Home BUSINESS ESRF INATEKELEZA MRADI WA LISHE BORA NCHINI

ESRF INATEKELEZA MRADI WA LISHE BORA NCHINI

Dr. Oswald Mashindano kutoka ESRF akifungua semina wakati wa wasilisho la Mradi wa Utafiti katika sekta ya afya kuhusu lishe bora ili kumudu vikwazo vya bei na upatikanaji wa vyakula ikiwemo uhamasishaji wa watu kula vyakula vyenye ubora hapa nchini iliyofanyika hivi karibuni katika Taasisi ya Utafiti wa Kiuchumi na Kijamii (ESRF) jijini Dar es Salaam.

Msimamizi wa Mradi huu Bwana Constantine Manda Mtafiti na Mkurugenzi wa Maabara ya Kutathimini Matokeo akiwasilisha matokeo ya utafiti huo katika semina iliyofanyika kwenye Taasisi ya Utafiti wa Kiuchumi na Kijamii (ESRF) jijini Dar es Salaam hivi karibuni.

Taasisi ya Utafiti wa Kiuchumi na Kijamii (ESRF) kupitia Maabara ya Kutathimini Matokeo (Impact Evaluation Laboratory) inatekeleza Mradi wa Utafiti katika sekta ya afya kuhusu lishe bora ili kumudu vikwazo vya bei na upatikanaji wa vyakula ikiwemo uhamasishaji wa watu kula vyakula vyenye ubora hapa nchini.

Msimamizi wa Mradi huu Bwana Constantine Manda Mtafiti na Mkurugenzi wa Maabara ya Kutathimini Matokeo akizungumza wakati akitoa taarifa ya utafiti huo hivi karibuni amesema Mradi huu wa Utafiti unafadhiliwa na Kituo cha Utafiti wa Maendeleo ya Kimataifa cha Taasisi Kanada (IDRC) unatekelezwa katika Wilaya ya Temeke Jijini Dar es Salaam umelenga kuamgalia sera na soko zima la upatikanaji wa vyakula lakini ikiwemo kuingiza mradi utakaosaidia kupunguza bei ya vyakula ambavyo ni bora kwa lishe ya binadamu kama mbogamboga na matunda.

“Mradi ulianza mwaka 2021 na unatarajia kumalizika mwaka 2024 ukihusisha watafiti wa Kitanzania na wa nje ya Tanzania wakiwemo  watafiti watatu kutoka nchini Marekani ambao  tunashirikiana nao kwa karibu zaidi ikiwa ni pamoja na serikali za mitaa na serikali ya wilaya ya Temeke,” Amesema Bw. Manda.

Bw. Manda amefafanua kuwa utafiti huo unalenga kuangalia ni mambo gani ambayo mtanzania anayafikiria wakati anapokwenda kuchagua, kutafuta, kununua au kufanya uchaguzi ni chakula gani atakachokula siku hiyo. Mradi pia utatafiti ikiwa bei itapunguzwa kwa vyakula hivyo ambavyo ni vizuri kwa lishe ya binadamu  walaji wataendelea kula hata baada ya punguzo hilo kukoma pindi mradi utakapokwisha.

Ameongeza kuwa  matarajio ya   utafiti huo ni kuwa utasaidia kuboresha sera zilizopo au kutunga sera mpya  ili  kushawishi watanzania kula vyakula bora kwa mpangilio ikiwemo mbogamboga  na matunda ili kupunguza au kuondoa kabisa  tatizo la Utapiamlo na Unene uliopindukia.

Naye Mhaziri na Mtafiti kutoka Chuo Kikuu cha Kilimo Sokoine Daktari Theresia Jumbe alisema  ulifanyika utafiti kuangalia hali ya lishe nchini na matokeo ya utafiti ule ulionyesha karibia asilimia 32%  ya watoto nchini waliokuwa na umri wa chini ya miaka 5 walionekana wana udumavu hasa katika mikoa ya nyanda za juu kusini, kanda ya ziwa na kanda ya kati ambapo katika mikoa ya kanda ya kati, mikoa ya Dodoma na Singida ndio ilionekana kuwa imeathirika Zaidi.

Aidha amefafanua kuwa  utafiti huo unaonyesha Kanda ya Mashariki mikoa ya Pwani na  Dar es Salaam  na Kanda ya Kaskazini mkoa wa Kilimanjaro  inaonesha wanawake wengi ambao wako kwenye umri wa kuzaa wana Kiriba Tumbo na Unene uliopindukia hayo yote yametokea baada ya kupitia nyaraka za tafiti mbalimbali zilizowahi kufanyika kuhusu lishe ambazo pia zinaonesha wanawake wengi wajawazito na watoto wanapata changamoto ya upungufu wa damu hasa kanda ya ziwa.

“Kimsingi tunayo matatizo matatu katika utapiamlo tunao  Utapiamlo kwa maana ya Uzito Umezidi, Tunao Utapiamlo kwa maana ya Upungufu Lishe na Utapiamlo kwa maana ya upungufu wa madini na vitamini ambazo ni muhimu sana kwa lishe ya binadamu, ” Amesema Dk. Theresia Jumbe

Ameongeza kuwa changamoto nyingine ni upatikanaji wa vyakula kwa maana ya kwamba vyakula vilivyo vingi hapa nchini kwa sasa ni vya nafaka  kama vile Ugali , Wali na Muhogo  ikiwemo ulaji wa vyakula vyenye  mafuta, Sukari na vinginevyo jambo ambalo linachangia sana watu kuwa na unene au uzito uliopindukia.

Ni muhimu sasa wadau wote kwa pamoja hasa wale wanaoshiriki katika mnyororo wa upatikanaji wa chakula kama vile wazalishaji , wachakataji, wasafirishaji mpaka wauzaji pamoja na  watunga sera kujipanga ili kuhakikisha  mlaji anapata chakula kilicho bora na kwa bei iliyo nafuu ili waweze kuboresha afya zao.

Naye Mtafiti Danford Sango kutoka Idara ya Kujenga Uwezo ESRF akizungumzia kuhusu sera amesema utafiti huo umeangalia sera kwa ujumla namna zinavyoweza kumfanya mtanzania kupata vyakula vyenye virutubisho na lishe hasa kwa jamii ya maisha ya kawaida ikiwa ni pamoja na kuona kwamba kama sera zilizopo zinakuwa kikwazo kwa mtu wa kawaida kupata chakula chenye kumfanya apate mlo wenye lishe bora ziweze kuangaliwa na kurekebishwa au kutungwa zingine kulingana na hali iliyo ili kuokoa watu wengi wenye shida ya utapiamlo.

  Mhaziri na Mtafiti kutoka Chuo Kikuu cha Kilimo Sokoine Daktari Theresia Jumbe akielezea viashiria mbalimbali vilivyoonekana kuhusu Utapiamlo katika maeneo mbalimbali nchini.

  Mmoja wa watafiti walioshiriki Ifakara akichangia mada katika semina hiyo.

Dr. Allan De Braw kutoka IFPRI akichangia baadhi ya mambo mara baada ya wasilisho la utafiti huo.

Washirikimbalimbali wakiwa katika semina hiyo.

Mtafiti Danford Sango kutoka Idara ya Kujenga Uwezo ESRF akizungumzia kuhusu sera mbalimbali zinazohusu masuala ya lishe.

 

Bw Said Rashid Mtafiti Msaidizi kutoka Taasisi ya Utafiti wa Kiuchumi na Kijamii (ESRF) akifafanua jambo wakati alipowasilisha moja ya hoja zinazohusu utafiti huo.

   

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here