Katibu Tawala wa Mkoa wa Kagera Prof Faustin Kamuzora amewataka wazazi na wakazi wa Mkoa wa Kagera kusaidiana na serikali katika kutatua changamoto za walimu.
Hayo ameyasema wakati wa kukabidhiwa ukarabati wa madarasa, madawati na Choo kilichojengwa na Tanzania Commercial Bank (TCB) kitakachosaidia kuboresha mazingira rafiki ya walimu kufundisha.
Prof Kamuzora amesema, wazazi na walezi wengi wa watoto wamesoma katika shule hiyo ila walimu wamekuwa na changamoto ya mazingira ambayo si rafiki na inaweza kupelekea walimu hao kuondoka na kwenda sehemu zingine.
“Walimu hawa wakiondoka tutakosa wa kuwafundisha watoto wetu, nyie wazazi wengi mmesoma hapa na mtu aliyesoma miaka ya nyuma akija hapa atapashangaa ila tusiwaachie serikali peke yake ila tushirikiane pamoja na wadau wa elimu pia,” amesema Prof Kamuzora.
Amesema, Benki ya TCB wamekuja na kujenga choo ila hii isiwe mwisho katika kutoa msaada bali walimu pia wanahitaji elimu ya fedha sababu wengi wamekuwa wanaingia katika mikopo inayowadidimiza kimaslahi.
Aidha, Prof Kamuzora ameitaka elimu ya fedha kuanza kutolewa mashuleni ili wanafunzi waanze kuwa na uelewa mkubwa na itawasaidia baadae.
“Na kwa upande wa walimu, haimaanishi ndio unajua kila kitu nao ni muhimu kuwa uelewa juu ya elimu ya fedha,” Mkurugenzi wa Wateja Wakubwa wa Tanzania Commercial Bank Adolphina William amesema wananchi wa Kijiji cha Msole wameweza kufurahia mradi wa kukarabati madarasa, kukabidhi madawati na walimu kupata choo cha kisasa.
Amesema, mradi huo uliofanyika katika Shule ya Kituga umeweza kugharimu kiasi cha Milioni 36.3 hadi kukamilika kwake.
“Tanzania Commercial Bank imekuwa inatenga fedha kila mwaka kwa ajili ya kusaidia jamii na mwaka huu tumetenga takribani Milioni 500 na kujikita zaidi katika sekta ya elimu na afya,” amesema Adolphina.
Kwa upande wa Mkuu wa shule Hashim kibaiza ameishukuru Tanzania Commercial Bank kwa kufanikisha mradi huo ambao utaenda kuboresha mazingira bora ya walimu katika kuinua taaluma.
Ameomba wadau mbalimbali kuiga mfano kwa Tanzania Commercial Banki ili kuendelea kujikita katika kusaidia jamii ikiwemo shule yao ya Kitunga.
Tanzania Commercial Bank imekabidhi ukarabati wa madarasa mawili, ujenzi wa choo cha walimu pamoja na kuchangia madawati 50 katika shule ya Msingi Kitunga iliyopo Muleba, mkoani Kagera
mradi umegharimu Milioni 36,274,500 pesa za kitanzania.