Home BUSINESS PROF. GODIUS KAHYARARA AWAKUTANISHA WADAU WA SEKTA YA CHUMA NCHINI KUJADILI CHANGAMOTO...

PROF. GODIUS KAHYARARA AWAKUTANISHA WADAU WA SEKTA YA CHUMA NCHINI KUJADILI CHANGAMOTO YA KUPANDA BEI YA BIDHAA HIYO JIJINI DAR

 

Katibu Mkuu Wizara ya Uwekezaji, Viwanda na Biashara Prof. Godius Kahyarara leo Tarehe 01 Februari, 2022 amewakutanisha wadau wa bidhaa za chuma waliowekeza nchini Tanzania na kujadiliana nao changamoto ya mabadiliko ya bei katika bidhaa za Nondo, Mabomba na Mabati.

Prof. Kahyarara ameanza kwa kuwapongeza wazalishaji wa bidhaa za chuma kuongeza uzalishaji siku hadi siku na wamekuwa na mchango mkubwa katika ujenzi wa nchi hii kwani Serikali ya awamu ya sita imekuwa ikitekeleza miradi mikubwa ya Majengo, Barabara, Nishati, Miundombinu ya Umeme, Maji na Shule kwa kutegemea bidhaa wanazozalisha.

Prof. Kahyarara Amesema kuwa miradi hii yote ya Serikali imekuwa ikifanyika kwa kutegemea Nondo, Mabati na Mabomba kutoka ndani ya nchi ambayo imepelekea kukua kwa sekta hii na kuongeza mapato ya nchi.

Aidha, Prof. Kahyarara amesema kuwa maoni watakayotoa yataisaidia Serikali kuchukua hatua nzuri itakayosaidia kuondoa changamoto ya mabadiliko ya bei ili kusaidia wananchi kupata bidhaa hii kwa gharama nafuu.

Nao wazalishaji wa bidhaa hiyo nchini wamesema kuwa uzalishaji wa bidhaa za chuma ambazo ni Nondo, bomba na Mabati unakumbwa na changamoto nyingi ikiwemo kuchelewa kwa malighafi zinazotoka nje ya nchi, changamoto ya Umeme kukatika mara kwa mara (Unstable power), kupanda kwa bei ya chuma chakavu zinazokusanywa ndani na nje ya nchi, sheria za taasisi za udhibiti na gharama ya usafirishaji wa billets kupanda.

Wazalishaji wa bidhaa za Chuma walioshiriki kikao hiki ni pamoja na Iron and Steel Ltd, Lodhia Steel Ltd, Alaf Limited, MMI, FMJ Hardware Ltd, Kamal Steel Ltd, Quaim Steel Ltd, Metro Steel Mills, Kamaka Co. Ltd, Steelmasters Ltd, Lake Steel Ltd, Hong Yu Steel Ltd, Fujian Co. Ltd.

Prof. Kahyarara amewaeleza wazalishaji hao kuwa wao ndio wenye jukumu la kuhakikisha wanafanya kazi kwa juhudi, kwa kuongeza uzalishaji zaidi na  changamoto walizoieleza Wizara yake imezipokea na zitafanyiwa kazi zote  na kuzimaliza kwani lengo la Serikali ni kuweka mazingira bora kwa wawekezaji nchini ili kuchochea uchumi na Ajira kwa Watanzania.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here