Home LOCAL MGANGA MKUU WA SERIKALI DKT. SICHALWE ATAKA KASI YA HAMASA KWA WANANCHI...

MGANGA MKUU WA SERIKALI DKT. SICHALWE ATAKA KASI YA HAMASA KWA WANANCHI KIGOMA ILI KUPATA CHANJO YA UVIKO 19


Na: WAF,  Kigoma.

MGANGA Mkuu wa Serikali Dkt. Aifello Sichalwe amewaelekeza Waganga Wakuu wa Halmashauri na Wilaya na Waratibu wa Chanjo wa Mkoa wa Kigoma kuongeza kasi ya kuhamasisha wananchi ili wapate chanjo ya UVIKO-19. 

Dkt. Sichalwe ametoa maelekezo hayo Januari 27, 2022 alipokutana na kufanya mazungumzo na viongozi wa Afya wa Mkoa wa Kigoma walioongozwa na Mganga Mkuu wa Mkoa huo Dkt. Simon Chacha ikiwa ni sehemu ya mikakati ya Serikali kupitia Wizara ya Afya ya kuwakinga wananchi dhidi ya ugonjwa wa UVIKO-19. 

“Serikali siku zote inapenda kuwalinda wananchi wake, chanjo ni salama, niwaombe wote mwongeze kasi ya kutoa Elimu kwa wananchi na kuondoa maswali yote yanayowatatiza ili kwa hiari wahamasike kwenda kupata chanjo ya UVIKO-19.” Dkt. Sichalwe. 

Kwa upande mwingine Dkt. Sichalwe amesema, mkakati wa  sasa wa Serikali ni kuhakikisha inaboresha hali ya utoaji huduma za afya kwa wananchi ili wanufaike na huduma hizo kwa kiwango kikubwa na kwa muda mfupi. 

Aidha, Dkt. Sichalwe amemwelekeza Mganga Mkuu wa Mkoa kutengeneza daftari litalolenga kupima utendaji kazi wa Waganga Wakuu wa Wilaya na Halmashauri katika maeneo yao ili kuongeza kasi ya utendaji katika Mkoa huo. 

Mwelekeo wa Serikali kupitia Wizara ya Afya ni kuhakikisha utoaji huduma unatolewa kwa viwango vya juu na wenye kuleta tija ili mwananchi aweze kunufaika na huduma hizo, hivyo ni jukumu lenu kama kama viongozi mliopewa dhamana ya kusimamia masuala ya afya mnatekeleza hayo. Alisisitiza Dkt. Sichalwe. 

Mbali na hayo, amewaelekeza Waganga  Wakuu ngazi ya Mkoa na Halmashauri  kuhakikisha wanaboresha suala la uongozi na utawala bora baina ya Watumishi ndani ya Mkoa ili kuleta matokeo chanya katika kuwahudumia wananchi wanaohitaji huduma. 

Hata hivyo, Dkt. Sichalwe amempongeza Mganga  Mkuu wa Mji wa Kasulu Dkt. Peter Luhega kwa jitihada alizofanya katika kutoa hamasa kwa wananchi  wake ili kupata Chanjo hali iliyopelekea kumaliza kwa Chanjo dozi 490 kwa vituo 15 ndani ya siku 20 na kuongeza dozi nyingine ambazo pia zimemalizika. 

Mwisho.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here