Home LOCAL BILIONI 12 KUBORESHA MIUNDOMBINU NA HUDUMA YA MAJI MKOANI MTWARA

BILIONI 12 KUBORESHA MIUNDOMBINU NA HUDUMA YA MAJI MKOANI MTWARA

 
Diwani wa kata ya Mikangaula Halmashauri ya wilaya Nanyumbu mkoani Mtwara Abdul Chiwili kushoto akimtwisha ndoo ya maji mkazi wa kijiji cha Mkwajuni Clara Simon katika moja ya vituo vya kuchotea maji viilivyojengwa na Wakala wa maji safi na usafi wa mazingira vijijini Ruwasa mkoa wa Mtwara ambapo Serikali kupitia wizara ya maji imetoa zaidi ya Shilingi bilioni 12 kwa ajili ya kujenga miradi mipya ya maji,kuboresha na kuimarisha huduma ya maji safi na salama katika mkoa huo.

Na: Muhidin Amri, Mtwara

SERIKALI kupitia wizara  ya maji imetenga jumla ya Sh.12,523,727,274.27 kwa mwaka wa fedha 2021/2022 ambazo zitatumika kujenga,kukarabati  na kufanya upanuzi wa miradi  mbalimbali ya maji katika mkoa wa Mtwara.

Meneja wa wakala wa usambazaji maji safi na usafi wa mazingira vijijini(Ruwasa)mkoa wa Mtwara Primy Damas, alisema hayo jana wakati akitoa taarifa ya utekelezaji wa miradi  mbalimbali ya maji katika mkoa huo.

Anataja mgawanyo wa fedha hizo kwa kila wilaya kuwa Masasi Sh.2,484,329,885 Mtwara imepokea Sh.3,367,250,973.27,Nanyumbu Sh.2,132,694,811, wilaya ya Newala Sh.2,079,857,372 na Tandahimba imepokea Sh.2,459,594,233.

Damas anaeleza kuwa, kwa sasa katika mkoa huo wananchi wanaopata huduma ya maji  kwa wakazi wa vijijini ni 672,672 sawa na asilimia 60.16 na mijini watu  282,945 sawa na asilimia 82.

Alisema, vyanzo vyote vilivyoendelezwa kwa pamoja vinauwezo wa kuzalisha lita 21,186,300 kwa siku ukilinganisha na mahitaji ya maji ambayo ni lita 46,088,340 ambapo uzalishaji huo ni  sawa na asilimia 46 ya mahitaji.

Alisema,  uwezo wa vyanzo vya maji  vilivyopo  ni kuzalisha maji mita za ujazo milioni 14,947 kwa mwaka na maji yanayotumika ni mita za ujazo milioni 2,661 kwa mwaka sawa na asilimia 17.80.

Meneja  huyo alisema,ongezeko  la utoaji wa huduma ya maji kwa wananchi waishio vijijini imekuwa inaongezeka kwa kasi kidogo ikilinganisha na kasi ya ongezeko la watu  na hali hiyo inatokana na uwekezaji mdogo uliokuwa unafanywa na serikali katika sekta ya maji.

Anabainisha kuwa,Mkoa ulikuwa na lengo la kufikisha asilimia 64 ya utoaji wa huduma ya maji kwa wakazi waishio vijijini,hata hivyo katika kipindi  husika hali imeongezeka kutoka wastani wa asilimia 59.53(Mwezi Juni 2020) hadi kufikia asilimia 60.16.

Kwa mujibu wa Damas,hatua hiyo inatokana na nguvu kubwa ya uwekezaji wa miundombinu ya maji unaofanywa na Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan kutekeleza mipango mbalimbali katika mkoa huo.

Alisema, kutokana na uwekezaji unaofanywa  katika sekta ya maji mkoani Mtwara,ni matumaini ya Ruwasa kwamba  huduma ya maji itazidi kuongezeka hadi kufikia malengo yaliyowekwa na Serikali pamoja na Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi kwa kuwa miradi mingi imeanza kutekelezwa.

