Home BUSINESS KAMPUNI YA UCHIMBAJI MADINI YA SHANTA YATOA SH.200 MILIONI KUSAIDIA MIRADI YA...

KAMPUNI YA UCHIMBAJI MADINI YA SHANTA YATOA SH.200 MILIONI KUSAIDIA MIRADI YA MAENDELEO IKUNGI

Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Ikungi Mika Likapakapa  (kulia) na Mkuu wa wilaya hiyo Jerry Muro (wa pili kutoka kulia) wakimtwika ndoo ya maji mkazi wa  Kijiji cha Banda Tatu katika mradi wa maji uliotekelezwa na Kampuni ya Shanta mradi ambao utahudumia vijiji vya Mlumbi na Mang’onyi katika hafla ya kukabidhi miradi yote iliyotekelezwa na kampuni hiyo wilayani humo iliyofanyika jana. Wa kwanza kutoka kushoto ni Kaimu Meneja Mkuu wa kampuni hiyo Mhandisi Kundaeli Ntiro na wa tatu ni Meneja Uhusiano wa kampuni hiyo Elisante Kanuya.
Mkuu wa Wilaya ya Ikungi akikagua ujenzi wa vyoo vya Shule ya Msingi Mlumbi kabla ya kukabidhiwa Serikalini.
Meneja Uhusiano wa Kampuni hiyo Elisante Kanuya akizungumzia ukamirishaji wa ukarabati wa Zahanai ya Mang’onyi.
Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Ikungi, Mika Likapakapa (wa pili kushoto) akizungumza wakati wakipokea madarasa yaliyo jengwa na kampuni hiyo katika Shule ya Sekondari ya Mwau. Kulia ni  Kaimu Meneja Mkuu wa kampuni hiyo Mhandisi Kundaeli.
Ukaguzi wa Zahanati ya Mang.onyi ukiendelea.
Safari ya kwenda kukagua kichomea taka za zahanati hiyo ikiendelea.
Ukaguzi wakichomea taka wa zahanati hiyo ukiendelea (kushoto ni kichomea taka)
Ukaguzi wa madarasa mawili na ofisi Shule Shikizi Namba 7 ukifanyika. 
Ukaguzi wa ujenzi wa vyoo Shule ya Msingi Mlumbi ukifanyika.
Ukaguzi wa mradi wa maji  Kijiji cha Banda Tau ukifanyika.
Wanafunzi wa Shule Shikizi ya Namba 7 wakiwa mbele ya madarasa yaliyojengwa na kampuni hiyo.

Na Dotto Mwaibale, Singida

KAMPUNI ya Uchimbaji Madini ya Shanta iliopo Wilaya ya Ikungi mkoani Singida imetoa zaidi ya Sh.200 Milioni kwa ajili ya kusaidia miradi mbalimbali ya maendeleo wilayani humo.

Hayo yalifahamika jana katika Sherehe za maadhimisho ya miaka 45 tangu kuzaliwa kwa Chama Cha Mapinduzi (CCM) yaliyofanyika Kata ya Mang’onyi wilayani Ikungi mkoani Singida jana wakati wa kukabidhi miradi hiyo kwa Serikali.

Akizungumza wakati akitoa taarifa hiyo Kaimu Meneja Mkuu wa kampuni hiyo Mhandisi Kundaeli Ntiro alisema fedha hizo zilitumika kusaidia miradi hiyo kwa mwaka 2020/2021.

Aliitaja miradi waliyoikabidhi kuwa ni ya elimu ambapo wamejenga madarasa mawili ya Shule ya Msingi Mlumbi, ujenzi wa madarasa mawili mawili na ofisi Shule Shikizi namba 7, kuweka sakafu madarasa mawili ya zamani Shule Shikizi namba 7 na kuweka sakafu darasa moja la zamani na ofisi Shule ya Msingi Mlumbi.

Alitaja mradi mwingine kuwa ni ujenzi wa vyoo kwa shule zote mbili ambao unatarajiwa kukamilika ndani ya mwezi Februari na kuwa ujenzi huo umezingatia umuhimu wa makundi yote kulingana na mwongozo, michoro na kuelekezwa kutoka kwa Mhandisi wa wilaya hiyo.

Akizungumzia miradi ya Afya alisema wamefanya ukarabati wa Zahanati ya Kata ya Mang’onyi kwa kujenga uzio kwenye tanuru la kuchomea taka, kuweka miundombini ya TEHAMA kwenye jengo la Zahanati hiyo ili kuunganishwa kwenye mfumo wa afya wa Serikali sambamba na kutoa vifaa kompyuta tatu na printa moja.

Alitaja kazi nyingine walioifanya kukarabati wa chumba cha maabara, kujenga ukuta wa kuzuia maji ya mvua na kumwaga zege sehemu ya kuingilia zahanati na ujenzi wa mabenchi manne ya zege ya kupumzikia wagonjwa ambao ujenzi wake unaendelea.

Katika mradi wa maji alisema kampuni imetandaza mtandao wa mabomba wenye urefu wa kilometa 4.6 na kujenga vituo vitatu vya kuchotea maji kwa ajili ya wananchi wa vijiji vya Mang’onyi na Mlumbi wanaoishi kandokando ya bomba kuu linalopeleka maji mgodini. 

Kwa upande wa barabara alisema kampuni imesaidia kutengeneza barabara kwenda Mlumbi shuleni kutoka Kisima Namba 08 yenye urefu wa kilometa tatu na barabara ya kwenda Mwau Sekondari kutokea barabara kubwa yenye urefu wa kilometa moja.

Alisema kazi zote za ujenzi zilifanyika kwa kutumia mafundi na wasaidizi kutoka katika maeneo yanayozunguka miradi iliyoorodheshwa na kuwa jumla ya kiasi cha fedha ambayo imetumika kwenye huduma za jamii na mahusiano ya serikali kwa mwaka 2021 ni Sh.235,495,327.00.

Akipokea miradi hiyo Mkuu wa Wilaya ya Ikungi Jerry Muro aliishukuru Kampuni hiyo kwa kuunga mkono jitihada za Serikali za kuwaletea maendeleo wananchi wa wilaya hiyo na kuagiza itunzwe na kuwa serikali itaendelea kushirikiana na wawekezaji katika wilaya hiyo.

Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) katika wilaya hiyo Mika Likapakapa aliwaambia wananchi kuondoa dhana ya kuamini maneno ya watu wasio penda maendeleo kuwa wawekezaji hao hawana tija yoyote katika wilaya hiyo na kuwa faida ya kuwepo kwao wilayani humo wanaiona na wamekuwa wakifuata sheria zote za uchimbaji na kulipa kodi.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here