Happy Mlwale, Afisa Sheria wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT) akiwasilisha mada kuhusu Dawati la Malalmiko kwenye semina ya wahariri na waandishi wa habari waandamizi kutoka vyombo mbalimbali vya Habari nchini inafofanyika kwenye tawi la benki hiyo jijini Mbeya.
Picha mbalimbali zikiowaonesha waandishi wa habari wakimsikiliza Happy Mlwale, Afisa Sheria wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT) kwenye semina ya wahariri na waandishi wa habari waandamizi kutoka vyombo mbalimbali vya Habari nchini inafofanyika kwenye tawi la benki hiyo jijini Mbeya.
BOT ilianzisha DAWATI la kutatua malalamiko ya wateja wa taasisi za fedha, 1 Aprili 2015 katika jitihada za kuondoa changamoto zilizokuwa zikijitokeza kabla ya kuanzishwa kwake kutokana na kutokuwa na mfumo rasmi wa kutatua malalamiko hayo kwenye sekta ya taasisi za fedha, isipokuwa Mahakama na vyombo vingine pekee.
Taasisi nyingi zilikuwa hazitatui malalalamiko na kusababisha baadhi ya wananchi kukosa imani kwenye sekta ya taasisi za fedha, hasa sekta ya mabenki, kutokana na changamoto hizo.
Hayo yameelezwa na Happy Mlwale, Afisa Sheria wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT) kwenye semina ya wahariri na waandishi wa habari waandamizi kutoka vyombo mbalimbali vya Habari nchini inafofanyika kwenye tawi la benki hiyo jijini Mbeya.
Happy Mlwale amesema wakati Benki Kuu haikuwa na dawati hilo, taasisi nyingine za usimamizi na udhibiti zilishakuwa na mifumo ya utatuzi wa malalamiko kama vile TIRA, TCRA, EWURA na SUMATRA, huku nchi nyingine nazo zikiwa na mifumo hiyo, kama vile Ghana, Nigeria, Namibia na Afrika Kusini.
“Benki ya Dunia ilifanya upembuzi yakinifu “Diagnostic Review 2013” na kushauri mfumo huu kuanzishwa hapa nchini ili kupunguza au kuondoa changamoto hizo ambapo baada ya kuanzishwa rasmi DAWATI, wataalamu walikwenda Afrika Kusini kujifunza na liliishirikisha Jumuiya ya Mabenki Tanzania (TBA) na kuendesha warsha kwa mabenki tarehe 9 Machi 2015,” amesema Happy Mlwale.
Ameongeza kuwa madhumuni na mamlaka ya DAWATI ni kutatua malalamiko ya wateja wa taasisi za kifedha kwa haraka, bila gharama, bila upendeleo, kwa uhuru kamili na kwa uwazi ili kujenga imani kwa wananchi kwenye sekta hii, iliyo muhimu kwa uchumi ili waendelee kuweka fedha zao benki.
“Kifungu cha 7(2) cha Sheria ya (BoT) 2006 kinaitaka (BoT) kuhakikisha kuna mfumo imara wa kifedha nchini ambapo Chini ya Kifungu 71 cha BAFIA 2006 (Sheria ya Mabenki na Taasisi za Fedha), Gavana alitoa “Mwongozo wa Utatuzi wa Malalamiko ya Wateja wa Huduma za Kibenki 2015,” amesema Happy Mlwale.
Amefafanua kwamba DAWATI lilipoanzishwa lilikuwa likiongozwa na Mwongozo wa Utatuzi wa Malalamiko ya Wateja wa Huduma za Kibenki, 2015 ambao, pamoja na mambo mengine, katika Kifungu cha 14: DAWATI liliwekewa ukomo wa kupokea malalamiko.
Aidha, ameongeza kuwa DAWATI kwa sasa lina uwezo wa kupokea malalamiko yote yatokanayo na taasisi za watoa huduma za kifedha nchini, kwa mfano. Maduka ya Kubadilisha Fedha za Kigeni, “Taasisi za Taarifa za Mikopo (Credit Reference Bureaux)”, mabenki, mwananchi mmoja mmoja, makampuni, SACCOS na VICOBA.
Malalamiko yanatatuliwa kwa mujibu wa Kanuni za Kumlinda Mlaji wa Huduma za Fedha, 2019 na Mwongozo wa Utatuzi wa Malalamiko ya Wateja wa Huduma za Kibenki, 2015 ambazo zinaeleza namna ya kupokea na kuyatatua malalamiko hayo.
Amesema DAWATI linatatua changamoto hizo kwa kufuata misingi ya kimataifa – Bila gharama, Bila upendeleo, Kwa uhuru kamili na kwa uwazi ambapo mlalamikaji anapaswa kwanza kupeleka malalamiko yake kwenye benki yake.
DAWATI litapokea malalamiko litayachunguza kuona kama yanakidhi vigezo (Checklist) ili yaweze kufanyiwa kazi kwa ajili ya utatuzi, Kama malalamiko hayo yamekidhi vigezo, ndani ya siku 4 DAWATI litamtumia mlalamikaji barua ya kuyapokea na vilevile DAWATI litaitumia benki inayolalamikiwa, Notisi kuitaka ijibu malalamiko hayo ndani ya siku10.
Baada ya kupokea majibu, DAWATI litakusanya ushahidi wote kisha litaandika hukumu na DAWATI linaweza kuziita pande zote 2 wakati wa kutoa hukumu hiyo, Pia hukumu ikitolewa dhidi ya benki basi benki hiyo inatekeleza kile kilichoelekezwa na DAWATI. Upande wowote usiporidhika unaweza kuomba Mapitio ya hukumu.
Happy Mlwale amesema kumekuwa na mafanikio makubwa kutokana na kuanzishwa kwa DAWATI hilo kwani malalamiko mengi yametatuliwa katika mabenki na wananchi wamepata chombo sahihi cha kuwasilisha malalamiko yao hivyo kuonesha kuwa na imani nasekta ya benki.
Ameongeza kuwa mafanikio mengine yaliyopatikana ni pamoja na nchi nyingine kuja kujifunza nchini mwetu kama vile Ethiopia na Uganda ambapo pia malalamiko hayo yametoa mchango katika uanzishwaji wa Sheria
mpya.
Baada ya ujio wa sheria mpya ya mwaka 2019, imetanua wigo ambapo taasisi zote za kifedha na watoa huduma za fedha wanaangukia kwenye mamlaka ya DAWATI.