Home LOCAL WAZIRI BASHUNGWA AAGIZA VITUO VYA HUDUMA KWA MTEJA KILA MKOA

WAZIRI BASHUNGWA AAGIZA VITUO VYA HUDUMA KWA MTEJA KILA MKOA




 Na: Angela Msimbira, OR- TAMISEMI.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Mhe. Innocent Bashungwa amemuagiza Katibu Mkuu Ofisi ya Rais TAMISEMI Prof. Riziki Shemdoe kuweka mikakati ya uanzishwaji wa Kituo cha kutolea huduma kwa mteja kwa kila Mkoa ili kurahisisha utoaji wa Huduma bora kwa wananchi.

Ametoa agizo hilo leo wakati alipotembelea Kituo cha Huduma kwa Mteja cha Ofisi ya Rais –TAMISEMI kwa lengo la kuangalia  maelekezo aliyoyatoa  kuhusu maboresho ya kuhakikisha huduma bora inatolewa kwa wananchi.

“Nimeridhishwa na utendaji kazi wa watumishi wa Kituo cha Kutolea Huduma kwa Wateja cha Ofisi ya Rais –TAMISEMI lakini ingekuwa vyema vituo hivyo  vingekuwa vinapatikana katika ngazi ya Mikoa ili kuwarahisishia wananchi  kupata huduma kwa haraka tofauti na sasa mpaka wapige simu Wizarani kutatuliwa kero zao, hivyo tunawajibu wa kuweka mikakati ya kushusha huduma hizo mikoani kuwapunguzia adha wananchi kufuata huduma ngazi ya Wizara” Amesisitiza Waziri Bashungwa 

Amemuagiza katibu Mkuu huyo kuhakikisha anatafuta rasilimali fedha na vifaa ili kuhakikisha ule makakati wa  kuweka nguvu na kuimarisha Sekretarieti za Mikoa katika utoaji wa huduma bora kwa wananchi  kuanzia ngazi ya kijiji, kata, Tarafa , Wilaya na Mkoa unafanikiwa. 

Ameagiza kuwa  Wakuu wa Mikoa na Makatibu Tawala wa Mikoa ndio watakaokuwa wasimamizi wakuu wa vituo hivyo vya kutolea Huduma kwa wateja lengo likiwa ni kuhakikisha huduma bora inapelekwa kwa wananchi kwenye maeneo yao na kuwapunguzia  adha ya kutembea umbali mrefu kufuata huduma Wiazarani. 

“Jambo hili limeanza vizuri ngazi ya Wizara, hivyo tuimarishe kwenye Mikoa ili kuweza kuwasaidia wananchi, hivyo nawaagiza kuhakikisha tunaweka mikakati ya kila Mkoa kuwa na Kituo cha Huduma kwa wateja ili wananchi wanapohitaji huduma  kutoka Mikoani wanakuwa na namba ambazo wanaweza kupiga badala ya  kutoka Vijijini  kuja kupata huduma Wizarani.” Amesisitiza Waziri Bashungwa 

Naye Msimamizi wa Kituo cha Huduma kwa Wateja  Bi. Antelma Mtemahanji  amesema kuwa lengo la kuanzishwa kwa kituo hicho ni kuwasaidia wananchi waliokuwa wakitembea umbali mrefu  kutoka vijijini hadi kufika Ofisi ya Rais –TAMISEMI  kufuata huduma mbalimbali za kiofisi  na toka kituo kimeanzishwa mwaka 2020  hadi sasa  simu 125, 381 zilizopokelewa na kufanyiwa kazi  katika kituo hicho.

Aidha , amesema  kabla ya kuanzishwa kwa kituo hicho Ofisi ya Rais –TAMISEMI ilikuwa ikipokea wateja 100 hadi 120  ambao walikuwa wakifika ofisini kufuata huduma, lakini hali hiyo kwa sasa imepungua na kupunguza mlundikano wa wananchi kufuata huduma Wizarani

Previous articleYASEMAVYO MAGAZETI ASUBUHI YA LEO J.NNE JANUARI 18-2022
Next articleRAIS SAMIA AFANYA UTEUZI WA VIONGOZI MBALIMBALI
Hughes Dugilo is a Writer, News Producer, Video-Photographer Journalist, and Video Editor experienced for 20 years now performing in News, Documentary, Advertisements and Television Programs. Aside from all above he own and operate his Blog known as Green Waves Media TZ since 2018.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here