Home LOCAL STAMICO YAENDELEA KUTATUA CHANGAMOTO ZA WACHIMBAJI WADOGO

STAMICO YAENDELEA KUTATUA CHANGAMOTO ZA WACHIMBAJI WADOGO


Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) limeendelea kutatua changamoto za kiuchimbaji kwa wachimbaji wadogo wenye usikuvu hafifu kwa kuwapa mafunzo ya uchimbaji salama, biashara ya madini na utunzaji mazingira yaliyofanyika katika wilayani Bukombe, Mkoa wa Geita.

Akiongea kwa niaba ya Mgeni Rasmi Mkuu wa Wilaya ya Bukombe, Katibu Tawala wa Wilaya Bw. Paul Cheyo  amesema mafunzo haya yameleta tija sana kwa wachimbaji wadogo kwa kuwa yametoa nafasi ya wao kujifunza mbinu mpya za kiuchimbaji na kuachana na uchimbaji duni.

Ameipongeza STAMICO kwa kutambua thamani ya watu wenye mahitaji maalumu na kuja na mbinu hii mpya ya kutoa elimu kwa wachimbaji hawa wenye usikivu hafifu. Makundi haya ya walemavu wana uwezo wa kufanya kazi lakini wanasahaulika kushirikishwa katika fursa kama hizi.

Ametoa wito kwa STAMICO kutanua wigo wa kutoa elimu hii ili kuweza kuwafikia wachimbaji wengi zaidi. Amewataka wachimbaji  wadogo wa Bukombe kutumia fursa ya mafunzo haya ili kuweza kuboresha shughuli  zao za uchimbaji na kuleta maendeleo.

Akiongea kuhushu mafunzo hayo, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa STAMICO Dkt. Venance Mwasse amesema mafunzo haya ni sehemu moja wapo ya utekelezaji wa mpango wa Shirika wa kuwaendeleza wachimbaji wadogo kwa kuwa wanahitaji kupata mafunzo ya uchimbaji wenye tija.

STAMICO imeandaa mpango maalumu wa kuwasaidia na kuwarasimisha wachimbaji wadogo kutatua  changamoto zao ambazo zimebainika kupitia tafiti mbalimbali zilizofanywa na Shirika. 

Amesema STAMICO inatekeleza mpango huo kwa hatua ambapo hadi sasa jitihada za utekelezaji wa mpango huo ni pamoja na kutengeneza mazingira wezeshi ya wachimbaji wadogo kukopesheka, kupata taarifa za kijiolojia na kuwawezesha wachimbaji wadogo kupata Madawa na Kemikali za uchenjuaji kwa kurahisisha  upatikanaji wa bidhaa hizi.

Kwa sasa bidhaa hizi zimeanza kupatikana kati vituo vya mfano vya wachimbaji wadogo vilivyopo mikoa ya Geita na Mbeya.

Aidha Shirika limepanga kununua mitambo mitano ya uchorongaji ambayo itakayoendana na mahitaji ya wachimbaji wadogo ili kuwarahishia kupata taarifa sahihi zitakazowawezesha kufanya uchimbaji wenye tija.

Naye Meneja wa Uchimbaji Mdogo wa STAMICO Bw. Tuna Bandoma amewataka washiriki wa mafunzo haya  kuacha kutumia tafiti duni za madini na badala yake watumie  teknolojia ya kisasa ikiwepo kufanya utafiti wa kina ili kuweza  kupata matokeo chanya kwa kuwa tafiti duni zinawasababishia kufanya uchimbaji wa muda mrefu bila mafanikio.

Bw. Bandoma amesema  utafiti huu wakina huwa unatoa matokeo ya uhakika hususani wanapotumia mitambo ya  uchorongaji kwa kuwa mitambo hii inauwezo wa kuzama chini ya ardhi kuanzia mita 200 hadi 1,000 wakati wa kuchukua sampuli hali inayoleta taarifa sahihi za rasirimali zilizomo katika eneo la mchimbaji.

Miongoni mwa wachimbaji wenye usikivu hafifu toka wilaya Mbogwe Bw. Lucas Mugunu amesema mafunzo haya yanawasaidia katika kuendelea na uchimbaji wa madini ya dhahabu kwa njia bora zaidi hasa baada ya kupata mafunzo aliyopata mkoani Geita

Hii ni mara ya tatu STAMICO kutoa mafunzo kama haya kwa kundi la wachimbaji wenye usikivu hafifu. Mikoa mingine ambayo mafunzo haya yamefanyika ni pamoja na Mikoa ya Geita na Mbeya.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here