NA: MWANDISHI WETU.
BAADA ya mdhamini mwenza wa Ligi Kuu ya Wanawake wauzaji wa taulo za kike (Rani Sanitary Pads) kutoa taulo hizo kwa baadhi ya timu zinazoshiriki ligi hiyo, jana ilikuwa zamu ya timu za Mlandizi Queens na Ilala Queens.
Zoezi hilo la ugawaji wa taulo hizo lilifanyika Uwanja wa Karume jijini Dar es Salaam na kuzishuhudia timu hizo zikiumaliza mchezo wao wa ligi hiyo kwa sare tasa, ukiwa muendelezo wa michezo ya ligi hiyo.
Mtendaji Mkuu wa Rani Ramadhan Badi alisema wamekuwa na utaratibu huo na moja ya mipango yao ni kuhakikisha wanatoa taulo hizo kwa timu zote 12 zinazoshiriki ligi hiyo.
Alisema mpaka sasa wameshazifikia timu nyingi katika zoezi hilo na zimebakia timu chache ambazo hawajazipa taulo hizo.
“Huu ndiyo utaratibu wetu tuliojiwekea, tunashukuru kuona tunakwenda vizuri na tumebakisha timu chache ambazo hatujazipa taulo zao.
“Tunaamini tutaifikia kila timu kwa muda wake na baada ya muda kila timu itakuwa imepata taulo zake na tunaamini huo utakuwa mwanzo wa kupunguza changamoto ya taulo hizo wakiwa katika maandalizi ya mechi zao” alisema Ramadhan.
Licha ya hivyo Ramadhani aliwataka wadau wengine kuja katika mpira wa Wanawake kutokana na kuwepo kwa changamoto nyingi.
“Uwepo wetu Rani Sanitary Pads hapa haujafunga milango kwa wadau wengine, taasisi na makampuni kuja kuwashika mikono hawa dada zetu ambao wana changamoto nyingi, hivyo tukiwa watu wengi kama sisi (Rani Sanitary Pads) tutakuwa tumeusogeza sehemu mpira wa dada zetu” alisema Ramadhan
Mpaka sasa Rani Sanitary Pads imeshagawa taulo hizo kwa timu za Simba Queens, JKT Queens, Ruvuma Queens, Oyesterbay Queens, Ilala Queens na Mlandizi Queens.
.