Home BUSINESS KIJAZI AMKABIDHI RASMI OFISI MWAKILEMA, AWAASA WAFANYAKAZI WA TANAPA KUIMARISHA MSHIKAMANO

KIJAZI AMKABIDHI RASMI OFISI MWAKILEMA, AWAASA WAFANYAKAZI WA TANAPA KUIMARISHA MSHIKAMANO


Na: Mwandishi Wetu.

Aliyekuwa Kamishna wa Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA) na ambaye kwa sasa ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Dkt. Allan Kijazi amewataka wafanyakazi wa TANAPA kuendeleza umoja, mshikamano na ushirikiano katika kutekeleza majukumu ya Shirika.

Alitoa wito huo wakati wa hafla fupi ya makabidhiano ya ofisi kwa Kamishna wa Uhifadhi mpya William Mwakilema.


Alisema “Mafanikio yaliyofikiwa kwa upande wa TANAPA yanahitaji kulindwa na kuendelezwa kwa kufanya kazi kwa juhudi, maarifa na kuimarisha mshikamano.”

Alielekeza TANAPA kuongeza bidii katika kuyatekeleza majukumu ya msingi ambayo ni kuendeleza uhifadhi na utalii.
Alitahadharisha kuwepo kwa dalili za ujangili katika hifadhi zetu na kusisitiza kuzilinda maliasili hizi kwa nguvu zote.

Kuhusu utalii, alisisitiza kuongeza bidii ili kuwavutia watalii wa ndani na nje. Ili kufikia lengo hili ni lazima kuboresha miundombinu, kutoa huduma bora kwa watalii na kuendelea kuvitangaza vivutio vyetu.

Naye Kamishna wa Uhifadhi, William Mwakilema alitoa shukrani zake za dhati kwa Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan kwa kumuamini kushika nafasi hii na kuahidi kutekeleza kazi hii kwa dhati na bila upendeleo, chuki wala majungu.

Aliwataka watumishi kuendelea kumpa ushirikiano ili kuendelea kulinda tuzo mbalimbali zilizopatikana hasa za ESQR na ISO.
Mwisho.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here