Na: Costantine James Geita.
Mkurugenzi mtendaji wa mamlaka ya maji safi na usafi wa mazingira (GEUWASA) mkoani Geita Mhandisi Frenk Changawa amempongeza mkuu wa mkoa wa Geita Mhe. Rosemary Senyamule kwa kusimamia kikamilifu kampeni ya kuhamasisha usafi wa mazingira ndani ya mkoa wa Geita.
Alisema hayo wakati wa zoezi la uzinduzi wa kampeni ya usafi wa mazingira mijini Geita aliposhiriki kuungana na Mkuu wa mkoa wa Geita Rosemary Senyamule kwenye zoezi la kuhamasisha usafi wa mazingira ndani ya Geita mji.
“Watu sasahivi wamehamasika kuweka mazingira yao safi sisi kama mamlaka ya maji safi na usafi wa mazingira jukumu letu ni kuhakikisha mazingira kama haya yako salama na safi kwahiyo tunampongeza sana mkuu wa mkoa na tunawapongeza wananchi na watu wote na taasisi zote zilizoshiriki tunaomba zoezi hili liwe endelevu angalau kila mwezi tutenge siku moja ya juma mosi ikiwa mwisho wa mwezi au mwanzo wa mwezi tunashiriki usafi wa pamoja ambao utawahamasisha watu wa chini usafi unaanza na sisi viongozi na watu wengine watatuunga mkono” Alisema Mhandisi Frenk Changawa Mkurugenzi mtendaji wa mamlaka ya maji safi na usafi wa mazingira (GEUWASA).
Mkuu wa Mkoa wa Geita alibainisha kwa kusema kuwa katika kuweka mazingira safi, zaidi ya wafanyabiashara wadogo (machinga) 6500 wamepangwa kwenye maeneo rasmi na Serikali inaendelea kuweka mazingira bora na kuhamasisha machinga wabaki kwenye maeneo hayo.
“Kulikuwa kuna maelekezo ya kupanga machinga katika maeneo maalumu na waondoke maeneo ambayo yalikuwa hayana staha kwao ili wakae maeneo yenye staha tumeshirikiana na viongozi wa machinga jambo hilo limetekelezwa maeneo mbali mbali tumeweza kuwapanga zaidi ya machinga 6500 wako katika maeneo ambayo ni rasimi wanaendelea kufanya biashara zao na tunaendelea kusimamia ili wasirudi maeneo ambayo siyo rasimi” Alisema Rosemary Senyamule Mkuu wa mkoa wa Geita.
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Mji Geita Bi. Zahara Michuzi alifafanua kuwa mwisho wa zoezi la kampeni ya usafi wa mazingira ndio mwanzo wa kufanya shughuli hizi kila wakati kwenye mji wetu wa Geita na amezishukuru taasisi zote zilizoshiriki kuanzia za dini umma na kikundi cha akina mama kwa kufanikisha zoezi hilo.
Mkuu wa Idara ya Usafi na Mazingira Mjini Geita Aloyce Mutayugwa alisema mji wa Geita ulishika nafasi ya 21 nchini Tanzania katika miji iliyo safi zaidi.
“Mwaka jana Mji wetu wa Geita umekua nafasi ya nne kati ya miji 21 nchini tukitanguliwa na Nyombe, Tunduma na Babati kwenye usafi na utunzaji wa mazingira kutokana na muitikio hafifu wa wananchi kwenye zoezi la usafi wa mazingira ila sasa tunakwenda vizuri na tunamshukuru sana Mkuu wa Mkoa na hamasa hili.” Alisema Mkuu wa Idara ya Usafi na Mazingira Mjini Geita, Aloyce Mutayugwa.