Mkuu wa Wilaya ya Ruangwa Hassan Ngoma akizngumza wakati wa uzinduzi rasmi wa Mafunzo kwa watoa huduma katika mnyororo wa utalii kupitia Mradi wa UVIKO -19 Awamu ya kwanza Mkoani Lindi.
Afisa Mtendaji Mkuu Chuo cha Taifa cha Utalii Dkt. Shogo Mlozi akitoa hotuba ya utangulizi wakati wa uzinduzi wa mafunzo hayo yanayofanyika katika Wilaya ya Ruangwa Mkoani Lindi.
Chuo cha Taifa cha Utalii kimezindua rasmi mafunzo kwa watoa huduma katika Mnyororo wa Utalii kupitia Mradi wa UVIKO 19 awamu ya kwanza kwa kuwakutanisha wadau mbalimbali katika Mkoa wa Lindi.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa Mradi huo kwa niaba ya mgeni rasmi Mkuu wa Wilaya ya Ruangwa Hassan Ngoma ambaye amemuwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Lindi amesema kuwa Serikali imeendelea kuchukua tahadhari katika mapambano dhidi ya janga la UVIKO -19 kwa kuweka mikakati madhubuti ya kuhakikisha tahadhari zote muhimu zinachkuliwa.
Amesema kuwa katika kipindi cha hivi karibuni kumeshuhudiwa jitihada kubwa iliyofikiwa na Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuchukua hatua kwa vitendo kwa kupeleka fedha za Uviko -19 katika maeneo mbalimbali zikiwemo taasisi za Serikali ambapo moja ya maeneo hayo ni Sekta ya Utalii na kwamba mafunzo hayo yatawawezesha wadau wa Sekta hiyo kupata uelewa wa namna bora ya kujikinga na ugonjwa huo wanapotoa huduma zao kwa wageni.
Aidha ameongeza kuwa kumekuwepo na shughuli nyingi zenye muingiliano wa wageni katika wilaya ya Ruangwa kutokana na Wilaya hiyo kuwa na shughuli nyingi za kiuchumi ikiwemo ujenzi wa miundombinu na madini hivyo amepongeza Chuo cha Taifa cha Utalii kuendesha mafunzo hayo katika Mkoa wa Lindi na kuweka kituo cha Mafunzo Wilayani Ruangwa.
“Katika Mkoa wa lindi hususani hapa Ruangwa kumekuwepo na shughuli nyingi za kiuchumi ukizingatia hii ni Wilaya inayoendelea kutokana na shughuli zake zinazofanywa hapa ikiwemo Utalii na uchimbaji Madini ambazo zimekuwa ikiwaleta watu wengi hapa wakiwemo wageni kutoka katika mataifa ya nje” Amesema Ngoma.
Kwa upande wake Afisa Mtendaji Mkuu wa Chuo cha Taifa cha Utalii Dkt. Shogo Mlozi amesema kuwa Mafunzo hayo yamegawanyika katika sehemu kuu mbili. Sehemu ya kwanza ikiwa ni mafunzo kwa watoa huduma kwenye Sekta ya Utalii na Ukarimu katika mikoa 8 ya Tanzania Bara ikiwemo Mikoa ya Mtwara, Lindi, Ruvuma, Njombe, Mbeya, Iringa, Mwanza na Mara, ambapo zaidi ya washiriki 150 watapatiwa mafunzo hayo kwa kila Mkoa kulingana na ukubwa wa Mkoa na shghuli za Utalii.
“Sehemu ya pili ya mafunzo haya, itahusisha utoaji wa mafunzo ya upimaji na upangaji ubora wa madaraja kwa watoa huduma za malazi na chakula kwa jumla ya washiriki 47. Ambao kati ya hao washiriki 14 wanatoka kwenye Sekta Binafsi na wengine watatoka katika mashirika na taasisi zilizo chini ya Wizara ya Maliasili na Utalii” amesema Dkt. Mlozi.
Aidha amewashukuru washiriki wote kwa kukubali wito wa kuhudhuria mafunzo hayo kwani yatawajengea uwezo wa kuinua ubora wa utoaji Huduma na ushindani katika Sekta ya Utalii.
Mafunzo hayo ya siku tano yamezinduliwa rasmi leo Februari 7, 2022 katika Wilaya ya Ruangwa Mkoani Lindi na yanatarajiwa kufikia tamati Febrari 11 Mwaka huu.