Home LOCAL ONGEZENI VITUO VYA CHANJO: Prof. Abel Makubi

ONGEZENI VITUO VYA CHANJO: Prof. Abel Makubi

Na: WAF – MOROGORO.
Waratibu wa chanjo wa Mikoa  wametakiwa kuongeza vituo vya kutolea huduma za chanjo katika maeneo yao ili kuwawezesha wananchi wengi zaidi kupata huduma za chanjo.

Hayo yamesemwa na Prof.Abel Makubi,Katibu Mkuu Wizara ya Afya wakati akifungua mkutano wa tathimini ya chanjo ngazi ya Mkoa unaofanyika Manispaa ya Morogoro.

Prof. Makubi amesema kuwa  waratibu hao wanapaswa kuongeza vituo hivyo ili wananchi wengi zaidi waweze kujitokeza kupata Chanjo dhidi ya UVIKO-19 na kuwaepusha kufuata nje ya maeneo Yao.

“Dar es Salaam sio watu wa mwisho kwa chanjo lakini mategemeo yetu ni zaidi ya hali ya sasa kwa watu kupata chanjo, mkaongeze vituo na maeneo mengine pia muongeze vituo.”amesisitiza Prof. Makubi

“Sote tunatambua kuwa dunia ilikumbwa na janga la UVIKO19 kuanzia mwaka 2019 na kusababisha watu kuugua na wengine kupoteza maisha duniani na hata hapa nchini kwetu. “Naendelea kuelekeza kila mkoa kufanya bidii kubwa katika kuelimisha na kuhamasisha jamii juu ya umuhimu wa kupata chanjo ili kujikinga na janga hili hatari.”Aliongeza Prof. Makubi

Hata hivyo Prof. Makubi amesema kuwa Kiwango cha uchanjaji kwa UVIKO 19 bado kiko chini sana kitaifa na hivyo kila mkoa ameutaka uongeze kasi ya uchanjaji ili kufikia walau asilimia 60 ya walengwa katika kudhibiti ugonjwa huu.

Kwa upande mwingine Prof.Makubi amesema Wizara yake kupitia mpango wa Taifa wa chanjo imefanikiwa kununua magari 216 ya huduma za chanjo nchini tangu mwaka 2010 hadi sasa.

“Wizara ya Afya inaendelea kutafuta rasilimali za kununua magari ya chanjo na kuyagawa kwa timu za mikoa na wilaya kwa ajili ya usambazaji elekezi.” amesema Prof. Makubi 

Amesema wizara ya Afya kwa kushirikiana na GAVI, UNICEF na CHAI imeendelea kuinua uwezo wa kuhifadhi chanjo kwa ngazi zote nchini hadi sasa imenunua na kufunga vyumba vya baridi (cold rooms) katika Mikoa yote 26 nchini. 

Ameongeza kuwa kwa  mwaka 2019 majokofu 1,385 ya kutunza chanjo yalinunuliwa na kusambazwa wilayani na kwenye vituo vya huduma nchini.

Mkutano huo umehudhuriwa na Wakurugenzi kutoka Wizara ya Afya, OR-TAMISEMI, Meneja Mpango wa Taifa wa Chanjo, Waratibu wa Huduma za Chanjo wa Mikoa, Waratibu wa huduma za Afya ya Uzazi na Mtoto wa Mikoa, Wadau wa huduma za chanjo nchini na Wafanyakazi wa Wizara ya Afya.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here