Damas alisema,katika kuhakikisha upatikanaji wa huduma ya maji kwa wananchi unaendelea kuboreshwa,Ruwasa  inaendelea kuwezesha, kusimamia ujenzi na kukamilisha miradi ya maji vijijini katika maeneo mbalimbali ya wilaya husika kupitia fedha za Mfuko wa Taifa wa Maji(NWIF)na mipango ya lipa kwa matokeo(P4R)na lipa kabla ya matokeo(PbR).

Hata hivyo alisema, pamoja na  jitihada mbalimbali zinazoendelea kufanywa na Serikali katika kuboresha huduma ya maji kwa wananchi waishio vijijini, bado kuna chagamoto kadhaa zinazoikabili sekta ya maji katika maeneo husika.

Anataja changamoto hizo ni uwekezaji mdogo katika ujenzi wa miradi  mipya na uboreshaji wa miradi iliyopo,uharibifu wa vyanzo vya maji kutokana na shughuli za kibindamu,uchangiaji duni wa wananchi katika huduma wanayoipata na kukosekana kwa vyanzo vya uhakika vya maji katika baadhi ya maeneo ya mkoa wa Mtwaraa hasa wilaya ya Nanyumbu.

Alisema,Serikali kupitia wataalam mbalimbali wa sekta ya maji katika mkoa wa Mtwara imejiwekea mikakati  mbalimbali ya utatuzi wa changamoto zilizopo pamoja na kuongeza utoaji huduma ya maji kwa wananchi.

Anataja baadhi ya mikakati hiyo ni pamoja na kuiomba Serikali, kuongeza bajeti ya uwekezaji wa ujenzi wa miundombinu ya maji katika maeneo mbalimbali vijijini,pamoja na wafadhili na wadau mbalimbali wa uboreshaji wa sekta ya maji kwa jamii.

Mikakati mingine ni kusimamia na kuimarisha vyombo vya watumia maji vijijini kwa lengo la kusimamia,kuchangia na kuendesha miradi hiyo,kushirikisha wataalam husika na wananchi  kwa ajili ya kutunza na kuhifadhi vyanzo vya maji, na kutoa elimu ya dhana ya umiliki wa miradi ya maji kwa jamii.

Alisema, kabla ya kuanzishwa kwa Ruwasa hali ya Utekelezaji wa miradi ya maji  ilikuwa mbaya licha ya Serikali kutoa fedha kwa wakandarasi  na pia  gharama ya miradi husika  ilikuwa kubwa tofauti na uhalisia.

Alisema, kwa sasa hali ni tofauti baada ya Ruwasa kuanza kutumia wataalam wake,hatua anayotaja imesaidia sana miradi mingi kukamilika kwa wakati,kupungua kwa gharama za utekelezaji na wananchi kuanza kupata huduma.

Damas ameipongeza serikali ya Chama cha Mapinduzi, kutoa fedha kwa Wizara ya Maji ili kutekeleza miradi  katika maeneo mbalimbali ambayo imesaidia  kupeleka na kuboresha huduma  ya maji kwa wananchi wa mkoa wa Mtwara.

Amewataka wananchi wa mkoa wa Mtwara,  kuhakikisha wanatunza  miundombinu ya maji,vyanzo  vya maji na mazingira  ili viweze kudumu kwa muda mrefu na kuleta tija iliyokusudiwa.
MWISHO.

Previous articleMSEMAJI MKUU WA SERIKALI AIPONGEZA NCAA KWA UHIFADHI WA NGORONGORO
Next articleMO DEWJI KUFADHILI MASOMO YA UDAKTARI BINGWA WA UPASUAJI WA UBONGO
Hughes Dugilo is a Writer, News Producer, Video-Photographer Journalist, and Video Editor experienced for 20 years now performing in News, Documentary, Advertisements and Television Programs. Aside from all above he own and operate his Blog known as Green Waves Media TZ since 2018.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here