Jaji mfawidhi wa mahakama kuu kanda ya Arusha Moses Mzuna akiongea katika kilele cha maadhimisho ya siku ya sheria nchini yaliyofanyika mkoani Arusha.
NA: NAMNYAK KIVUYO, ARUSHA.
Jaji mfawidhi wa mahakama kuu kanda ya Arusha Jaji Moses Mzuna amekemea vitendo vinavyoendelea kutokea katika mkoa wa Arusha vinavyovunja amani na usalama wa nchi mojawapo ikiwa ni kukithiri kwa mauaji miongoni mwa wanafamilia au jamii ambayo badhii hutokana na migogoro ya ardhi.
Jaji Mzuna aliyasema hayo katika kilele cha maadhimisho ya siku ya sheria nchini yaliyofanyika katika viwanja vya kituo jumuishi cha utoaji haki, mahakama kuu Arusha ambapo alisema kuwa Kuna mambo yanayotokea mkoa wa Arusha ambayo yeye kama msimamizi hana budi kuyazungumzia kwani ni mambo mtambuka yanayogusa jamii hasa hayo ya mauaji.
Alisema kuwa mambo mengine ni pamoja na tabia zilizoanza za kubomoa majengo au nyumba bila amri halali huku mashauri yakiwa mahakamani na wakati mwingine kutumia madalali wasiokuwa wamesajiliwa.
Alieleza kuwa pia jambo lingine ambalo linagusa jamii ni wanafamilia kutofungua maombi ya asimamizi ya mirathi mapema mahakamani na hivyo kuchochea migogoro ya familia na hatimaye kupelekea mashauri ya msingi kuchelewa.
“Lakini pia jamii kutotumia njia ya usuluishi kama mbinu mbadala hali inayope wanafamilia kufikishana mahakamani hata kwa migogoro midogo midogo,”Alisema Jaji Mzuna.
Aidha akizungumzia kilele cha maadhimisho ya siku ya sheria yaliyobeba kauli mbiu isemayo “ zama za mapinduzi ya nne ya viwanda, safari ya maboresho kuelekea mahakama ya mtandao” Jaji Mzuna alisema kuwa serikali imekuwa ikisisitiza matumizi ya mashine ya kiteknolojia ili kuongeza ufanisi wa kazi na kuweza kukuza uchumi wa nchi.
“Moja ya hatua kubwa katika utekelezaji wa maboresho ambayo mahakama imekuwa ikifanya ni matumizi ya TEHAMA katika kuharakisha na kurahisisha upatikanaji wa huduma za kimahakama na kusisogeza karibu na hata kiganjani mwa mwananchi,” Alisema Jaji Mzuna.
Kwa upande wake mkuu wa mkoa wa Arusha John Mongela alisema kuwa mabadiliko kwenye mahakama yamewasaidia katika mambo mbalimbali hasa wao kama viongozi wanaofanya shughuli zinazoingiliana na wananchi ambapo imejihisisha na utoaji wa msaada wa kisheria ambayo imesaidia kuhakikisha kunakuwa na usalama na utulivu.
Naye mwenyekiti wa chama cha mawakili kanda ya Arusha Njooka George alisema kuwa pamoja na maboresho makubwa yenye manufaa yaliyofanya na mahakama kwa sasa wanakabiliwa na changamoto ya ukosefu wa mtandao katika jengo la kituo jumuishi la utoaji haki, kupotea kwa nyaraka mtandaoni pamoja na kuchelewa kupata control namba wakati wa usajili wa kesi mpya.