Katika kuhakikisha Jeshi la Uhifadhi linatekeleza nia njema ya Serikali ya kuhakikisha usalama wa maeneo yaliyotengwa kwa ajili ya uhifadhi wa misitu na wanyamapori nchini, Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) imenunua magari mapya 28 na kusajiliwa kwa namba za jeshi la uhifadhi ili kurahisisha usimamizi wa rasilimali za misitu na nyuki ilizopewa kisheria.
Akizungumza wakati wa zoezi la ugawaji magari hayo mapema hivi leo Kamishna Msaidizi Mwandamizi anayeshughulikia Mahusiano na Umma wa Jeshi la Uhifadhi β TFS, Martha Chassama alisema TFS imepokea magari mapya kumi na tano (15) kutoka Wakala wa Huduma za Ununuzi Serikalini (GPSA) kati ya 28 yaliyonunuliwa katika mwaka wa fedha 2020/2021.
Chassama alisema magari hayo yametoka na namba za jeshi la uhifadhi ambazo Wakala huo umeanza kutumia rasmi mfumo huo mpya wa usajili wa namba hizo kwenye magari yake kama ilivyoelekezwa kwenye Amri za Jumla za Jeshi la Uhifadhi za mwaka 2021.
βLeo tumekamilisha zoezi la ugawaji wa magari haya 15 tuliyopokea kutoka GPSA kwa kuyapeleka katika vituo vyetu mbalimbali vilivyopo nchi nzima Tanzania Bara kwa ajili ya kuimarisha shughuli za uhifadhi na kama mnavyoona gari hizi ni Toyota Land Cruiser Pick Up na Hardtop ni gari za kazi,β alisema Chassama.
Alitaja maeneo magari hayo yanakokwenda kuwa ni Wilaya za Bahi, Chunya, Mufindi, Longido, Rombo, Serengeti, Mlele, Mpanda, Tunduru, Songea, Mvomero, Kibaha na Hifadhi ya Nyuki Manyoni.
Akifafanua kuhusu magari hayo na matumizi ya namba za Jeshi Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Uhifadhi anayesimamia β Utawala (SACC-Admn), Luoga Erasto alisema anaishukuru Ofisi ya Waziri Mkuu kwa kuipa kibali TFS cha kununua magari 28 na Pikipiki 36 ili kuongeza tija katika utekelezaji wa majukumu yake.
Luoga aliongeza kuwa utaratibu wa kubadiri namba za magari, mitambo na pikipiki zote za Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania kwenda kwenye namba rasmi za kijeshi unaendelea na tayari utaratibu ushawekwa na Wizara ya Maliasili na Utalii kuhakikisha taasisi zote zinazounda Jeshi la Uhifadhi Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA), Hifadhi za Taifa (Tanapa), Mamlaka ya Wanyamapori (TAWA) na Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) zinatambulisha magari yao kwa namba za kijeshi.
Credit – Fullshangwe Blog.