Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi amesema Serikali itazingatia maslahi mapana ya wananchi katika utekelezaji wa mradi mkubwa wa Uwekezaji uliopangwa kufanyika katika eneo la Kizingo, Mkoa wa Mjini Magharibi Unguja.
Dk. Mwinyi amesema hayo wakati alipofanya mkutano na waandishi wa habari kutoka vyombo mbalimbali hapa nchini, mara baada ya kuwasili katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Abeid Amani Karume kufuatia kukamilika kwa ziara yake ya siku tatu ya Kiserikali aliyofanya katika nchi za Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE).
Alisema Serikali inatambua na kuthamini shughuli mbali mbali zinazofanywa na wananchi, ikiwemo Wavuvi katika eneo hilo la Kizingo, hivyo itahakikisha inazingatia namna bora ya kuliendeleza eneo hilo na kuwapatia wazawa maeneo ya michezo, ajira na mafunzo kutokana na mradi utakaowekezwa, sambamba na maeneo mengine ya visiwa ambako miradi mingine ya aina hiyo itafanyika.
Alisema kupitia ziara hiyo kuna Kampuni kubwa zilizoonyesha nia ya kuwekeza hapa nchini na kubainisha sekta tano zitakazofanyiwa kazi, ikiwemo ya ujenzi wa Bandari ya Mangapwani ambayo inahusisha bandari tofauti, ikiwemo ya Mafuta na Gesi.
Kuhusiana na sekta ya Uvuvi, Dk.Mwinyi alisema kuna Wawekezaji watakaoanzisha Viwanda vya kuchakata samaki, hatua itakayokwenda sambamba na harakati zinazofanywa na wananchi katika ufugaji wa samaki.
Alisema katika kuimarisha sekta ya Utalii, kuna Wawekezaji watakaokuja kwa ajili kuanzisha ujenzi wa Kumbi za Mikutano, hatua itakayochochea ujio wa watalii na wageni mbali mbali hapa nchini.