Home LOCAL WAZIRI JAFO AZINDUA KAMPENI YA UPANDAJI MITI KWA WANAFUNZI WA SHULE NA...

WAZIRI JAFO AZINDUA KAMPENI YA UPANDAJI MITI KWA WANAFUNZI WA SHULE NA VYUO


Na: Robert Hokororo.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira Mhe. Selemani Jafo amezindua Kampeni ya upandaji wa miti kwa wanafunzi wa shule na vyuo jijini Dodoma leo Januari 20, 2022 inayofahamika kama ‘Soma na Mti’.

Akizindua kampeni hiyo katika viwanja vya Shule ya Sekondari Dodoma, Dkt. Jafo alisema lengo la kampeni hiyo ni kuwafanya wanafunzi waone zoezi la upandaji miti ni sehemu ya maisha ili kukabiliana na changamoto za mabadiliko ya tabianchi.

Alisema hapa nchini kuna takriban wanafunzi milioni 14.1 ambao kila mmoja akipanda mti wake itasaidia katika kukabiliana na changamoto hizo za kimazingira ikiwemo ukame na uhaba wa maji.

“Ndugu zangu katika kampeni hii tunataka kila mwanafunzi ajivunie mti wake alioupanda na tutaona fahari kubwa kuwa wanafunzi weyu wanajali mazingira na tunajali nchi yetu,” alisema.

“Leo hii tunashuhudia ukame, mvua hainyeshi na tulitegemea ingenyesha tangu mwezi wa tisa lakini hadi leo maeneo mengi hakuna mvua, hayo yote ni mabadiliko ya tabianchi kutokana na kukosekana kwa miti,” aliongeza Waziri Jafo.

Pia, Waziri Jafo alikizungumza na wanafunzi na wananchi mbalimbali baada ya kupokea maandamano yaliyoanzia viwanja vya Nyerere Square Dodoma aliwashukuru na kuwapongeza wadau mbalimbali kwa kushiriki kikamilifu katika kampeni za upandaji miti.

Kwa upande wake Naibu Waziri Ofisi ya Rais – TAMISEMI, Mhe. David Silinde aliipongeza Ofisi ya Makamu wa Rais kwa kuzindua kampeni hiyo na kuahidi kuitekeleza.

Silinde aliagiza shule zote nchini kuhakikisha wanaitekeleza kwa vitendo pamoja na kuanzisha au kufufua klabu za mazingira ngazi ya msingi na sekondari ambayo alisema ni sehemu ya masomo.

Kwa upande wake Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais (Mazingira), Bw. Edward Nyamanga alisema zoezi kampeni hii ina umuhimu kwa sababu inalenga kuwafundisha wanafunzi kupanda miti.

Alisema linawafundisha vijana kupambana na athari za mabadiliko ya tabanchi na uharibifu wa mazingira kwa ujumla kwa vitendo.

Nae Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Elimu ya Juu, Prof. Carolyn Nombo alisema wanaunga mkono kampeni hii na kuwa inawajega wanafunzi kupenda mazingira.

Alisema kuwa wizara hiyo itasimamia ipasavyo kwa kuwa inawafundisha kwa vitendo kuhusu lmasomo ya Kilimo, Biolojia na Mazingira.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here