Home BUSINESS MHE. KIGAHE AWATAKA WAJASIRIAMALI WANAOFANYA BIASHARA KATIKA MAENEO YOTE YA SIDO NCHINI...

MHE. KIGAHE AWATAKA WAJASIRIAMALI WANAOFANYA BIASHARA KATIKA MAENEO YOTE YA SIDO NCHINI KULIPA KODI MARA MOJA KABLA HAWAJACHUKULIWA HATUA KALI ZA KISHERIA.



Naibu Waziri Wizara ya Viwanda na Biashara, Mhe. Exaud Kigahe (Mb) Ameyasema hayo leo alipotembelea ofisi za SIDO Mkoa wa Dar es salaa zilizopo Vingunguti na kujionea shughuli mbalimbali za uzalishaji zinazofanywa na Wajasiliamali waliopo katika eneo moja linalosimamiwa na SIDO.

Mhe. Kigahe amesema kuwa shughuli za ujasiliaamali ndio zinasaidia ajira kwa wingi nchini hivyo SIDO ina jukumu kubwa la kuhakikisha wanawasaidia Wajasiliamali wadogo hasa mpango wa viatamizi (incubation) ambapo wale ambao wamekuwa zaidi wanatoka na kutoa nafasi kwa wengine.

Ameongeza kwa kusema kuwa faida ya wajasiriamali kuzalisha katika eneo linalosimamiwa na SIDO ina faida kubwa kubwa kusaidia wajasiliamali kuzalisha kwa gharama ndogo, kupata usaidizi wa karibu katika teknolojia na mafunzo mbalimbali, miundombinuwezeshi kama majengo na kushirikiana na wajasiliamali wengine waliopo katika eneo moja.



“SIDO inawasaidia wajasirimali wadogo kupata mikopo zaidi ya bilioni nane (8) za mfuko wa NEDF na mifuko mbalimbali mahsusi kwa ajili ya wajasiriamali, Aidha SIDO wameanzisha kituo maalumu cha mafunzo kwa ajili ya wajasiriamali na wakishafuzu mafunzo hayo wanaanza uzalishaji hapahapa.” Amesema Mhe. Kigahe.

Mhe. Kigahe ameagiza wajasiriamali wote wanaodaiwa kodi ya pango katika majengo ya SIDO kote nchini kuhakikisha wanalipa madeni yao wanayodaiwa na SIDO ili kuwezesha ujenzi wa miundombinu ya kufanyia biashara katika maeneo mengine ili kusaidia Wajasiriamali wengi zaidi kupata majengo ya kufanyia shughuli zao.

Naye meneja wa SIDO Mkoa wa Dar es salaam ndugu Ridhiwani Matange amemshukuru sana Naibu Waziri wa Wizara ya Viwanda na Biashara kwa kuwatembelea kwani ni fursa nzuri ya kueleza changamoto wanazokutana nazo ili aweze kuzifikisha katika ngazi za juu.


Bwana Matange ameongeza kwa kueleza changamoto ya bajeti ambapo amesema SIDO haifanyi biashara na inatoa huduma hivyo ni vyema wakaongezewa fedha ambazo zitasaidia shughuli wanazofanya ikiwemo ukarabati wa majengo na ujenzi wa majengo mapya nay a kisasa kwa ajili ya Wajasiriamali wengi zaidi.

Ameongeza kwa kusema pia changamoto nyingine wanayokutana nayo ni kwa Wafanyabiashara wasio waaminifu wamekuwa hawalipi kodi na kulimbikiza madeni makubwa na kudhoofisha utendaji wa SIDO katika Mkoa wa Dar es salaam na maeneo mengine.

Aidha Mkurugenzi wa kiwanda cha “Star Natural Products” kilichopo katika eneo la SIDO Bwana George amefurahi sana kwa ujio wa Mhe. Naibu Waziri na Mkurugenzi Mkuu wa SIDO Mhandisi Prof. Sylivester Mpanduji kwani kuja kwao kunawapa faraja ya kuona serikali ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inayoongozwa na Mhe. Samia Suluhu Hassan imekuwa ikiwajali sana wajasiriamali nchini kwani wamekuwa wakipatiwa mikopo isiyokuwa na vikwazo na kwa kujenga majengo yenye gharama nafuu kwa Wajasiriamali kufanya shughuli zao.

Mwisho.

Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini,

Wizara ya Viwanda na Biashara

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here