TRANSFOMA kubwa ya kisasa yenye uwezo wa Megawati 58 ambayo imegharimu fedha Sh.bilioni 2.5 imewasha rasmi leo Februari 24,2022 katika Kituo cha kupoza Umeme cha Shirika la Umeme Tanzania(TANESCO)kilichopo Kunduchi mkoani Dar es Salaam, ikiwa ni sehemu ya mkakati ya Shirika hilo kutatua changamoto ya kukatika kwa umeme kwa wateja wanaohudumiwa na kituo hicho.
Akizungumza na waandishi wa habari baada ya kuwashwa rasmi kwa transfoma hiyo, Mhandisi Mkuu wa Usafirishaji Umeme Kanda ya Mashariki-TANESCO Mhandisi Nemes Didas amesema kuanza kutumika kwa trasnfoma hiyo kunakwenda kuondoa changamoto ya kukata umeme wakati wa matengenezo ya transfoma zilizopo kituoni hapo.
“Kabla ya transfoma hii ambayo tumeiwasha leo kuanza kutumika, tulikuwa na transfoma mbili, kila mmoja ina Megawati 58, hivyo kwa transfoma hizo mbili tulikuwa na jumla ya Megawati 116, na tulipokuwa kufanya matengezo ya transfoma moja ilitubidi baadhi ya maeneo wateja wetu wakose umeme ili kuipunguzia mzigo.
“Sasa leo tumewasha transfoma ya tatu ambayo ujenzi wake umechukua miezi 12 hadi kukamilika, uwezo wake ni Megawati 58, kwa maana hiyo hata tukiamua kufanya matengenezo ya transfoma mojawapo basi mbili zitaendelea kuwahudumia wateja wetu wote,hivyo hakutakuwa na kukatika kwa umeme au umeme kuwa chini,”amesema Mhandisi Didas.
Amefafanua Kituo cha Kunduchi kinahudumia wateja wa Mbezi Beach, Tegeta, Bagamoyo ,Jangwani Beach na maeneo mengine , hivyo ni kituo muhimu kwa wateja Shirika hilo na kuanza kwa kutumika kwa transfoma hiyo mpya kunafanya kuwepo na umeme megawati 174 wakati mahitaji ya wateja wao waliopo sasa ni megawati 66, hivyo kuna ziada ya umeme megawati 110.
Akielezea zaidi kuhusu kituo hicho amesema kinapokea umeme kutoka Kituo kikubwa cha Ubungo kupitia laini mbili za msongo wa kilovoti 132 ambazo zikishafika kwenye kituo hicho zinapoozwa na baada hapo unatoka umeme wa msongo wa kilovoti 33 ambazo ndizo zinakwenda kwa wateja.
Mhandisi Didas amesema kituo hicho cha Kunduchi ndicho kinachopeleka umeme Zanzibar kupitia ‘Cable’ zinazopita chini bahari huku akitumia nafasi hiyo kutoa mwito kwa wananchi wanaohudumiwa na kituo hicho wafahamu kwamba sasa umeme uko wa uhakika , hivyo wenye viwanda wawekeze kwasbabu hakutakuwa na changamoto ya nishati ya umeme.
“Umeme tunao wa kutosha kwa hiyo tunatoa rai wenye viwandsa waje wawekeze kwa kujenga viwanda kwani umeme upo wa kutosha.Tanzania ya viwanda inawezekana na TANESCO tumejipanga katika kuhakikisha tunawahudumia wananchi,” amesema Mhandisi .
IMEANDALIWA NA: Saidi Mwishehe Msagala, MICHUZI BLOG.