Katibu Mkuu wa Wizara ya Uwekezaji Biashara na Viwanda Mhe. Prof. Godius Kahyarara ameiagiza Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA) kuandaa mkakati utakaowezesha soko la bidhaa kuwa na bei halali.
Prof. Kahyarara ametoa agizo hilo Ijumaa ya tarehe 18 Februari, 2022 kwa Menejimenti ya BRELA alipofanya ziara ya kikazi katika ofisi hizo Jijini Dar es Salaam.
Ameeleza kuwa, mkakati huo, kupitia utoaji wa leseni za biashara utaiwezesha BRELA kudhibiti na kujiridhisha na mnyororo wa usambazaji wa bidhaa, ufuatiliaji wa wafanyabiashara waliopo kwenye masoko na kuwaweka kwenye mfumo rasmi.
Prof. Kahyarara amesema, Wizara kupitia taasisi zake zinapaswa kuwa na udhibiti wa masoko wenye lengo la kuleta usawa kuanzia kwa mzalishaji msambazaji hadi kwa mlaji.
“Kama Serikali tunapaswa kuhakikisha kuwa kunakuwa na biashara ya haki kwa anayezalisha, anayeuza na mlaji na kama Wizara ya Uwekezaji, Biashara na Viwanda bado suala la bei za bidhaa sokoni, halijafanyiwa kazi kikamilifu,” alifafanua Prof. Kahyarara.
Aliongeza kuwa, imefika wakati sasa taasisi zinatakiwa kubadili taratibu za utendaji kazi, kwani majukumu na matarajio yaliyopo ni makubwa, hivyo tunatakiwa kuondokana na uchumi wa kivuli na kwenda kwenye uchumi wa nuru (from shadow to light economy).
Prof. Kahyarara amesisitiza kuwa licha ya kuwa na wafanyabiashara wengi, bado Serikali haijaweza kuwadhibiti kikamilifu kwa kuhakikisha kuwa wanafanyabiasha bila ya kuvunja sheria na taratibu zilizopo.
Aliongeza kuwa, bila ya kuwa na udhibiti kwenye masoko wananchi wa kipato cha chini, wataendelea kuumia kwani utafiti mdogo uliofanywa na Wizara umebaini kuwa asilimia kubwa ya wanaopandisha bei za bidhaa ni wale wanaopeleka sokoni.
“Tunapaswa kutumia kila silaha ili watanzania wasiumizwe kwenye bei, hivyo BRELA muanze kufikiri njia gani itumike ili hatimaye wauzaji wazingatie bei halali ya soko,” alisisitiza Prof. Kihyarara.
Kwa upande wake Afisa Mtendaji Mkuu wa BRELA Bw. Godfrey Nyaisa amemhakikishia Prof. Kahyarara kuwa, BRELA itatekeleza agizo hilo kwa ukamilifu kwa kuzingatia majukumu pamoja na malengo ya Taasisi kwa kuweka mifumo rasmi ambayo hatimaye itawasaidia wananchi.
IMETOLEWA NA KITENGO CHA HABARI NA MAWASILIANO -BRELA