwa njia ya mtandao.

Kwa upande wake Afisa Mtendaji Mkuu wa BRELA  Bw. Godfrey Nyaisa amesema utekelezaji wa Sheria ya Leseni za Biashara ni vyema ukazingatiwa kwa umakini na Maafisa Biashara kwa kuzingatia mipaka ya utendaji kazi ili kutoleta migongano na kuwachanganya wafanyabiashara. 

“Nidhahiri kuwa Maafisa Biashara mnaelewa kuwa Leseni za Biashara kundi A zinapaswa kutolewa na BRELA  na za kundi B zinatolewa na Halmashauri lakini baadhi ya Maafisa Biashara hukiuka utaratibu na kutoa leseni ya Biashara Kundi B kwa mfanyabiashara anayepaswa kupewa leseni ya kundi A, vitendo hivi vinaipotezea Serikali mapato,”anafafanua Bw. Nyaisa.

Leseni za Biashara kundi A hutolewa kwa wafanyabiashara wanaofanya biashara kutoka mkoa mmoja kwenda  mkoa mwingine na hata nje ya nchi na zile za kundi B hutolewa  kwa wale wanaofanya biashara katika  ngazi ya  Halmashauri.

Mafunzo haya ya siku tano yanayofanyika mkoni Mbeya ni mwendelezo wa mafunzo yanayofanyika kikanda kwani kwa mwaka wa fedha 2021/2022 pekee, tayari mafunzo yamekwishafanyika Kanda ya Kati mkoani Dodoma , Kanda ya Ziwa mkoani Mwanza na Kanda inayofuata ni Kanda ya Magharibi mkoani Tabora.

IMETOLEWA NA KITENGO CHA HABARI NA MAWASILIANO BRELA

Previous articleSERIKALI YA TANZANIA YAKARIBISHA WAWEKEZAJI SEKTA YA KILIMO.
Next articleDKT. KIJAJI AIAGIZA FCC KUFANYA TATHIMINI KATIKA SOKO ILI KUBAINI MAPUNGUFU YALIYOPO KATIKA KUMLINDA MTUMIAJI
Hughes Dugilo is a Writer, News Producer, Video-Photographer Journalist, and Video Editor experienced for 20 years now performing in News, Documentary, Advertisements and Television Programs. Aside from all above he own and operate his Blog known as Green Waves Media TZ since 2018.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here