Home LOCAL KISWAHILI SASA NI FURSA

KISWAHILI SASA NI FURSA


Na: Mwandishi wetu – MAELEZO,  07/02/2022.

Watanzania watakiwa kuchangamkia fursa ya lugha ya Kiswahili ambacho kwa sasa kinakuwa kwa kasi, kikiwa na zaidi ya watumiaji milioni 150 Duniani.

Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Utamaduni Sanaa na Michezo, Saidi Yakubu amesema hayo leo, Februari 7, 2022 Jijini Dar es Salaam alipotembelea ofisi za Baraza la Kiswahili la Taifa (BAKITA).

“Kiswahili kinaendelea kukua siku hadi siku, hivi sasa kuna wazungumzaji zaidi ya milioni 150 duniani na kinatumika katika taasisi nyingi. Miaka ya hivi karibuni imepitishwa kuwa lugha ya kazi na lugha rasmi katika nchi za Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC), alisema Yakubu.

Ameendelea kusema kuwa, katika mkutano wa 35 wa Wakuu wa Nchi  na Serikali wa Umoja wa Afrika (AU) uliofanyika Addis Ababa, Ethiopia kuanzia Februari 5 hadi 6, 2022, ambapo Makamu wa Rais, Dkt. Philip Mpango alimuwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan katika mkutano huo umepitisha Kiswahili kuwa moja ya lugha za kazi katika Jumuiya hiyo.

Amesema kuwa, fursa ya lugha ya Kiswahili ni nyingi ambapo Tanzania ina mkakati wa kufanya Kiswahili kuwa moja ya bidhaa ambazo zitatolewa nje na kuuzwa sawa na bidhaa nyingine zinavyouzwa kama vile pamba na madini. 

Aidha Yakubu ameitaka BAKITA kuwa na ubunifu katika utendaji wake na kujiendesha kibiashara na kutosubiri wateja bali watafute masoko ndani na nje ya nchi ambapo kuna zaidi ya vyuo 100 duniani vinavyofundisha kwa lugha ya Kiswahili na  redio za idhaa ya Kiswahili 34.

Vilevile amesema kuwa, Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa alitoa maelekezo kwa BAKITA kuwa na madarasa ya Kiswahili katika Balozi za Tanzania, hivyo ni jukumu la BAKITA kusimamia utekelezaji wa shughuli hizo ili kuwawezesha Watanzania kupata fursa za ajira kupitia Kiswahili Duniani.  

Naibu Katibu Mkuu pia ametoa wito kwa Watanzania kujitokesa hasa wataalam wa lugha ya Kiswahili, wajiandikishe BAKITA ili waweza kutambulika, kwani  fursa za  ajira za Kiswahili Duniani zinaendelea kukua siku hadi siku. 

Ziara hiyo ya Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Utamaduni Sanaa na Michezo, Saidi Yakubu BAKITA ni mwendelezo wa utaratibu wa viongozi kupitia Taasisi zote zilizo chini ya Wizara hiyo, ikiwa ni katika kuona utendeji kazi wa taasisi husika pamoja na kutoa maelekezo ili kuhakikisha majukumu ya Taasisi hizo yanatekelezwa kwa ufanisi.

 MWISHO.

Previous articleYASEMAVYO MAGAZETI ASUBUHI YA LEO J.TATU FEBRUARI 7-2022
Next articleASKOFU MAPUNDA: ‘WATAWA TUHANGAIKE NA MALEZI YA WATOTO, TUZUNGUMZE NA FAMILIA KUTOKOMEZA UHALIFU
Hughes Dugilo is a Writer, News Producer, Video-Photographer Journalist, and Video Editor experienced for 20 years now performing in News, Documentary, Advertisements and Television Programs. Aside from all above he own and operate his Blog known as Green Waves Media TZ since 2018.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here