Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Uwekezaji, Viwanda na Biashara Dkt. Hashil Abdallah kwa niaba ya Katibu Mkuu Prof. Godius Kahyarara ameongoza mkutano wa ngazi ya wataalamu ulioshirikisha wadau mbalimbali kutoka upande wa Tanzania na Kenya kujadili Vikwazo visivyo vya kiushuru (NTB’s) vilivyopo baina ya nchi hizi mbili.
Kikao hicho kilichofanyika leo tarehe 11 Machi, 2022, Zanzibar ni muendelezo wa Vikao kuanzia ngazi ya wataalamu tarehe 9 Machi, 2022 vilivyoshirikisha nchi ya Tanzania na Kenya na tarehe 12 Machi, 2022 ni ngazi ya Mawazili wa sekta husika baina ya Tanzania na Kenya watakaokutana kwa ajili ya kuja na majibu ya pamoja kuhusu umalizwaji wa Vikwazo visivyo vya kiushuru.
Dkt. Abdallah kwa niaba ya kuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Uwekezaji, Viwanda na Biashara Prof. Godius Kahyarara amesema ana Imani kubwa na kamati hiyo iliyohusisha wataalamu wa Tanzania na Kenya katika kuhakikisha wanafanya majadiliano kwa kina na kitaalamu zaidi ili kufikia makubaliano ya kuondoa vikwazo hivyo ili kurahisisha biashara baina ya nchi hizi mbili.
Dkt. Abdallah amesema kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan pamoja na Rais wa Serikali ya Jamhuri ya Kenya wamekuwa wakijadiliana namna bora ya kumaliza changamoto hizi za kibiashara ili kukuza biashara na kuchochea uchumi wa Tanzania na Kenya kukua kwa kasi na kutumia vizuri masoko ya SADC, AGOA na AfCFTA.
Naye Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo na Mifugo kutoka Serikali ya Jamhuri ya Kenya Bw. Harry Kimutai amesema kuwa ni wakati sasa wa Tanzania na Kenya kuonesha mshikamano uliokuwepo kipindi kirefu.
Bw. Kimutai ameongeza kuwa Tanzania na Kenya zimekuwa na mahusiano mazuri ya kibiashara kwa kipindi kirefu na changamoto hizi zimekuwa zikifanyiwa kazi na kupunguzwa mara kwa mara hivyo amesema ni wakati sasa wa kuionesha Afrika na Dunia kwa ujumla kuwa nchi hizo ni ndugu.
Kikao hiki kimehudhuria na Viongozi mbalimbali kutoka Jamhuri ya Muungano wa Tanzania akiwemo Katibu Mkuu wa Wizara ya Biashara na Maendeleo ya Viwanda kutoka Serikali ya Mapinduzi Zanzibar Dkt. Islam Seif, Katibu Mkuu anayeshughulikia biashara kutoka Wizara ya Viwanda, Biashara na Maendeleo ya Ujasiliamali kutoka Kenya Dkt. Bruno Linyiru, Mhe. Balozi Fatma Mohamed Rajah Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki kutoka Tanzania na Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Maliasili na Utalii Bw. Juma S. Mkomi wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar