(Habari na Picha na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Rukwa)
Na: OMM Rukwa.
Watumishi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Rukwa wametakiwa kutumia uwepo wa baraza la wafanyakazi kuibua mawazo mapya yatakayochochea upatikanaji wa tija sehemu za kazi.
Wito huo umetolewa leo (15.02.2022) na Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Joseph Mkirikiti wakati alipohutubia kikao cha Baraza la Wafanyakazi wa Ofisi yake kilichofanyika mjini Sumbawanga.
“Kikao cha Baraza la Wafanyakazi kipo kwa mujibu wa sheria hivyo kitumieni kujadili mipango na mikakati ya kufanya malengo ya serikali yaweze kutimia na kuwezesha wananchi kupata huduma bora “ alisema Mkirikiti.
Mkuu huyo wa Mkoa aliongeza kusema watumishi wa umma wanapaswa kufanya kazi katika hali ya uhuru na kutoa mawazo yao kuboresha utekelezaji wa shughuli za serikali ikiwemo usimamizi endelevu wa miradi ya maendeleo katika halmashauri.
Mkirikiti aliwaasa pia watumishi hao kuwa na mahusiano mazuri kazini wakitanguliza uzalendo na kutambua mipango ya serikali ya awamu ya sita na namna ya kuitekeleza.
“Sasa lazima muwe makini kujua mpango wa bajeti ya mkoa na wilaya zake na namna utekelezaji utakavyofanyika katika mwaka ujao wa fedha 2022/2023. Tambue miradi kipaumbele katika maeneo yenu na mkawafahamishe watumishi wenzenu “alisisitiza Mkiikiti.
Kwa upande wake Katibu Tawala Mkoa wa Rukwa Denis Bandisa alisema lengo la kikao hicho cha Baraza la Wafanyakazi ni kuwajulisha na kuwapitisha watumishi wajue mpango wa bajeti ijayo 2022/23 na itakavyotekelezwa ikiwemo maslahi ya watumishi na vitendea kazi.
Akizungumza kwa niaba wa watumishi Afisa Utumishi Oresta Haule alisema watumishi wako tayari kuendelea kufanya kazi kwa ubunifu na moyo wa kujituma ili kufanya mkoa wa Rukwa upige hatua za kimaendeleo zaidi.
Ofisi ya Mkuu wa Rukwa ina wilaya tatu za Sumbawanga, Nkasi na Kalambo ambapo mahitaji ya watumishi ni 245 ambapo waliopo ni 141 na upungufu ni watumishi 104.
Mwisho.