Home BUSINESS TANZANIA KUWAVUTIA WAWEKEZAJI KWENYE SIKU YA TANZANIA MAONESHO YA EXPO 2020 DUBAI

TANZANIA KUWAVUTIA WAWEKEZAJI KWENYE SIKU YA TANZANIA MAONESHO YA EXPO 2020 DUBAI

Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imejipanga kuendelea kuwavutia Wawekezaji kwenye Siku maalum ya Tanzania kwenye Maonesho ya Expo 2020 Dubai ambapo lengo la siku hiyo ni kuitangaza nchi ya Tanzania kwenye Maonesho hayo makubwa Duniani yanayoshirikisha nchi 192.

Hayo yamesemwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Uwekezaji, Viwanda na Biashara Prof. Godius Kahyarara leo tarehe 01 Februari , 2022 Jijini Dar es Salaam wakati akiongoza kikoa cha Maandalizi ya Siku ya Tanzania kwenye Maonesho ya Expo 2020 Dubai kilichoshirikisha viongozi wa Taasisi za Serikali na Sekta Bianfsi. 

Prof. Godius Kahyarara amesema kuwa Siku ya hiyo inalenga kutangaza miradi mikubwa ya uwekezaji hivyo amezitaka Taasisi zinazoshiriki kwenye Siku hiyo kuhakikisha zinakuwa na taarifa kutosha za miradi ili kuwashawishi wakezaji kuwekeza nchini. 

Prof. Kahyarara ameongeza kuwa sisi kama waandaaji tunapaswa kuwa na taarifa za kutosha na za kina za fursa za uwekezaji zilizopo nchini ili kupata wawekezaji kuja kuwekeza nchini Tanzania na sio kutoa taarifa ambayo haijitoshelezi.

“Taasisi zote zifanye maandalizi mazuri ya kutangaza fursa katika miradi mbalimbali ili ilete manufaa makubwa kwa nchi yetu kupitia Siku hiyo na Kongamano la Biashara ambalo litawakutanisha wawekezaji na wafanyabiashara ” alisema Prof. Godius Kahyarara

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TanTrade) Bi. Latifa Khamis ambao ndio waratibu wa ushiriki wa Tanzania kwenye Maonesho hayo alieleza kuwa kwenye Maonesho ya EXPO 2020 Dubai kila Nchi inapewa fursa ya kuandaa Siku ya Kitaifa kwenye Maonesho hayo ili kujitangaza ambapo siku maalum ya Tanzania itakuwa tarehe 26 Februari, 2022 na Mgeni rasmi anatarajiwa kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan.

Bi. Latifa ameongeza kuwa kwenye siku hiyo mgeni Rasmi anatarajiwa kutembelea Banda la Tanzania, Banda la Wanawake (Women Pavilion) pamoja na banda la “ Nature Pavilion “ na siku hiyo itapambwa na burudani kutoka kwa wasanii wa Tanzania na anatarajiwa kuhudhuria kwenye Kongamano la Biashara na Uwekezaji linalotarajiwa kufanyika siku ya Tarehe 27 Februari, 2022 ambapo, atahutubia na kushuhudia utiaji wa saini wa mikataba ya Biashara na Uwekezaji kwenye Kongamano hilo.

Aidha Bi. Latifah amesema Kongamano hilo litatoa tathmini ya tulichofanikiwa katika Maonesho hayo ya Expo 2020 Dubai toka yalipoanza tarehe 01 Oktoba, 2021 na litatoa fursa kwa Wafanyabiashara wa Tanzania kukutana na Wafanyabiashara kutoka Nchi mbalimbali sambamba na kuendelea kutangaza fursa za uwekezaji zinazopatikana Nchini Tanzania.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Taasisi ya Sekta Binafsi Tanzania (TPSF) Bi. Angelina Ngalula amesema Siku hiyo sio ya Serikali peke yake ni shughuli ya Kitaifa ambayo Taasisi za Serikali na Sekta Binafsi zinapaswa kushirikiana katika kupanga ajenda zitakazotoa nafasi kwa Sekta Binafsi kuunganishwa na fursa za Biashara na Uwekezaji.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here