Home LOCAL WAZIRI UMMY ATAJA MKAKATI WA KUPUNGUZA MAAMBUKIZI YA VVU KWA WATOTO WACHANGA

WAZIRI UMMY ATAJA MKAKATI WA KUPUNGUZA MAAMBUKIZI YA VVU KWA WATOTO WACHANGA


Na.WA-Dar es Salaam.

Serikali kupitia Wizara ya Afya inajipanga kupunguza idadi ya Watoto wanaozaliwa na maambukizi ya VVU kutoka kwa mama nchini.
Hayo yamesemwa leo na Waziri wa Afya Mhe.Ummy Mwalimu wakati wa Uzinduzi wa Mpango Mkakati wa pili wa miaka mitano wa tafiti na mafunzo Katika masuala ya afya ya Jamii na lishe uliofanyika jijini Dar es Salaam.
Waziri Ummy amesema kuwa Serikali inajipanga kuja na mkakati wa kuhamasisha na kuwahimiza akina mama wajawazito ambao bado hawajajua hali zao kujitokeza kupima ili kuwalinda Watoto watakaozaliwa wasiwe na maambukizi ya VVU.
“Suala la mtoto kuzaliwa na maambukizi ya Virusi vya UKIMWI halikubaliki, tutaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali Katika kufuatilia watu ambayo hawajaweza kujua Hali zao za maambukizi wapatao 200,000 kwa kuwahamasisha ili kufikia malengo ya milenia ifikapo mwaka 2030”. Amesema Waziri Ummy.
Aidha, amesema kwa takwimu za mwaka 2021, Tanzania imefanikiwa ambapo asilimia 88 ya watanzania wenye maambukizi wanafahamu hali zao huku asilimia 98 wakiwa wanatumia dawa na asilimia 92 wamefubaza makali ya virusi hivyo kwa asilimia kubwa.
“Kwenye suala la matumizi ya dawa tuko vizuri ambapo 98% ya watu wenye maambukizi ya VVU wanatumia dawa ambapo kati yao 92% virusi vimedumazwa kwahiyo unaweza kuwa na virusi vya UKIMWI lakini usiwe na changamoto za maradhi”. Amesema Waziri Ummy.
Uzinduzi huo ulihudhuriwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya Prof. Abel Makubi, viongozi mbalimbali na wadau wa maendeleo wa ndani na nje ya nchi.
MWISHO

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here