Wataalamu wa Wizara ya Maendeleo ya Jamii Jinsia Wanawake na Makundi Maalum wakiongozwa na Waziri mwenye dhamana ya Wizara Mhe. Dkt. Dorothy Gwajima, (Mb) wamefanya ziara ya kwenye Kijiji cha Matumaini kilichopo mkoani Dodoma ikiwa ni mwendelezo wa ziara za kujifunza juu ya mbinu bora zaidi za kutekeleza mpango wa kuwapatia malezi na makuzi stahiki watoto waishio kwenye mazingira magumu.
Dkt. Gwajima amekipongeza kituo hicho na kushuhudia kuwa, amekuwa akisikia Kijiji cha Matumaini ni mojawapo ya vituo vilivyofanikiwa sana katika huduma ya malezi na makuzi ya watoto waishio kwenye mazingira magumu na sasa kituo ambacho kwa sasa kina miaka 20 kwenye huduma hiyo.
Kituo kina watoto wachanga, wanaosoma chekechea, shule ya msingi, sekondari, vyuo vya kati, vyuo vikuu na wengine walishamaliza shule wanaendelea na maisha yao.
“tumekuwa tukishauriana namna gani tunaweza kuboresha maisha ya watoto wanaoishi mazingitra magumu na baadae Katibu Mkuu akaniambia twendeni Kijiji cha Matumaini, tukajifunze kwani hawa wamefanikiwa sana” Dkt. Gwajima.
Dkt. Gwajima amesema, taaluma ya maendeleo na ustawi wa jamii lazima ijikite kwenye kuimarisha msingi wa watoto kuanza safari ya ustawi wa maisha yao tangu kabla ya kuzaliwa na wanapozaliwa na kukua kufikia utu uzima ili waweze kuchangia maendeleo ya taifa kwa tija, hivyo kwa ziara hizi tunazofanya na hatimaye leo kwenye kituo hiki ni Dhahiri safari yetu ya matumaini tunaianzia hapa katika Kijiji chenu” alisema Dkt. Gwajima.
“Hatuwezi kuvumilia kuona watoto ambao katika kipindi wanatakiwa wawe shule hawapo shuleni, katika kipindi wanacho takiwa wawe na wazazi wao wapate upendo wa jamii yao unakuta wapo wanahangaika mtaani, hili halikumpendeza Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan, ndio maana akaamua kuunda Wizara hii hivyo dhamana iliyopo mbele yetu nikuhakikisha tunafanikisha kukinusuru kizazi hiki” alisema Dkt. Gwajima.
Naye Naibu Waziri Mhe. Mwanaidi Khamisi, alisema ziara hiyo ni mwanzo wa kwenda nchi nzima kwa ajili ya kuyafikia makundi yote, ikiwepo Wanawake, Wazee na watu Wenye ulemavu, hivyo akatuma salamu kwa maafisa ustawi wa jamii kujiandaa kwani Dodoma ni Mwanzo wa safari ndefu ya matumaini.
Awali akisoma Risala ya kituo hicho mtoto Apia Aveline, aliyelelewa katika kituo hicho na kusoma hadi kufikia ngazi ya Utabibu, alisema wanakishukuru kituo hicho kwani zimefanikisha ndoto zao kuwa kweli, huku akiiomba Serikali kwa niaba ya Kituo kuangaliwa uwezekano wa kupata msamaha wa kodi wa vifaa vyao vinavyo ingizwa nchini, jambo ambalo Waziri alisema amelichukua na kuahidi kulifanyia kazi.
Kijiji cha Matumaini kilianza mwaka 2002 kikiwa na watoto watatu lakini kimeendelea kukuwa na kufikia sasa kituo hicho kina watoto 145 wakiwepo wavulana 62 na waschana 83 watoto hao wanaishi kwenye Nyumba 13 kwa mtindo wa kifamilia, kila nyumba kuna watoto wa umri tofauti na kutunzwa na Baba na Mama walezi wakujitolea.
MWISHO.