Mojawapo ya anwani ya makazi ya awali iliyowekwa katika jengo mojawapo lililopo kata ya kati mtaa wa Pangani.
NA: NAMNYAK KIVUYO, ARUSHA.
Zoezi la uwekaji anwani za makazi jiji la Arusha limeanza rasmi katika kata tano za halmashauri hiyo ambazo ni kata ya Kati,Themi , Levolosi, Sekei na Kaloleni lengo likiwa ni kuweza kutekeleza zoezi Hilo katika kata zote 25.
Akiongea na waandishi wa habari mwenyekiti wa mtaaa wa corridor area kata ya Themi Chambi Agrey Kashimbiri alisema kuwa muamko wa wananchi katika kutoa ushirikiano juu ya zoezi hilo ni mkubwa na baadhi ambao hawana uwelewa baada ya kueleweshwa na kujua manufaa wamelifurahia zoezi Hilo.
“Mpaka Sasa tumeweza kuzifikia nyumba 40 lakini wapo wenzetu waliopo katika mitaa mingine na tutakapo kutana jioni naamini tutakuwa tumezifikia nyumba nyingi zaidi na tutaweza kulimaliza zoezi hili la kuweka anwani za makazi kwa muda tuliopangiwa ambapo tunatakiwa kulikamilisha Februari 28 kwa kata hii,” Alisema Chambi.
“Tumegundua kuwa watu hawana uelewa lakini tunavyopita na kuwaelimisha wanalifurahia sana kwani tunawaeleza manufaa ya zoezi hili na kutokana na umuhimu wake wanatupa ushirikiano bila shaka yoyote kuliko mambo mengine tuliyowahi kuyafanya katika mtaa,” Alieleza.
Kwa upande wake mwenyekiti wa mtaa wa Pangani kata ya Kati Ismail Halili alisema kuwa zoezi linaenda vizuri na muamko wa wananchi ni mkubwa kwani hwajapata usumbufu sana na wanashirikiana kwa pamoja kuhakikisha zoezi hilo la anwani za makazi linakamilika.
Awali mkurugenzi wa jiji la Arusha Dkt John Pima akifunga mafunzo yaliyotolewa kwa watu wanaotekeleza zoezi hilo katika kata hizo alisema kuwa hawatamvumilia mtu yoyote kati ya waliyopewa kazi hiyo atayeenda kuhujumu au kukwamisha zoezi hilo hivyo wakashirikiane na kuheshimiana na hao wanaotakiwa kwenda kuwasimamia.
Dkt Pima aliwataka kwenda kujituma na kiwajibika ipasavyo kwani zoezi hilo litafanya nchi kuingia katika historia nyingine nzuri kwani mataifa mengi yaliyoendekea yanatumika anwani za makazi katika mambo mengi.
Hata hivyo manufaa ya mfumo huo ni kurahisisha utoaji, upatikanaji na upelekaji wa huduma kwa wananchi au wateja, Kuongeza wa ukusanyaji mapato, kuongeza ajira, kuimarisha ulinzi na usalama, kurahisisha upatikanaji wa huduma majumbani pamoja na Kuimarisha biashara kwa njia ya mtandao.