Home BUSINESS WAKULIMA WA KOROSHO TUNDURU WAUZA KILO MILIONI 25,284,493

WAKULIMA WA KOROSHO TUNDURU WAUZA KILO MILIONI 25,284,493

Meneja Mkuu wa Chama Kikuu cha Ushirika wilayani Tunduru(Tamcu Ltd) Iman Kalembo akitoa taarifa ya uzalishaji wa zao la korosho kwenye kikao kazi cha mpango wa kuchangia pembejeo kwa wakulima wa zao hilo kilichofanyika katika Ukumbi wa Klasta ya Walimu mjini Tunduru ambapo jumla ya kilo milioni 25 zimeuzwa kupitia minada mbalimbali.


Baadhi ya wenyeviti wa vyama vya msingi vya ushirika(Amcos)wilayani Tunduru wakimsikiliza Mkuu wa wilaya hiyo ambaye pia ni Mwenyekiti wa mfuko wa Pembejeo Julius Mtatiro(hayupo pichani)wakati wa kikao kazi cha mpango wa kuchangia pembejeo kwa wakulima wa korosho wilayani humo.

Na: Muhidin Amri,Tunduru

WAKULIMA wa korosho mkoani Ruvuma wanaohudumiwa na Chama Kikuu cha Ushirika wilayani Tunduru(Tamcu Ltd), wamefanikiwa kuvuka lengo la uzalishaji  kutoka kilo 24,000,000 msimu wa kilimo 2020/2021  hadi kufikia kilo 25,284,493  katika msimu 2021/2022.

Hayo yamesemwa jana na Meneja Mkuu wa Chama hicho Imani Kalembo, wakati akitoa taarifa ya uzalishaji na uuzaji wa korosho kupitia minada 13, katika kikao kazi cha mpango wa uchangiaji wa Pembejeo za wakulima kwa msimu wa kilimo 2022/2023.

Kalembo alisema, uzalishaji huo ni mafanikio makubwa tofauti na msimu wa mwaka 2020/2021 ambapo malengo yalikuwa kuzalisha  kilo milioni 25, hata hivyo walizalisha kilo milioni 24.

Kwa mujibu wa Kalembo,mafanikio hayo yametokana na matumizi sahihi ya pembejeo  ikiwamo Salphur,viuatilifu bora na wakulima kuzingatia maelekezo ya wataalam wa  kilimo.

Kikao hicho kilichoongozwa na Mkuu wa wilaya hiyo Julius Mtatiro, kilihudhuriwa na Wenyeviti wa vyama vya msingi vya Ushirika(Amcos)Makalani na Wajumbe wa Chama Kikuu cha Ushirika Tamcu kilifanyika katika Ukumbi maarufu wa Klasta mjini Tunduru.

Kalembo, amewaeleza viongozi hao kwa niaba ya wakulima kuwa, utaratibu  wa kuchangia pembejeo una faida nyingi  ikiwamo uhakika wa kupata pembejeo kwa gharama nafuu  ambapo mkulima atachangia asilimia 50  na Serikali itatoa asilimia 50.

Aidha alisema,utakomesha vitendo vya kitapeli kwa baadhi ya watu ambao kila msimu wanajipatia pembejeo hasa Sulphar bila kuwa na mashamba ya korosho na kwenda kuuza kwa wafanyabiashara kwa lengo la kujipatia fedha.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Tamcu Mussa Manjaule amewahakikishia  wanachama wa Amcos kuwa,mpango huo utaongeza uzalishaji wa zao la korosho katika msimu 2022/2023 kwa kuwa wakulima watakuwa na uhakika wa kupata pembejeo zilizo bora na kwa wakati na kuwaomba  kuchangia kwa wingi ili wanufaike na punguzo la asilimia 50.

Manjaule ambaye ni mjumbe wa Bodi ya Korosho  Tanzania,amewataka viongozi wa Amcos kwenda kuwashirikisha viongozi wa Serikali katika maeneo yao ili waweze kuwasaidia kufanikisha utekelezaji wa mpango huo badala ya kufanya kazi kwa kujificha.

Ameiomba Serikali kuwasaidia viongozi wa Amcos kutoa elimu kwa wakulima kuhusu umuhimu wa kuchangia pembejeo hizo,badala ya kuwaachia viongozi  hao kwenda kuhamasisha mpango huo ambao unakusudia kuongeza uzalishaji wa korosho  katika wilaya hiyo.

Mkuu wa wilaya ya Tunduru Julius Mtatiro, ametaja faida za kuchangia pembejeo kwa wakulima ni pamoja na kudhibiti  biashara haramu ya viuatilifu inayofanywa na baadhi ya watu wachache na utasaidia viongozi wa Amcos kuwatambua wanachama wenye mashamba na wasio na mashamba.

Pia,ameagiza utaratibu wa kuchangia pembejeo kwa wakulima kuwa ajenda ya kudumu katika wilaya hiyo na elimu inatolewa kwenye mikutano mbalimbali ya vijiji na kata ambapo amewataka wataalam wa idara  katika Halmashauri ya wilaya kuhakikisha kila wanapofanya mikutano ya maendeleo wanaeleza  faida ya mpango huo.

Amewaasa viongozi wa vyama vya msingi, kufanya kazi kwa uaminifu,kufuata misingi na maadili katika utendaji wa kazi za kila siku na kuepuka  vitendo vya wizi vinavyosababisha wanachama kutokuwa na imani kwa  viongozi wao.

Aidha ametoa muda wa wiki moja kwa viongozi wa Amcos wilayani humo, kumaliza changamoto zilizopo kwenye vyama vyao kabla Serikali haijaanza kuchukua hatua dhidi yao na kuepuka  kutafuta ugomvi na Serikali kwa kufanya mambo kinyume na sheria na taratibu zinazoongoza vyama vya ushirika.

Katika hatua nyingine Mtatiro alisema,mikakati madhubuti ya Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan kutoa pembejeo na viuatilifu bure kwa wakulima umesaidia  kuongeza uzalishaji wa korosho katika wilaya  hiyo na mkoa wa Ruvuma.

Alisema, kwa mara ya kwanza wilaya ya Tunduru imefanikiwa kuingiza sokoni korosho zote daraja la kwanza na kuwataka viongozi wa Amcos kwenda kutoa elimu kwa wanachama juu ya kuzalisha korosho bora  ambazo zitauzwa kwa bei ya juu ambayo itawanufaisha wakulima  na kuwa na uhakika wa kupata fedha.

Amempongeza Rais Samia Suluhu Hassan,kwa kuteua wasaidizi wazuri akiwamo Waziri wa kilimo Hussen Bashe ambaye ni mhimili mkubwa katika sekta ya kilimo hapa nchini ambapo  kutokana na mikakati ya wizara  ya kilimo,wilaya  ya Tunduru ina matumaini makubwa ya kuendelea kuongoza katika uzalishaji wa zao la korosho Tanzania.
MWISHO.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here