Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Uhifadhi -Mawasiliano wa Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA), Pascal Shelutete amesema, Tanzania ni miongoni mwa nchi zinazoshiriki Maonesho ya Utalii nchini Hispania yanayofahamika kama FITUR kuanzia tarehe 19 hadi 23 Januari, 2022.
Shelutete amesema, Maonesho ya Fitur yanayofanyika katika Jiji la Madrid na ni mojawapo ya maonesho makubwa ya utalii duniani na Hispania ni nchi ya 11 kwa kuleta watalii wengi nchini Tanzania.
“Maonesho haya yanafanyika kwa mara ya kwanza kwa kukutanisha nchi mbalimbali baada ya kutofanyika mwaka jana 2021 kutokana na janga la UVIKO-19,”ameeleza Shelutete.
Haya ni maonesho ya siku tano, zenye shughuli nyingi katika maonesho na makongamano ya biashara kimataifa katika sekta ya utalii. Ni siku ambazo kulingana na vivutio vya utalii viliyopo hapa Tanzania zinatoa ishara njema ya kuunga mkono juhudi za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan za kuutangaza utalii wetu Kimataifa.
Ushiriki wa Tanzania katika siku hizi tano ambazo hutafsiri kuwa na mamia ya fursa za kufanya mawasiliano, kuanzisha miradi na kufanya makubaliano pia unawawezesha kufikia wadau wengi kwa wakati mmoja.
Miongoni mwao ni wataalamu walio na kiwango cha juu cha uwezo wa kufanya maamuzi katika sehemu yoyote ya utalii, wenyeviti,mameneja wakuu,wasimamizi wa masoko,mauzo,biashara na wasimamizi wa mauzo na washauri katika sekta ya utalii.
Kupitia FITUR pia, Tanzania kupitia Sekta ya Utalii inajumuika na makundi mbalimbali ya watu ambao utalii ni sehemu ya maisha yao ya kila siku, hivyo kuongeza mawazo mapya na vyanzo vya biashara.
Pia ushiriki wa Tanzania, ni moja wapo ya hatua muhimu kwani maonesho hayo yanaweza kuwatangaza zaidi ikizingatiwa kuwa, kwa mujibu wa waratibu wa maonesho hayo kuna zaidi ya vyombo vya habari 1,170 kutoka kila kona ya Dunia, hivyo ni njia muhimu katika kujitangaza zaidi.
Aidha ushiriki wa Maonesho hao ni njia rahisi ya kufanya mawasiliano mapya na kupanua mtandao wa sekta ya utalii nchini, pili ni kuongeza fursa za biashara na tatu ni kukutana na wauzaji wapya na wateja na kuimarisha uhusiano uliopo wa biashara.
Maonesho haya ya Utalii yanatajwa kuwa moja ya eneo muhimu zaidi la kukutania kimataifa kwa wataalamu na vinara wa masoko kupitia Sekta ya Utalii na yamekuwa yakiwaunganisha pamoja wadau mbalimbali kutoka mataifa mengi yakiwemo ya Amerika Kusini.
Kwa mwaka 2018, makampuni zaidi ya 10,000 yalishiriki katika tukio hilo kubwa, ambalo hutumikia kwa maonesho ya sekta hii.